Wakati
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli imejipambanua
kuongeza vitega uchumi kama vile ununuzi wa ndege mpya aina ya
bombardier, Chadema wameibuka na uchambuzi wa hali ya uchumi na kudai
hali sasa ni tete ukilinganisha na awamu iliyopita.
Jana,
Chadema ilitoa tamko la tathmini ya hali ya uchumi nchini baada ya
kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kukutana kwa dharura kwa siku mbili
mfululizo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
na wanahabari, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alisema tamko
hilo limejikita katika ripoti ya hali ya uchumi inayotolewa kila mwezi
na Benki Kuu Tanzania (BoT) kama ilivyotolewa Julai 14, 2017.
Alisema Julai 14, BoT ilitoa ripoti ya Juni inayohusu tathmini ya Mei.
Kwa
kuzingatia umuhimu wake, alisema Chadema imefanya uchambuzi wa ripoti
hiyo kwa kuangalia hali ya uchumi mpaka kufikia Mei 2017 ikilinganishwa
na hali ya uchumi iliyokuwapo Mei 2015 ikiwa ndio mwaka wa mwisho wa
Awamu ya Nne ili kuona mwelekeo wa hali ya uchumi na athari zake chanya
au hasi kwa mustakabali wa Taifa.
Hata
hivyo, alipoulizwa kuhusu madai ya Chadema kuhusu kuporomoka kwa uchumi
wa Tanzania, Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu hakuwa tayari
kuzungumzia suala hilo kwa madai kwamba yuko kijijini na hajui
kinachoendelea.
“Mimi
nataka nikiongelea kitu niwe ninakifahamu vizuri, hilo suala
sijalisikia kwa hiyo siwezi kusema chochote kupitia mtu wa tatu,” alisema Profesa Ndulu akisisitiza kwamba kwa sasa hayupo ofisini.
Lakini,
Mbowe ambaye aliambatana na viongozi waandamizi wa chama hicho akiwamo
Katibu Mkuu, Dk Vincent Mashinji na Mjumbe wa Kamati Kuu, Edward Lowassa
alisema uchumi hupimwa kwa vigezo vingi na umuhimu wa vigezo husika
huwa na maana kutegemeana na namna vinavyoathiri maisha ya wananchi.
Katika uchambuzi wao, waliangalia vigezo vichache ambavyo vina uhusiano
wa moja kwa moja kwenye maisha ya wananchi.
Mbowe
alisema kwa kipindi cha Mei, 2015 kiasi cha akiba ya chakula kwenye
Ghala la Taifa (NFRA) kilifikia tani 406,846 ukilinganisha na akiba ya
tani 74,826 ilipofika Mei 2017, sawa na asilimia 18.3 tu ya kiasi cha
chakula katika kipindi kama hicho mwaka 2015.
“Bei
za jumla kwa vyakula muhimu kama mahindi, Mei 2015 ilikuwa Sh47,163 kwa
gunia wakati mwaka huu mwezi kama huo ilifikia Sh90,149.9 sawa na
ongezeko la bei kwa asilimia 92 wakati mchele gunia mwaka 2015 ilikuwa
Sh162,701 na mwaka huu mwezi kama huo ilifika Sh176,330,” alisema Mbowe.
Mwanasiasa
huyo aliongeza kuwa mazao mengine yote ya chakula ikiwamo maharage,
viazi na sukari nayo yamepanda bei kwa wastani wa asilimia kati ya 40 na
60 kutegemea na msimu.
Mbowe
alisema kuwa sekta hiyo imekua kwa asilimia 1.7 pekee mwaka 2016/17,
kiwango ambacho ni cha chini kupata kutokea kwa zaidi ya miongo mitatu.
“Wakati
mataifa yote duniani yanasaidia wakulima kuongeza tija katika kilimo
kwa kuwasaidia ruzuku ya mbolea, Tanzania ambayo asilimia 75 wanategemea
kilimo mwaka 2015 ilikuwa Sh78 bilioni wakati mwaka 2016/17 ruzuku hii
ilikuwa Sh10 bilioni tu,” alisisitiza Mbowe.
Alisema
kwa upande wa tume ya maji iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria 2015 kwa
lengo la kuhakikisha wanaongeza kilimo cha umwagiliaji katika bajeti ya
mwaka 2016/17, ilipata Sh 0 (sifuri) katika bajeti yake ya maendeleo.
Mwenyeiti
huyo ambaye aliwahi kugombea urais kwa tiketi ya chama chake na
kushindwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete alisema wakati bei zikiwa juu
sasa kuliko mwaka 2015 kabla ya Awamu ya Tano kuingia madarakani, hali
ya ujazo wa fedha imekua kinyume chake na hivyo kuathiri biashara,
uzalishaji, thamani ya mali kama ardhi huku ujazo wa fedha katika dhana
pana kwa mwaka kwenye uchumi uliongezeka kwa asilimia 15 Mei 2015
ukilinganisha na ongezeko la asilimia 5.2 Mei mwaka huu.
Alisema
kwa upande wa mzunguko wa fedha kwa maana ya kiasi cha fedha katika
matumizi kwa mwaka, inaonyesha Mei 2015 kiliongezeka kwa asilimia 15.2
wakati 2017 kilikuwa na ongezeko hasi kwa asilimia tatu.
“Hiki ni kielelezo cha usimamizi hafifu wa uchumi na ndio msingi wa ukata unaoendelea nchini.”
