Na Jonas Kamaleki- MAELEZO
Serikali
imebuni vyanzo vingine vya mapato ili kupanua wigo wa kodi kwa ajili ya
maendeleo endelevu nchini na kukuza uchumi wa Taifa.
Dkt.
Mpango alisema kuwa Serikali ikusudia kuongeza mapato kwa kuwatambua
wafanyabiashara wasio rasmi kwa kuwapatia vitambulisho maalum kulingana
na biashara zao.
“Serikali
itawatambua rasmi wafanyabiashara wadogo wadogo wasio rasmi na
wanaofanyia biashara katika maeneo yasiyo rasmi mfano mama lishe,
wauzaji mitumba wadogowadogo, wauzaji wa mazao ya kilimo wadogo kama
mboga mboga, ndizi, matunda, na kadhalika kwa kuwapatia vitambulisho
maalum vya kazi wanazozifanya,” alisema Dkt. Mpango.
Aidha
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amesema kuwa Serikali
itaendelea na ukusanyaji wa kodi ya majengo (yaliyothaminiwa na
yasiyothaminiwa) kwenye halmashauri zote nchini.
Ameongeza
kuwa jukumu hilo litasimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango kupitia
Mamlaka ya Mapato Tanzania. Serikali itatoza Kodi ya Majengo kwa nyumba
zote kwa viwango vitakavyopangwa na Waziri wa Fedha na Mipango. Nyumba
ambazo hazijafanyiwa uthamini zitatozwa kwa kiwango maalum (flat rate)
cha shilingi elfu kumi (10,000) kwa nyumba na shilingi elfu hamsini
(50,000) kwa nyumba za ghorofa kwa kila ghorofa.
Dkt.
Mpango amesema kuwa Serikali itaendelea kusimamia na kuhimiza matumizi
ya mashine za kielektroniki (EFDs) kwenye Wizara, Idara, Taasisi za
Serikali na kwa wafanyabiashara.
Ili
kudhibiti mapato yatokanayo na madini, Dkt. Mpango amesema Serikali
haitoruhusu usafirishaji wa madini kutoka migodini na kupeleka moja kwa
moja nje ya nchi. Aidha, Serikali itaanzisha maeneo maalum (clearing
houses) katika viwanja vya kimataifa, migodini, na kadhalika ambapo
madini hayo yatathibitishwa na kupewa kibali cha kusafirisha madini hayo
ambacho kitatozwa ada ya asilimia moja (clearing fee) ya thamani ya
madini hayo.
Waziri
huyo wa Fedha na Mipango amesema Serikali itafungua akaunti maalum
(Escrow Account) kuanzia mwezi Julai 2017 ili kurahisisha na kuhakikisha
kwamba marejesho ya Ushuru wa Forodha wa ziada (Additional Import Duty)
wa asilimia 15 unaolipwa na waagizaji wa sukari ya viwandani
yanafanyika kwa wakati. Hatua hii itaiwezesha Mamlaka ya Mapato kufanya
marejesho kwa wakati kwa wazalishaji wanaotumia sukari hiyo katika
kuzalisha bidhaa mbalimbali.
Katika
hatua nyingine Dkt. Mpango amesititiza kuwa Serikali itaimarisha mifumo
ya ukusanyaji wa mapato kwa kutumia vifaa na mifumo ya kielektroniki
ili kuzuia uvujaji wa mapato ya Serikali.
“Mfumo
uitwao “Government e-payment Gateway System” uko tayari kwa ajili ya
matumizi ya Wizara, Idara na Taasisi za Serikali. Wizara, Idara na
Taasisi zote za Serikali zinaagizwa zianze kutumia mfumo huu,” alisema
Dkt. Mpango.
Amebainisha
pia kuwa Serikali imezindua mfumo mpya wa ukusanyaji mapato kwa njia ya
kielektroniki (Electronic Revenue Collection System (e-RCS)) ambao
utadhibiti udanganyifu unaofanywa na maafisa wa Serikali kwa
kushirikiana na walipa kodi katika kukadiria kodi sahihi.
Aidha,
mfumo huu utawasaidia walipa kodi kwa kuwa na uhakika wa kiasi cha kodi
wanayopaswa kulipa. Mfumo huo wa e-RCS utaanza rasmi katika mwaka huu
wa fedha kwa usimamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa upande wa Bara na Bodi ya Mapato
Zanzibar (ZRB) kwa upande wa Zanzibar.
Katika
mwaka 2017/18, Serikali inapanga kutumia jumla ya shilingi bilioni
31,712.0. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 19,712.4 zimetengwa kwa
ajili ya matumizi ya kawaida, ikijumuisha shilingi bilioni 7,205.8 za
mishahara na shilingi bilioni 9,461.4 kwa ajili ya kulipia deni la umma
na huduma nyinginezo. Aidha, matumizi ya maendeleo yatakuwa shilingi
bilioni 11,999.6 sawa na asilimia 38 ya bajeti.
0 comments:
Chapisha Maoni