I.
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, naomba
kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu lipokee, lijadili na kupitisha Makadirio ya
Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2017/18. Bajeti hii inawasilishwa kwa
kuzingatia matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,
Ibara ya 137 ikisomwa pamoja na Sheria ya Bajeti namba 11 ya mwaka 2015 kifungu
cha 26.
2.
Mheshimiwa Spika, pamoja
na hotuba hii, ninawasilisha vitabu vinne vinavyoelezea kwa kina makadirio ya
Bajeti kwa Mafungu. Kitabu cha Kwanza ni Makadirio ya Mapato; Kitabu cha Pili
ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi
na Wakala za Serikali; Kitabu cha Tatu ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa
Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; na Kitabu cha Nne ni
Makadirio ya Matumizi ya Maendeleo kwa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za
Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo
Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2017 pamoja na Muswada wa Sheria ya
Matumizi ya Serikali wa mwaka 2017 ambayo ni sehemu ya Bajeti hii.
3.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi
Mungu kwa baraka na amani anayoendelea kuijalia nchi yetu na pia kwa
kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha Bajeti ya Serikali
kwa mwaka 2017/18.
4.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee napenda nichukue fursa hii
kumshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini katika dhamana hii kubwa ya
kuongoza wizara nyeti ya Fedha na Mipango. Aidha, ninamshukuru sana kwa
kuniongoza na kunitia moyo pale mawimbi yalipozidi kuwa makubwa. Maneno yake
mazito kwamba aliniteua ili nipigwe mawe badala yake na badala ya Watanzania
maskini na kuwa nimtegemee Mungu daima, yamekuwa ndiyo nguvu yangu katika kazi.
Vile vile, nampongeza Mheshimiwa Rais pamoja na wasaidizi wake wakuu,
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na Mbunge wa jimbo la Ruangwa kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya
ya kutuletea maendeleo Watanzania wote.
5.
Mheshimiwa
Spika,
naomba pia kuwapongeza viongozi wakuu wa mihimili ya dola, nikianza na wewe
mwenyewe Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa jimbo
la Kongwa, na Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson (Mbunge) Naibu Spika. Ninawapongeza
kwa umahiri na busara zenu katika kuongoza Bunge hili. Vile vile, ninawapongeza
kwa dhati Mheshimiwa Profesa Ibrahim Juma, Kaimu Jaji Mkuu, kwa kuongoza vyema
mhimili wa mahakama katika kutoa haki.
6.
Mheshimiwa
Spika,
ninawapongeza pia wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, nikianza na Mkuu wa
Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo; Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro;
Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Alli Malewa; Kamishna Jenerali wa
Uhamiaji Dkt. Anna Makakala; Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Dkt. Modestus
Kipilimba; Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,
Kamishna wa Polisi, Valentino Mlowola; Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kuzuia
na Kupambana na Madawa ya Kulevya Bw. Rogers William Siang’a; na Kamishna
Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji Bw. Thobias Andengenye, pamoja na makamanda,
askari na watumishi wote wa vyombo hivyo kwa uhodari wao katika kuilinda nchi yetu
na kuhakikisha amani, usalama na uhuru wetu wa kisiasa na kiuchumi
vinadumishwa.
7.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwapongeza Wabunge wapya
walioingia katika Bunge hili mwaka huu wa fedha ambao ni Mheshimiwa Juma Ali
Juma, Mbunge wa Dimani (CCM); Mheshimiwa Mchungaji Dkt. Getrude Pangalile
Rwakatare – Mbunge wa Viti Maalum (CCM); na Mheshimiwa Catherine Nyakao Ruge,
Mbunge wa Viti maalum (CHADEMA). Nawapongeza pia Waheshimiwa Wabunge
walioteuliwa na Rais: Mheshimiwa Abdallah Majura Bulembo (Mb); Mheshimiwa Anne
Kilango Malecela, (Mb); Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete (Mb); na Mheshimiwa
Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (Mb) ambaye pia ni Waziri wa Katiba
na Sheria. Hongera sana kwenu nyote. Sambamba na hilo, niwapongeze Waheshimiwa
Wabunge waliochaguliwa na Bunge hili kuiwakilisha nchi yetu ya Tanzania katika
Bunge la Afrika Mashariki ambao ni: Mhe. Fancy Nkuhi, Mhe. Happiness Legiko,
Mhe. Maryam Ussi Yahya, Mhe. Dkt. Abdallah Makame, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe,
Mhe. Mhandisi Habibu Mnyaa, Mhe. Alhaji Adam Kimbisa, Mhe. Pamela Massay na
Mhe. Josephine Lemoyani. Nawatakia kazi njema na kuwasisitiza wasiyumbe katika
kusimamia maslahi ya kimkakati (strategic interests) ya Taifa letu katika
mijadala ya Bunge hilo la Afrika Mashariki.
8.
