NAIBU
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha, amesema
Serikali ya awamu ya tano imeanza kurejea katika mtazamo wa Mwalimu
Julius Nyerere juu ya uchumi wa viwanda aliouanzisha.
Akizindua
Kongamano la Kumbukumbu ya Kifo cha Mwalimu Nyerere lililofanyika
katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam
juzi, Ole Nasha alisema Mwalimu Nyerere alijenga viwanda vingi hapa
nchini.
Alivitaja
viwanda ambavyo Mwalimu Nyerere alivijenga kuwa ni viwanda vya nguo
kama Urafiki, Mbeya Tex, Mwatex, Mutex, viwanda vya ngozi, viwanda vya
zana za kilimo, viwanda vya kutengeneza vipuli pamoja na viwanda
vinavyotegemea malighafi za mazao yanayolimwa hapa nchini.
Alisema
Taifa linahitaji viongozi wazalendo na waadilifu kama alivyo Rais Dk.
John Magufuli ambaye ameonesha nia ya dhati ya kufuata nyendo za Mwalimu
Nyerere kwa kuhimiza maendeleo ya kiuchumi yanayotegemea viwanda.
“Serikali
ya awamu ya tano kwa muda wa miaka miwili iliyokaa madarakani,
imejitahidi kurejea na kuweka kwenye vitendo dhana ya Mwalimu Nyerere ya
uchumi wa viwanda, kwani kwa sasa inatekeleza Mpango wa Pili wa
Maendeleo wa Taifa, mwaka 2016/2017-2020/2021 unayojikita katika ujenzi
wa viwanda kama njia ya maendeleo ya kiuchumi na maisha ya
watu,”alisema Ole Nasha.
Alisema
mtazamo wa Mwalimu Nyerere ulikuwa ni kutumia viwanda vya ndani kama
njia ya kujinasua kutoka kwenye unyonyaji wa muda mrefu.
Kama
Taifa huru kuna haja ya kuondoa tofauti za kisiasa na kuishi katika
misingi ya usawa, umoja, ushirikiano ili kujiletea maendeleo ya uchumi
kwa mtu mmoja na taifa kwa ujumla, ikiwemo kuhimiza uzalendo kwa kila
mtanzania ili kujenga Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo
2025.
Kwa
upande wake Mkuu wa Chuo cha Kumbumbuku ya Mwalimu Nyerere, Profesa
Shadrack Mwakalila, alisema kuwa ili kufikia Tanzania ya viwanda taifa
linahitaji viongozi wazalendo wenye uchu wa maendeleo na wasio na
misingi ya ukabila wala udini.
“Mwalimu
Nyerere aliwahi kusema kuwa, ili tuendelee tunahitaji vitu vinne
ambavyo ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora, hivyo ustawi wa
uchumi wa viwanda unahitaji viongozi na watendaji ambao ni wazalendo,
watiifu na wenye kutanguliza mbele masilahi ya taifa,”alisema Profesa
Mwakalila.
Kongamano
la maadhimisho ya siku ya Mwalimu Nyarere hufanyika kila mwaka ili
kujadili busara, fikra na hekima zake katika kujenga usawa, maendeleo,
umoja na ustawi wa uchumi wa taifa letu.
Maadhimisho
ya mwaka huu ni ya 18, tangu Mwalimu Nyerere afariki mnamo Oktoba 14,
1999, ambapo kauli mbiu ya kongamano la mwaka huu inasema “Mtazamo wa
Mwalimu Nyerere katika Uchumi wa Viwanda na Maendeleo ya Jamii”.
Maadhimisho hayo yatafanyika visiwani Zanzibar ambapo shughuli ya kuzima mwenge wa uhuru itafanyika.
0 comments:
Chapisha Maoni