Wakati
diwani wa saba wa Chadema akijiuzulu jana, Mwenyekiti wa chama hicho,
Freeman Mbowe amesema hata yeye kama angekuwa na moyo mwepesi na mpenda
fedha, angekuwa ameshahama upinzani.
Mbowe
alisema jana kwamba kuwa kiongozi wa upinzani awe mbunge, diwani, au
mwenyekiti wa mtaa, kunahitaji roho ngumu na kwamba hiyo si kazi ya watu
wenye kupenda fedha, bali ni ya maumivu, kudhalilishwa, kunyimwa
ushirikiano, kufungwa wakati wowote na kunahitaji msimamo wa hali ya
juu.
“Upinzani
ni wito, wenye roho nyepesi hawawezi, kama ningekuwa napenda fedha,
nina roho nyepesi, ningeshachukua hizo pesa na ningeshakimbia kabisa
upinzani,” alisema.
Mbowe
amesema hayo wakati chama hicho kikipitia misukosuko ya madiwani wake
wa Mkoa wa Arusha kukihama na jana ilikuwa zamu ya Diwani wa Ambuleni,
Arumeru, Japhet Jackson.
Diwani
huyo aliwasilisha barua yake ya kuhama Chadema kwa Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri ya Meru, Christopher Kazeri jana mchana pia kama wenzake
sita, akisema anamuunga mkono Rais John Magufuli.
Diwani
wa karibuni kujiuzulu wa Ngobobo, Solomon Laizer pia wa wilaya hiyohiyo
katika jimbo linaloongozwa na Joshua Nassari wa Chadema.
Akizungumza
kwa simu jana, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai alisema wanaowania
nafasi za uongozi na viongozi wa Chadema wanahitaji kuwa na msimamo wa
hali ya juu.
“Mara
nyingi wanaowania nafasi kwa upande wa upinzani, ni wale waliokomaa,
lakini katika uchaguzi uliopita, chama kilichopata watu wengi ni
Chadema. Kutokana na mfumo huo wa kuwafungulia milango, wakaingia wengi,
mbu, mende na mambo mengine,” alisema.
Kiongozi
huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alidai kwamba kuondoka kwa
madiwani hao wa Chadema kunasababishwa na baadhi ya watendaji wa
Serikali hasa wakuu wa wilaya ambao wanataka kumfurahisha Rais.
“Inashangaza
kuona wote wanaojiuzulu wanatoa kauli moja ya kumsifu Magufuli, ina
maana hawana sababu nyingine labda pengine Chadema kuna matatizo, sera
zao mbovu, kuna hiki na hiki hakijakaa sawa,” alisema.
Aliongeza
kuwa juhudi za kuwarubuni viongozi wa Chadema zipo katika majimbo yote
ya Chadema na juhudi hizo zinapata nguvu zaidi mahali ambako kuna mkuu
wa wilaya dhaifu ambaye anatumia nguvu za ziada.
Alisema wamebaini kuwa baadhi ya wakuu wa wilaya ndiyo wanaotumiwa na wamewekwa kwa makusudi kwa ajili ya kuua upinzani nchini.
“DC
anawahimiza wanachama na viongozi eti wapeleke barua za kujizulu kwake,
kwa sababu ana jeuri ya mamlaka. Kisheria hana mamlaka ya kupokea barua
ya kujiuzulu kwa mwanasiasa. Tumebaini hawa baadhi ya watendaji
wanatumiwa na kuahidiwa makubwa endapo watawadhibiti wapinzani,” alisema.
Alisema
walipata tetesi za kujiuzulu kwa madiwani hao lakini hawakutaka
kuchukua uamuzi wa kuwafukuza kwani si vizuri kuishi kwa tetesi lakini
kwa kuwa wameamua kuondoka anawatakia kila heri.
Alisema
baadhi ya madiwani hao walionekana kwenye vikao vya CCM na kusema mtu
anayezidiwa akili na kudanganywa kwa fedha hata akibaki katika chama
hatakuwa na maana.
“Kuliko kubaki na watu wengi wanaopenda fedha, wanaohadaiwa kwa rushwa, bora tubaki watu wachache wenye maadili,” alisema.
Mbowe
alisema, licha ya Serikali kuudhofisha upinzani, chama hicho kinaamini
kuwa safari yake ni kama ya treni ya kwenda Kigoma ambayo wapo
wanaopanda na wanaoshuka.
“Bado
tunavuna maelfu ya wana CCM, alianza Edwin Mtei, lakini sasa
tunazungumzia wanachama zaidi ya milioni sita. Muelewe kuwa upinzani
haudhoofiki, bali unakua,” alisema.
Alisema wale waliodhani watapata ulaji kama wa fedha, ndiyo wanaokuwa wepesi kuondoka na kwenda kutafuta wanachokitaka.
“Tuna imani watabaki wachache wenye imani na nafasi za walioondoka zitachukuliwa na wengine walio bora zaidi,” alisema.
Kuhusu
kuswekwa rumande kwa saa 48 kwa amri za wakuu wa wilaya, Mbowe alisema
sheria za kumuweka ndani kiongozi zina masharti yake.
“Kuna
utaratibu wa kufanya.DC sio polisi, anaweza kuagiza polisi, kamkamateni
fulani kisha mumhoji na kisha afunguliwe mashtaka, lakini si kumuweka
ndani kwa saa 48. Haya maagizo yote yanatolewa na ngazi za juu. Sisi
sasa tunawashtaki hao Ma-DC wote na hata mimi nimemshtaki DC wa Hai, kwa
kuharibu miradi yangu,” alisema.
0 comments:
Chapisha Maoni