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kutoa pole kwa
Watanzania waliopatwa na majanga mbalimbali na misiba, nikianza na Bunge ambalo
liliwapoteza wenzetu, Mheshimiwa Hafidh Ali Tahir aliyekuwa Mbunge wa Dimani
(CCM) na Mheshimiwa Dkt. Elly Marko Macha aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum
(CHADEMA). Aidha, Bunge liliondokewa na Spika mstaafu, Mheshimiwa Samuel John
Sitta, mzee wa kasi na viwango. Vile vile, natoa pole kwa wazazi na ndugu wa
wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja wa shule ya Lucky Vincent
waliofariki kwa ajali ya gari tarehe 06 Mei, 2017 katika wilaya ya Karatu.
Vivyo hivyo, ninatoa pole kwa ndugu wa askari wetu wanane na wananchi wengine
ambao wameuwawa na kundi la kihalifu katika wilaya za Kibiti na Rufiji kwa
nyakati tofauti katika mwaka huu. Mungu azilaze roho za marehemu wote hao
mahala pema peponi. Amina!
9.
Mheshimiwa Spika, ninawiwa kuishukuru
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti inayoongozwa na Mhe. Hawa Abdulrahman
Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini na makamu wake Mhe. Josephat Sinkamba
Kandege, Mbunge wa Kalambo, kwa kupitia na kuchambua mapendekezo ya bajeti
ninayowasilisha hivi sasa na kutoa maoni na ushauri uliochangia kuboresha
Bajeti hii ya Serikali kwa mwaka 2017/18. Aidha, napenda kuwashukuru wenyeviti
wa kamati za kudumu za kisekta na waheshimiwa wabunge wote kwa ushauri na
mapendekezo mliyotoa kwa Serikali wakati wa kuchambua Bajeti za kisekta.
Ninamshukuru pia Mhe. George Mcheche Masaju (Mb), Mwanasheria Mkuu wa Serikali
kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2017 na Muswada
wa Sheria ya Matumizi wa mwaka 2017.
10.
Mheshimiwa Spika,
napenda
kumshukuru Mhe. Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji, Mbunge wa Kondoa, ambaye ni Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, kwa ushirikiano na msaada anaonipatia katika
utekelezaji wa majukumu ya wizara yangu. Aidha, napenda kumshukuru Bwana Doto
M. James, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali
kwa usimamizi wa kazi za kila siku za wizara na uratibu mzuri wa maandalizi ya
Bajeti hii, akisaidiwa na Naibu Makatibu Wakuu, Bibi Dorothy Mwanyika, Bibi
Amina Kh. Shaaban na Dkt. Khatibu Kazungu.
11. Mheshimiwa Spika, ninaendelea
kumshukuru sana Profesa Benno Ndulu, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania kwa
kuongoza kwa weledi taasisi hiyo nyeti yenye jukumu la kusimamia sekta ya fedha
na kulinda utulivu na ukuaji wa uchumi wa Taifa. Aidha, napenda kutambua kazi
nzuri ya viongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania katika kukusanya mapato ya
Serikali wakiongozwa na Bw. Charles Kichere, Kamishna Mkuu wa Mamlaka. Pia
ninawashukuru Dkt. Oswald Mashindano, Msajili wa Hazina na Dkt. Albina Chuwa,
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu. Vile vile, ninawashukuru Kaimu
Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara;
Wakuu wa idara na vitengo vya Wizara, pamoja na watumishi wote wa Wizara na
taasisi zake kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kukamilisha Bajeti hii.
12. Mheshimiwa
Spika,
Bajeti hii pia imezingatia mawazo na mapendekezo ya wadau mbalimbali wakiwemo
jumuiya ya wafanyabiashara na Washirika wa Maendeleo. Nawashukuru wote kwa
mawazo na ushauri. Kipekee niwashukuru wajumbe wa Kikosi Kazi cha Maboresho ya
Mfumo wa Kodi (Task Force on Tax Reforms) ambayo inaundwa na wawakilishi wa
sekta binafsi na wataalam wa kodi kutoka vyuo vikuu na taasisi za utafiti.
Aidha naishukuru Kamati ya Ushauri kwa Waziri wa Fedha kuhusu hatua za mapato
(Advisory Committee on Revenue Measures). Uchambuzi na ushauri wao umechangia
kufikia hatua mpya za kodi nitakazopendekeza hivi punde.
13.
Mheshimiwa Spika, hotuba hii inawasilisha Bajeti ya pili ya
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Serikali inaleta Bajeti hii
kwa dhamira ya kuongeza kasi ya kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2025 kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015 – 2020; Mpango wa
Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17-2020/21; Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu;
na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030.
14.
