test

Ijumaa, 20 Oktoba 2017

CCM yawarudisha kugombea madiwani waliohama Chadema


Chama cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Arusha, kimewateua wagombea wanane wa udiwani, watakaoshiriki uchaguzi mdogo, watatu wakiwa ni madiwani ambao walijiuzulu Chadema ili kumuunga mkono Rais John Magufuli, lakini wakadondoshwa kwenye kura za maoni ndani ya CCM.
 
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shaban Mdoe amesema leo Ijumaa kuwa madiwani hao watapeperusha bendera ya CCM, katika  uchaguzi huo mdogo.

Uchaguzi unafanyika baada ya waliokuwa madiwani wa kata nane kupitia Chadema kuachia ngazi kwa hiyari yao wakiunga mkono jitihada za Rais Magufuli.

Mdoe amesema miongoni mwa waliopitishwa ni madiwani watatu waliojiuzulu udiwani Chadema na kujiunga na CCM kisha kupokelewa na mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli ambapo alishauri vikao vya kikatiba kuwarejesha katika nafasi zao kama bado wanazo sifa.

Madiwani waliokuwa Chadema na kujiuzulu ambao walishindwa kura za maoni ndani ya CCM na jana kupitishwa ni Japhet Joseph Jackson (Ambureni), Anderson Sikawa (Leguruki) na Solomon Laizer (Ngabobo).

Mdoe amesema katika kikao hicho cha leo makada wengine walioteuliwa kupeperusha bendera ya CCM na majina ya kata zao katika mabano ni pamoja na Francis Mbise (Muriet) iliyopo katika jiji la Arusha, Flora Zelothe (Mussa) iliyoko wilayani Arumeru.

Wengine ni pamoja na Prosper Damuni MeyanI (Moita), iliyoko wilayani Monduli, Samson Laizer (Makiba) na Yona Kaaya (Maroroni) halmashauri ya Meru.
 
Amesema katika kikao hicho wajumbe wote na kwa kauli moja walikubaliana kuhakikisha ushindi unapatikana kwa chama cha mapinduzi na kuzitwaa kata hizo ambazo zilikua zikishikiliwa na madiwani wanaotokana na Chadema.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni