Mkuu wa
Wilaya ya Geita, Herman Kapufi
Mauaji ya walinzi mkoani Geita yamendelea kuwa tishio kwa usalama wao baada ya mlinzi mwingine aliyekuwa akilinda maduka yapatayo 15, kuuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani.
Mauaji ya walinzi mkoani Geita yamendelea kuwa tishio kwa usalama wao baada ya mlinzi mwingine aliyekuwa akilinda maduka yapatayo 15, kuuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani.
Mauaji ya mlinzi huyo Kisusi Iddy (40) aliyekuwa
akilinda maduka hayo kwenye Mtaa wa Mwatulole, ni muendelezo wa matukio
ya kuuawa walinzi wa maduka na mali mbalimbali kwani katika kipindi cha
miaka miwili jumla ya walinzi 20 wameuawa.
Taarifa
zilizopatikana jana kuhusu mauaji ya mlinzi huyo na kuthibitishwa na
mwenyekiti wa mtaa huo, Fikiri Toi zilieleza kuwa tukio hilo lilitokea
usiku wa kuamkia Januari Mosi na wauaji hao hawakuiba kitu chochote.
Mwili wa Iddy ulikutwa umefunikwa kwa shuka lake alilokuwa akilitumia
lindoni, huku likiwa limetapakaa damu.
Kutokana na tukio hilo, Mkuu wa
Wilaya ya Geita, Herman Kapufi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Ulinzi na Usalama amefuta vibali vyote vya waganga wa tiba za asili kwa
madai wao ni moja ya chanzo cha imani za kishirikina zinazosababisha
mauaji hayo.
Alisema kutokana na kukithiri kwa mauaji hayo, mamlaka yake
inakusudia kufufua Jeshi la Jadi (Sungusungu) ili kusaidia kuyadhibiti.
Hata hivyo, Kapufi alisema uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa wakati wa
uhai wake, Iddy alikuwa analinda maduka ya wafanyabiashara yanayofikia
15 na kwamba baada ya kufuatilia, hakuwa na mafunzo yoyote ya ulinzi.
Aliyepigwa na wafugaji Moro afariki
Fabian Bago (21) anayedaiwa kushambuliwa na wafugaji katika Kijiji cha Kolelo, Morogoro, amefariki dunia
katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro alikokuwa akipatiwa
matibabu.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Frank Jacob alisema kijana
huyo alifariki dunia saa 11 jioni jana akiwa kwenye wodi ya wagonjwa
wanaohitaji uangalizi wa karibu na kwamba mwili wake umehifadhiwa
kusubiri taratibu nyingine za kipolisi.
Dk Jacob alisema mara baada ya
kufikishwa hospitalini hapo, kijana huyo alifanyiwa vipimo na matibabu
lakini alifariki dunia kutokana na majeraha makubwa kichwani
yaliyoharibu sehemu ya ubongo.
Baba mzazi wa kijana huyo, Alan Bago
alisema ameshatoa taarifa polisi kuhusina na kifo cha kijana wake na
sasa anasubiri maelekezo ya polisi ili aweze kuendelea na taratibu za
mazishi.