Alisema
athari za kushuka kwa ujazo wa fedha na mzunguko wa fedha kwenye uchumi
katika vipindi hivyo tofauti wakati kiasi cha mfumuko wa bei kikiwa na
tofauti ndogo, kwa maana kutoka asilimia tano mwaka 2015 mpaka asilimia
sita 2017 ni pamoja na fedha kuwa vigumu kupatikana japo inashuka
thamani.
“
Ndio maana pamoja na mwaka 2017 fedha kuwa ngumu kuliko mwaka 2015 kwa
mujibu wa takwimu hizi za BoT, lakini thamani ya bei ya chakula kama
mahindi na maharage vimepanda karibu mara mbili kwa ulinganisho wa miaka
hiyo miwili,” alisisitiza.
Mwenyekiti
huyo alisema pia kuwa gharama ya uzalishaji kwa sehemu kubwa inabaki
kuwa juu kwa sababu bidhaa za mtaji na mashine sehemu kubwa zinanunuliwa
nje na hivyo bei yake haiamuliwi na hali ya ndani kwa sababu wateja
kipato kimeshuka, soko la bidhaa zinazozalishwa hushuka na kusababisha
mdororo wa biashara.
Alisema
kwa sababu ya mdororo wa biashara, wafanyabiashara wanashindwa kulipa
mikopo na hivyo kuongeza presha kwenye kasi ya mikopo isiyolipika (non
performing loans -NPL).
Alisema
mpaka sasa kwa mujibu wa ripoti mbalimbali mikopo isiyolipika
imeongezeka kutoka chini ya asilimia tano mwaka 2015 mpaka asilimia
zaidi ya nane mwaka 2017 jambo alilodai kuwa linapunguza imani ya benki
za biashara kukopesha sekta binafsi.
Alisema
ukata huo unasababisha kushuka kwa thamani ya mali kama ardhi, nyumba
au mashine na mitambo iliyowekwa dhamana benki kwa ajili ya kupata
mikopo kwa sababu uwezo wa watu kununua umeshuka.
“Ndiyo
sababu viwanja ambavyo viliuzwa Sh100 milioni sasa ukitangaza bei ya
Sh50 milioni hupati mteja, gari au mashine ambayo mwaka 2015 ungeuza kwa
Sh50 milioni leo huwezi kupata nusu yake kwa sababu ya ukata.”
Alisema
pia uwezo wa Serikali na watu kujitegemea unapungua kwa sababu wigo wa
makusanyo unapungua kutokana na biashara nyingi na ajira kupotea.
“Kwa
sababu hiyo, maamuzi ya kisera na kisheria ya kushinikiza kampuni za
simu zilizoorodheshwa soko la mitaji (DSE) yamekuwa na mafanikio hafifu
hata kuhitajika kubadilisha sheria kwa sababu sera mbovu za kiuchumi
zimepunguza uwezo wa Watanzania kutumia fursa hizo kuwekeza. Ndio sababu
majuzi kampuni ya Vodacom imejaribu kuongeza muda kuwa ipo pamoja na
sasa kuruhusu wasio wazawa kununua hisa hizo,” alisema mbunge huyo wa Jimbo la Hai.
Serikali Yajibu Mapigo
Akizungumzia
tuhuma za Chadema kuhusu hali ya uchumi, Msemaji wa Serikali, Dk Hassan
Abbas alihoji tuhuma hizo kwamba haziendani na hali halisi ipi wakati
wanafunzi wanasoma bure hadi kidato cha nne?
Dk Abbas aliwashangaa Chadema kwa kusema;
“hawaoni miradi mikubwa ya ujenzi inayoendelea kama vile barabara,
mradi wa umeme wa Kinyerezi II Dar es Salaam, flyover ya Tazara na
ununuzi wa ndege.
“Serikali
inaajiri wafanyakazi wapya; inalipa mishahara kwa wakati; miradi ya
maji inaendelea nchi nzima ikiwemo mikubwa ya kutoa maji Ziwa Victoria,”
alifafanua Dk Abbas.
Alisema
Serikali imeongeza makusanyo ya mapato na imeongeza bajeti katika
huduma za jamii, kama vile afya hasa kwenye ununuzi wa dawa. Na kwamba
hata wabunge wa Chadema wakiwa bungeni wanalipwa posho zao kama kawaida.
“Wanataka uhalisia upi zaidi ya ushahidi huu kuwa uchumi wa nchi unafaidisha wananchi kupitia huduma hizo?" alihoji Dk Abbas .
Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole yeye alisema chama chake
hakina muda wa kulumbana na kwamba sasa wana kazi ya kuwaletea
maendeleo wananchi.
“Sisi
tuna mkataba na wananchi wa Tanzania kuhakikisha tunawaletea maendeleo,
kwa sasa tupo ‘busy’ kufanya kazi hiyo, kiukweli hatuna muda wa kufanya
malumbano yasiyo na tija, tunachojua ni kazi kubwa iliyopo mbele yetu
ambayo tumesaini mkataba mpaka mwaka 2020.”
“Hatuna
muda wa kuhangaika na watu wasio na dhamira njema, tunaendelea na kazi
na matunda yake yatawanufaisha wananchi wa kawaida kabisa ambao ni
wakulima, wafanyabiashara na wafanyakazi. Sisi hatuna muda wa kupoteza,”alisisitiza Polepole
0 comments:
Chapisha Maoni