Jovina Bujulu na Benjamin Sawe-MAELEZO
Baadhi
ya wasomi na wananchi wameisifu bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/18
wakisema kuwa imelenga kumkomboa mwananchi na imeakisi ahadi za Rais za
kusaidia Tanzania ya uchumi wa viwanda.
Akizungumzia
bajeti hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Dk. Benson Bana
amesema kuwa bajeti hiyo inajibu maswali mengi yaliyo kwenye Ilani ya
Chama Cha Mapinduzi na Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano 2020/21 na
Dira ya Taifa ya Mwaka 2020/25 na kwamba ni yenye kutegua vitendawili
vinavyowakabili wananchi katika kujiletea maendeleo.
“Kwa
sura ya bajeti ilivyo ni bajeti yenye ukombozi kwa mwananchi wa kawaida
kwa sababu inagusa masuala ya kupunguziwa kodi kwenye pembejeo,
vyakula, kilimo, miundombinu, umeme na maji,” amesema Dk Bana.
Naye
Dk Bashir Ally ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
ameipongeza bajeti hiyo na kushauri kuwa baada ya kupitishwa, mchakato
wa utekelezaji uanze kwa hamasa ya kisiasa, kitaaluma na kijamii ili
kufikia malengo yake.
‘’Unaweza
kuwa na mpango mzuri, lakini ikiwa watekelezaji ni wala rushwa,
wazembe, na wasiofuata sheria, wala kulipa kodi ni vigumu kufikia
malengo ya bajeti hiyo,’’ alisema Dk. Bashir.
Aliongeza
kusema kuwa bajeti hii inajenga msingi wa uchumi wa viwanda kwa
kuboresha miundombinu ya reli ya kisasa, bandari, , kulinda viwanda
vyetu na kuwekeza kwenye mafunzo ya vijana kutaongeza ari ya kujenga
uchumi wa kati na wa viwanda.
Wakati
huo huo Mtafiti na Mtaalam wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es
salaam Prof. Haji Semboja alisema kitendo cha Serikali kuondoa Kodi ya
ngezeko la Thamani (VAT) kwa wasafirishaji kutazivutia nchi ambazo
hazina bandari kutumia bandari na kuleta kuongeza ajira kwa Watanzania.
Alisema
kuondoa kodi ya tozo ya leseni ya barabarani kutairahisishia serikali
ukusanyaji wa mapato na gharama za ukusanyaji wa kodi hizo utakuwa ni
mdogo ila akaonya kuwa inaweza kuongeza gharama kwa yule ambaye
ataendesha gari mara kwa mara.
Akiongea
na Idara ya Habari kwa njia ya simu, Mhadhiri wa ChuoKikuu Huria
chaTanzania (OUT) Dkt. Damas Ndumbaro ametaja uwekezaji katika
miundombinu, kuondolewa kwa tozo ya kodi ya leseni ya barabarani na
punguzo la kodi katika mazao ni mambo muhimu yanayopeleka faraja kwa
wananchi na yatachochea maendeleo kwa kiwango kikubwa.
“Karibu
asilimia 80 ya watanzania wanaishi vijijini na wanategemea kilimo sasa
nafuu ya kodi katika mazao ya kilimo itasaidia sana kuwahamasisha
wakulima na kuwainua kiuchumi lakini pia mazao hayo yatatumika katika
viwanda mbalimbali ambavyo vinaanzishwa nchini na kuongeza ajira,”
alieleza Dkt. Ndumbaro.
Kuhusu
kodi ya leseni ya barabarani, Dkt. Ndumbaro alisema kuwa hiyo ni nafuu
kubwa kwa watu wenye magari na vyombo vingine vya moto kwani watalipia
gharama katika mafuta na hivyo kumfanya mtu alipe kwa kadiri ya
anavyotumia chombo chake.
Kwa
upande wake Shehe wa Dar es Salaam, Alhaji Musa Salum alisema bajeti
hiyo ni ya kizalendo na kimaendeleo kwani imewapa watanzania unafuu na
kuwasihi wananchi kuipokea na kuitendea haki kwani imekuja kuboresha
maisha yao.
Mmoja
wa Wakulima wa Tumbaku na mazao ya chakula, Bw. John Pinini kutoka
Tabora ameeleza kufurahishwa na bajeti na kutoa wito kwa Watanzania
kuipokea na kuhakikisha wanashirikikatika utekelezaji wakeikiwemo
kuhakikisha wanalipa kodi stahili kwa mujibu wa sharia na taratibu.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpanga jana alisoma mapendekezoya
bajeti kwa mwaka wa fedha 2017/2018 yenye thamani ya shilingi trilioni
31.7 ambapo miongoni mwa vipaumbele ni pamoja na kuendeleza ukuaji wa
uchumi na kujenga uchumi wa kipato cha kati, ujenzi wa miundombinu ya
kiuchumi, kuboresha kilimo cha mazao, mifugo na uvuvi na kuongeza ubora
wa elimu, huduma za afya, maji na umeme.
0 comments:
Chapisha Maoni