Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan
ameagiza kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria kwa viwanda na migodi
ambayo inafanya shughuli zake za uzalishaji kwa kuharibu mazingira
ikiwemo utitirishaji wa kemikali kwa wananchi kwani kufanya hivyo
kunahatarisha usalama wa wananchi na viumbe hai wengine.
Makamu
Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo tarehe 4-Jun-2017
kijijini Butiama mkoani Mara wakati anahutubia wananchi katika kilele
cha siku ya mazingira Duniani.
Makamu
wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan alisema uharibifu wa mazingira
ukiachiwa uendee nchini ni hatari kwa usalama wa maisha na viumbe hivyo
ni muhimu kwa viongozi katika ngazi zote kuchukua hatua zitakazosaidia
kukabiliana na vitendo hivyo kote nchini.
Makamu
wa Rais alisisitiza kuwa umefika wakati kwa viongozi kwa ushirikiano na
jamii kuhakikisha wanaweka mikakati ya kuokoa mifumo ya ikolojia,
uhifadhi wa bioanuai, kudhibiti uchomaji miti kiholela ili kurejesha
uoto wa asili ambao umeharibiwa na shughuli mbalimbali za kibinadamu
katika maeneo mengi nchini.
“Kutozingatia
hifadhi ya mazingira kunaweza kusababisha kuparaganyika kwa mfumo huo
na kufanya maisha yetu na ya vizazi vijavyo kuwa mashakani”. Alisisitiza
Makamu wa Rais.
Makamu
wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan alisema katika kuadhimisha siku ya
mazingira Dunia viongozi wanapaswa kuchukua hatua za kuelimisha wananchi
na kuwahamasisha ili kila mtu ashiriki katika juhudi za kuwa na uchumi
unaozingatia hifadhi ya mazingira.
Kuhusu
wananchi kutembelea hifadhi za taifa nchini, Makamu wa Rais aliipongeza
Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuruhusu wananchi kutembelea hifadhi
za taifa bila kiingilio na kusema mpango huo ni mzuri na unatakiwa
kufanyika kila mwaka.
Alisema
kuwa mkakati huo unalenga kuhamasisha wananchi ili kuwa mahusiano
rafiki na mazingira kwa kuzingatia ukweli kwamba jinsi wananchi
wanapoona ndipo wanapoamini na kuelewa umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.
Alieleza
kuwa katika kuadhimisha siku hiyo inapasa jamii kutafakari mchango wa
kila sekta na kila mwananchi katika uhifadhi wa mazingira kwenye maeneo
wanayoishi.
Kwa
upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na
mazingira January Makamba alisema Serikali imeamua kuadhimisha siku ya
Mazingira Duniani kijijini Butiama kama hatua ya kuenzi mchango mkubwa
uliofanya na baba wa taifa mwalimu Julius Nyerere katika uhifadhi wa
mazingira.
Alisema
baba wa taifa mwalimu Julius Nyerere alifanya kwa vitendo katika
kuhifadhi mazingira ambapo alianzisha msitu wake katika eneo la Butiama
hivyo wananchi wote ni lazima waige mfano huo katika kulinda na kutunza
mazingira.
Kwa
upande wa familia na mwalimu Nyerere wameishukuru Serikali kwa kupeleka
maadhimisho hayo kijijini Butiama ikiwa ni sehemu ya kuenzi na kutambua
mchango wa baba wa taifa katika uhifadhi wa mazingira nchini.
Kabla
ya Kuhutubia katika Kilele cha Siku ya Mazingira Duniani, Makamu wa
Rais Mhe Samia Suluhu Hassan alipanda miti katika msitu wa Mwalimu
Nyerere na kuweka shada la maua kwenye mnara wa kumbukumbu ya ajali ya
Ndege ya Kivita ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) uliopo katika
msitu wa Muhunda katika kijiji cha Butiama mkoani MARA.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Butiama – Mara
4-June-2017.
0 comments:
Chapisha Maoni