WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haina mpango wa kuanzisha maeneo
mapya ya utawala hadi ikamilishe kuboresha miundombinu kwenye maeneo
iliyoyaanzisha.
“Ili
kutimiza azma hiyo, Serikali katika mwaka wa fedha 2017/2018 imetenga
kiasi cha shilingi bilioni 412.38 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kati
ya fedha hizo, Serikali imetenga shilingi bilioni 16.985 kwa ajili ya
kuboresha miundombinu ya majengo ya ofisi na makazi ya viongozi katika
mikoa yote mipya,” amesema Waziri Mkuu.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Julai 5, 2017), bungeni mjini
Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa saba wa Bunge la 11.
Bunge limeahirishwa hadi Septemba 5, mwaka huu.
“Katika
mgawo huo, mkoa wa Njombe umetengewa jumla ya shilingi bilioni 3.34;
mkoa wa Katavi umetengewa jumla ya shilingi bilioni 3.080; mkoa wa
Simiyu umetengewa jumla ya shilingi bilioni 3.775, mkoa wa Geita
umetengewa jumla ya shilingi bilioni 2.978 na mkoa wa Songwe umetengewa
jumla shilingi bilioni 3.812,” amesema.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imetenga jumla ya shilingi
bilioni 61.7 kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri 64
ambapo kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 28.7 ni kwa ajili ya
kukamilisha majengo ya ofisi katika Halmashauri 44 na shilingi bilioni
33 ni kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri mpya 20.
Sambamba
na hatua hizo, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Wazee na Watoto imetoa vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuboresha huduma za
afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa vyenye thamani ya shilingi
bilioni 2.9 pamoja na kununua magari ya kubebea wagonjwa katika
Halmashauri 67.
Waziri
Mkuu amesema miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja
na kuendeleza juhudi za ugatuaji wa madaraka kwenda katika Mamlaka za
Serikali za Mitaa pamoja na kuongeza mgawo wa fedha za ruzuku ya
maendeleo inayopelekwa kwenye vyombo hivyo.
Amesema
Serikali inachukua hatua hizo ili kuhakikisha kuwa Mamlaka za Serikali
za Mitaa nchini zinatimiza malengo ya kuanzishwa kwake kwa mujibu wa
Ibara ya 145 na 146 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
0 comments:
Chapisha Maoni