WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema wazazi wana jukumu la kulea watoto kwenye
misingi ya kumcha Mungu ili Taifa liweze kuwa na watu waadilifu na
wachapakazi.
“Taifa
la watu waadilifu na wachapakazi huanzia katika ngazi ya familia. Kama
kaya zetu haziishi kwa uadilifu, ni vigumu sana kuwa na Taifa lenye
wananchi waadilifu. Ni muhimu basi familia zetu zihakikishe kuwa
tunakuwa na watoto wenye hofu ya Mungu na wenye kumcha Mungu,” alisema.
Alitoa
kauli hiyo Jumamosi, Juni 17, 2017 wakati akizungumza na wageni
waliohudhuria harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa na nyumba ya Paroko
katika Parokia Teule ya Zuzu, nje kidogo ya mji wa Dodoma.
Harambee
hiyo ilitanguliwa na ibada ya misa ya shukrani kwa ajili ya marehemu
Mzee Xavery Mizengo Pinda, ambaye ni baba yake, Waziri Mkuu mstaafu,
Mizengo Peter Pinda. Mzee Xavery Pinda alifariki Novemba 27, mwaka jana
katika hospitali ya mkoa wa Dodoma na kuzikwa kijijini kwake Kibaoni,
wilayani Mlele, Katavi.
Waziri Mkuu alisema wazazi wanapaswa kujitathmini juu ya malezi ya watoto wao na kujihoji kama wamepata malezi yanayostahili.
“Kupitia
funzo tulilolipata leo, tujitathmini kuhusu makuzi ya watoto wetu. Je
watoto wetu wanapata malezi stahiki? Je tunawalea katika misingi ya
kutoa kwa ajili ya Mungu au tunawafundisha wajilimbikizie mali? Je,
tunawahoji watoto wetu kuhusu utajiri wanaoupata ghafla? Au
tunawapongeza na kufurahia bila kujua wanapata wapi utajiri huo?,” alihoji.
“Nitumie
nafasi hii kuwasihi wazazi wote kwamba tujitahidi kuwekeza katika
malezi ya watoto wetu. Ili tuwe kioo cha aina ya Taifa tunalotaka
kulijenga, hatuna budi kuwalea watoto wetu katika misingi ya imani,
uadilifu na uzalendo mkubwa kwa nchi yetu,” alisisitiza.
Katika
harambee hiyo, Waziri Mkuu na mke wake walichangia sh. milioni 10
ambapo jumla ya sh. milioni 160 zilikusanywa. Kati ya hizo, sh.
111,150,000 zilikuwa ni ahadi, sh. 38,447,000 zilikuwa ni fedha taslimu
na sh. 10,403,000 zilikuwa ni vifaa vya ujenzi.
Mapema,
akiongoza ibada ya shukrani, Makamu wa Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la
Dodoma, Padre Chesco Msaga alisema kila mtu anapaswa kumshukuru Mungu
kwani hakuna mwanadamu anayeweza kudai kuwa yuko jinsi alivyo kwa sababu
ya akili zake.
“Hata
sisi tunasahau kumshukuru Mungu hasa pale mambo yetu yanapotunyookea.
Tunadhani ni kwa akili zetu ndiyo mambo yetu yananyooka. Tunapaswa
tukumbuke kuwa maishayetu yapo mikononi mwa Mungu, na yeye ndiye anajua
njia zetu,” alisema akirejea mfano wa wakoma 10 walioponywa na Bwana Yesu na mmoja tu ndiye alirudi kushukuru.
Kwa
upande wake, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda alisema harambee hiyo
inafuatia uamuzi wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dodoma, Mhashamu Beatus
Kinyaiya wa kuiteua Zuzu iwe parokia.
“Sasa
hivi tulikuwa na kigango. Kuteuliwa kuwa parokia maana yake tutakuwa na
padre anakaa hapa Zuzu saa 24 na tutakuwa na ibada kila Jumapili, na
katikati ya wiki kadri ratiba zitakavyoruhusu.
“Kikubwa
tunachopaswa kufanya kufuatia uamuzi huo, ni kuhakikisha kuwa mapadre
wana nyumba ya kuishi. Sasa hivi, wa kwetu anakaa Dodoma mjini. Kwa hiyo
tuna kazi ya kukarabati kanisa, lakini kwanza tukamilishe ujenzi wa
nyumba ya mapadri,” alisema wakati akielezea madhumuni ya harambee hiyo.
0 comments:
Chapisha Maoni