WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itawashughulikia watu wote
wanaotoa matamshi ya kichochezi nchini bila ya kujali nyadhifa zao.
Amesema ni vema watu wakawa makini na kijiepusha kutoa matamshi ambayo yataathiri mfumo wa maisha kwa wananchi wengine.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Jumatano, Julai 19, 2017) wakati wa ibada
ya mazishi ya mke wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt.
Harrison Mwakyembe Bibi Linnah Mwakyembe iliyofanyika wilayani Kyela.
Alisema
Serikali haitavumilia kuona baadhi ya watu wakitoa matamshi ambayo
hayana tija kwa jamii na badala yake yanalenga kuwavuruga wananchi na
kuchochea migogoro.
”Tutashughulika
na watu wote wanaotoa matamshi ya kichochezi, popote walipo bila ya
kujali uwezo wao, vyeo vyao na mamlaka walizonazo.”
Pia aliwaomba viongozi wa dini waendelee kuliombea Taifa na viongozi wake na kwamba Serikali inawategemea na iko pamoja nao.
Waziri
Mkuu alitoa kauli hiyo baada ya Askofu wa Kanisa la Evarinjerical
Brother Hood, Rabison Mwakanani kuonya vitendo vya baadhi ya watu
kumtukana Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli.
Alisema ni vema watu hao wakajifunza namna ya kuwasilisha hoja zao bila ya kutumia lugha za matusi.
“Rais
Dkt. Magufuli amefanya mambo mengi makubwa kwa ajili ya maendeleo.
Wanaofanya hivyo wasidhani kama wanamtukana Rais tu bali wanawatukana
Watanzania wote waliomchagua wakiwemo viongozi wa dini.”
Pia
aliwaomba wananchi kufanya maandalizi mapema kwa sababu wote ni
wapitaji, hivyo waandae roho zao kwa kuacha kufanya dhambi na maovu yote
ili wawe na mwisho mwema.
Vile
Vile Waziri Mkuu aliwaomba wananchi wote washirikiane kwa pamoja
kumuombea Dkt. Mwakyembe na familia yake ili Mwenyezi Mungu aweze
kuwafariji katika kipindi hiki kigumu.
“Wajibu
wetu sote ni kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali
pema. Tunajua kwa sasa Dkt. Mwakyembe yuko katika wakati mgumu,
namuhakikishia kwamba hayuko peke yake kwani Serikali iko pamoja naye
katika kipindi hiki kigumu.”
Naye,
Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai alimpa pole Dkt. Mwakyembe huku
akiitaka familia kuendelea kuwa na upendo kama ule uliokuwepo wakati wa
uhai wa marehemu Bibi Linnah.
Kwa
upande wake, Mtoto mkubwa wa marehemu, George Mwakyembe alisema
anaamini mama yao, alijiandaa na kifo hicho kwa kuwa alikuwa mchamungu.
“Mama
alikuwa na ratiba kila siku ifikapo saa nne usiku lazima afanye ibada,
Hivyo nina matumaini makubwa kupitia Uchamungu wake, Mwenyezi Mungu
atamuweka mahala pema.”
0 comments:
Chapisha Maoni