Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli jana
tarehe 24 Julai, 2017 ameweka jiwe la msingi katika miradi mikubwa
miwili ambayo ni mradi wa maji kutoka ziwa Victoria kwenda miji ya
Tabora, Igunga na Nzega na mradi wa ukarabati na upanuzi wa uwanja wa
ndege wa Tabora, na amefungua barabara mbili za Tabora – Nyahua na
Tabora – Puge – Nzega.
Mradi
wa maji kutoka ziwa Victoria utatekelezwa kwa muda wa miezi 30 kwa
gharama ya Shilingi Bilioni 600 ikiwa ni Mkopo kutoka Serikali ya India
na utazalisha takribani lita Milioni 80 za maji kwa siku kwa ajili ya
wakazi wa Tabora ambao kwa sasa wanahitaji lita Milioni 36 na pia
utamaliza tatizo la maji katika miji ya Igunga, Nzega, Tinde, sehemu ya
Wilaya ya Uyui, Shinyanga Vijijini na Vijiji 89 vilivyo kando ya mabomba
ya mradi huo.
Mradi
wa ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Tabora unatarajiwa
kukamilika katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu kuanzia sasa na ni
miongoni mwa miradi inayotekelezwa kwa awamu tatu katika Mikoa ya
Bukoba, Kigoma, Tabora na usanifu wa viwanja vingine 11 katika Mikoa
mbalimbali nchini kwa gharama ya Shilingi Bilioni 69.7.
Barabara
ya lami ya Tabora – Nyahua yenye urefu wa kilometa 85 imejengwa kwa
gharama ya Shilingi Bilioni 123.773 na barabara ya Tabora – Puge – Nzega
yenye urefu wa kilometa 114.9 imejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni
160.515, fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Baada
ya kuweka mawe ya msingi na kufungua miradi hiyo, Mhe. Rais Magufuli
aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli alifanya mkutano wa hadhara
katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Mjini Tabora ambapo aliipongeza
Wizara ya Maji na Umwagiliaji na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano kwa kutekeleza miradi hiyo, na pia alimuomba Balozi wa India
hapa nchini Mhe. Sandeep Arya kumfikishia shukrani zake na za
Watanzania kwa Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi kwa kutoa mkopo
wa Shilingi Bilioni 600 kwa ajili ya kufanikisha mradi huo wa maji na
pia kutoa fedha nyingine Shilingi Trilioni 1.2 kwa ajili ya kutekeleza
miradi mingine 17 hapa nchini.
Mhe.
Rais Magufuli alimtaka Mkandarasi anayejenga mradi wa maji kutoka ziwa
Victoria kuharakisha kazi hiyo na kuikamilisha kabla ya miezi 30 ili
wananchi wa Tabora na maeneo yanayosubiri maji ya mradi huo waanze
kunufaika mapema na pia ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano kuongeza urefu wa njia ya kurukia ndege ya uwanja wa Tabora
kutoka kilometa 1.9 waliyopanga hadi kufikia kilometa 2.5 na kujenga
jengo kubwa zaidi la abiria litakaloweza kuchukua abiria laki 5 kwa
mwaka badala ya abiria 50,000 kama ilivyopangwa hali itakayouwezesha
uwanja huo kupokea ndege kubwa na ndogo.
Mhe.
Rais Magufuli amewahakikishia wananchi wa Tabora kuwa Serikali yake
imejipanga kutekeleza ahadi alizotoa ikiwemo kujenga reli ya kati kwa
kiwango cha kisasa (Standard Gauge) itakayoanzia Dar es Salaam –
Morogoro – Dodoma – Tabora hadi Kigoma ili kurahisisha usafiri na kukuza
biashara ya ndani na nje ya nchi na amewataka wote waliojenga majengo
katika hifadhi ya reli kujipanga kuondoa majengo yao kwa hiari kwa kuwa
Serikali haitawalipa fidia yoyote.
Kuhusu
kero mbalimbali ambazo wananchi wengi wamekuwa wakitaka kumweleza Rais
katika mikutano na kwa kutumia mabango Mhe. Dkt. Magufuli aliwaagiza
viongozi wa Mikoa na Wilaya kutenga muda kila wiki kwa ajili ya
kusikiliza kero hizo na ameonya kuwa kuendelea kwa vitendo hivyo
kunaashiria kuwa viongozi wa maeneo husika hawatekelezi wajibu wao
ipasavyo.
Pamoja
na Mawaziri Prof. Makame Mbarawa Mnyaa na Mhandisi Gerson Lwenge
mkutano huo umehudhuriwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Miundombinu Prof. Norman Sigalla King na Wabunge wa Mkoa wa Tabora ambao
walimtaka Mhe. Rais Magufuli kutokatishwa tamaa na watu wanaobeza
juhudi kubwa anazozifanya kuwapigania Watanzania, na wamemhakikishia
kuwa Wabunge wote wenye nia njema na Tanzania wataendelea kumuunga mkono
katika dhamira yake ya kuijenga Tanzania Mpya.
Leo
tarehe 25 Julai, 2017 Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake
Mkoani Singida ambako atafungua mradi wa barabara ya Manyoni – Itigi
yenye urefu wa kilometa 89.3
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Tabora
0 comments:
Chapisha Maoni