Mbunge
wa Kibamba (Chadema), John Mnyika amesema atachukua hatua kwa kitendo
cha kusukumwa kilichofanywa na askari wa Bunge mwishoni mwa wiki.
Alisema atafanya hivyo mara baada ya kumaliza msiba wa mmoja wa waasisi wa chama hicho, Philemon Ndesamburo.
“Nitatoa
tamko na kuchukua hatua nikimaliza msiba, leo (jana) na kesho (leo)
nipo msibani huku Moshi, lakini nitafafanua na kuzungumzia hilo
nikimaliza,” alisema.
Mnyika
alitolewa bungeni kwa nguvu na askari wa Bunge baada ya Spika wa Bunge,
Job Ndugai kuwaamuru kumtoa ndani akidaiwa kukiuka kanuni za Bunge
wakati akichangia mjadala wa Wizara ya Nishati na Madini.
Pia, mbunge huyo alipewa adhabu ya kutohudhuria vikao saba vya Bunge, huku askari hao wakimtoa ndani kwa nguvu na kumsukuma.
Ndesamburo,
ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Moshi Mjini kwa miaka 15 mfululizo
ataagwa leo katika Uwanja wa Majengo mjini Moshi na baadaye mwili wake
utapelekwa nyumbani kwake ambako taratibu za mazishi zitafanyika kesho.
Wakati
Mnyika akisubiri kumzika Ndesamburo, Chadema Wilaya ya Ubungo imelaani
kitendo alichofanyiwa mbunge huyo ikisema hakikuwa cha kiungwana na
kilikiuka hadhi yake.
Katibu
Mwenezi wa Chadema wilayani humo, Perfect Mwasiwelwa alisema kitendo
alichofanyiwa Mnyika kingeweza kumletea majeraha kama angeanguka
kutokana na mazingira ya eneo aliposukumiwa.
Mwasiwelwa
alisema mwanasiasa huyo anawawakilisha wananchi zaidi ya 78,000 hivyo
Chadema inalaani kitendo hicho kwa sababu si cha utu.
“Alitolewa
nje katika mazingira ambayo sio ya utu, sio ya Kitanzania, sisi kama
chama ngazi ya wilaya tunasema hakikuwa kitendo cha kawaida kabisa,”
alisema.
Wakati
huo huo, wabunge wawili wa Chadema; Halima Mdee (Kawe) na Esther Bulaya
(Bunda Mjini) leo watasomewa hukumu yao baada ya Kamati ya Kudumu ya
Maadili ya Bunge kuwajadili na kumshauri Ndugai hatua sahihi za
kuwachukulia.
Bulaya
na Mdee watasomewa hukumu kutokana na kulivalia njuga suala la Mnyika
kutolewa ndani ya ukumbi wa Bunge wakati spika alipoamuru atolewe na
askari wa chombo hicho.
0 comments:
Chapisha Maoni