WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe alifanyie mapitio Baraza la Michezo
Tanzania (BMT) na iwapo hatoridhika na utendaji wake alivunje.
“Ninamuagiza
Waziri mwenye dhamana kufanya mapitio na kutathmnini upya utendaji kazi
wa Baraza la Michezo Tanzania juu ya usimamizi wake wa michezo nchini
na kama hataridhika, anayo mamlaka ya kulivunja Baraza hilo.”
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Julai 5, 2017) katika hotuba yake
ya kuahirisha Mkutano wa Saba wa Bunge mjini Dodoma.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano haitafumbia macho usimamizi mbovu na utawala wa michezo usiojali maslahi ya Taifa. “Serikali imeazimia kuimarisha utendaji kwa vyombo vya michezo nchini ili kila mwenye dhamana awajibike ipasavyo.”
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu ameipongeza timu ya vijana walio chini ya
umri wa miaka 17, Serengeti Boys iliyoshiriki na kutoa upinzani mkubwa
kwenye mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika.
Amesema
licha ya timu hiyo kumaliza ikiwa na jumla ya pointi 4 sawa na timu
iliyoshika nafasi ya pili, ila Vijana hao wameonesha vipaji na uzalendo
wa hali ya juu kwa nchi yao.
“Msisitizo
wangu kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni kuendelea
kuwatunza vijana hao, na kusimamia vilabu vya michezo nchini kuwekeza
kwenye soka la vijana ili tujenge timu imara kwa miaka michache ijayo.”
Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua umuhimu wa michezo kwa afya, umoja wa kitaifa na kama fursa ya ajira kwa vijana nchini.
“Wiki
iliyopita, mkoani Mwanza yamehitimishwa mashindano ya UMISSETA na
UMITASHUMTA. Wananchi wa Mwanza na Watanzania kwa ujumla wamejionea
uwezo wa kimichezo, vipaji na hamasa kubwa iliyopo miongoni mwa vijana
wetu kutumia vipaji vyao. “
Amesema Serikali itaendelea kuratibu michezo shuleni, ikiwa ni pamoja na kusimamia ufundishaji wa michezo kama somo. “Maelekezo
yetu ni kwamba kila Mkoa uwe na shule angalau mbili zenye mchepuo wa
michezo na walimu wenye sifa stahiki za kufundisha michezo.”
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini,
wahakikishe kwamba kila shule inakuwa na viwanja vya michezo mbalimbali
ili kuwapa fursa wanafunzi kushiriki michezo ili kupandisha na kuinua
vipaji vyao.
Pia
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John
Magufuli kwa kuunga mkono jitihada za michezo nchini kwa dhamira yake ya
kujenga uwanja mkubwa wa michezo mjini Dodoma kwa kushawishi mataifa
rafiki kama vile Morocco ambao wanajenga uwanja huo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
0 comments:
Chapisha Maoni