Mheshimiwa
Spika,
katika hotuba ya uzinduzi wa Bunge la 11 tarehe 20/11/2015, Mheshimiwa Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwaeleza
Watanzania kwamba, vipaumbele vya Serikali yake kuhusu uchumi ni kuendeleza na
kuimarisha misingi imara ya uchumi wa nchi yetu iliyojengwa katika awamu za
uongozi zilizotangulia. Vipaumbele hivyo ni vifuatavyo:
i.
Kuendeleza ukuaji wa uchumi na kujenga uchumi wa kipato cha kati ambapo
sura na maisha ya Watanzania walio wengi yafananefanane na nchi ya kipato cha
kati;
ii.
Kuongeza mapato, kuziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali,
kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, na kusimamia sheria za manunuzi ya umma;
iii.
Ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi (barabara, reli, usafiri wa anga na wa
majini, umeme) ili kushawishi na kuvutia wawekezaji wa ndani na wa nje;
iv.
Kuhakikisha kwamba madini na maliasili zetu zinatumika kwa manufaa ya
Taifa letu;
v.
Kuweka mkazo mkubwa na kusimamia uendelezaji wa viwanda kwa kutambua
kwamba sekta binafsi ndiyo mhimili mkubwa wa kujenga uchumi wa viwanda. Aidha,
aina ya viwanda tunavyotaka ni vile
ambavyo vina sifa ya kuzalisha ajira nyingi, sehemu kubwa ya malighafi
husika itatoka ndani, na vile vya kuzalisha bidhaa zinazotumiwa na watu wengi
nchini;
vi.
Kuboresha kilimo cha mazao, mifugo na uvuvi, hususan kuongeza thamani na
kuzifanya shughuli hizi kuwa za kisasa zaidi kwa kutoa mafunzo, pembejeo, zana
na wataalam;
vii.
Kuweka mkazo katika kuendeleza utalii, ardhi na utunzaji wa mazingira;
viii.
Kuongeza ubora wa elimu, huduma za afya, maji na umeme;
ix.
Kupambana na tatizo kubwa la rushwa, ufisadi na madawa ya kulevya; na
x.
Kufanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji serikalini ili kupunguza
urasimu.
Hivyo, mapitio ya mwenendo
wa uchumi wa Taifa na tathmini ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali katika
mwaka 2016/17 yamelenga kutoa picha ya utekelezaji wa vipaumbele hivyo vya
Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
15.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba niliyosoma leo asubuhi,
nilieleza kwa kirefu hali ya uchumi wetu ilivyokuwa katika mwaka 2016 na miezi
minne ya kwanza ya mwaka huu wa 2017. Inatosha nirejee kuwaambia Watanzania
kwamba uchumi wa Taifa umeendelea kuimarika ambapo Tanzania ilikuwa miongoni
mwa nchi tano za Afrika zilizoongoza kwa kuwa na kasi kubwa ya ukuaji wa
uchumi. Kwa mujibu wa takwimu za uchumi za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF
World Economic Outlook Database), nchi hizo tano ni Ivory Coast (asilimia 7.9);
Tanzania (asilimia 7.1); Senegal (asilimia 6.6); Djibouti (asilimia 6.5); na
Ethiopia (asilimia 6.5). Aidha, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha
Duniani Bw. Tao Zhang alipotembelea Tanzania kwa mara ya kwanza mwezi Mei 2017,
alitoa tathmini yake kwamba uchumi wa Tanzania umebaki kuwa imara kutokana na
maboresho ya kisera yaliyotekelezwa chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa
Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli hasa katika maeneo ya ukusanyaji wa
mapato ya ndani na vita dhidi ya rushwa na ufisadi.
16.
Mheshimiwa Spika, jarida la Benki ya Dunia (Tanzania Economic
Update) lililochapishwa Aprili 2017 linabainisha waziwazi kuwa uchumi wa Taifa
ni imara kwa kuangalia viashiria mbalimbali kama ukuaji wa uchumi, mfumuko wa
bei, urari wa biashara, akiba katika fedha za kigeni na thamani ya shilingi, na
naomba kunukuu kwa kiingereza:
“Tanzania’s
economic performance continues to rank among the highest in the region. The
real GDP growth rate has consistently outpaced its EAC peers. The inflation
rate remains relatively low. The current account deficit has significantly
improved, with gross reserves sufficient to cover four months of imports. The
shilling has also remained stable in 2016, following significant depreciation
and volatility in 2015.”
17.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo, pamekuwa na maeneo
ambayo yametawala mijadala kuhusu afya ya uchumi wa Taifa, ambayo napenda
kuyaelezea kwa kifupi. Maeneo hayo ni pamoja na ukwasi katika uchumi, kufungwa
kwa biashara, na madai kwamba sekta binafsi imepoteza matumaini na kujiamini
(private sector confidence) kutokana na baadhi ya hatua zilizochukuliwa na
serikali bila ushirikishwaji wa wadau.
Hali ya Ukwasi Katika Uchumi
18.
Mheshimiwa Spika, ukwasi ni kiasi cha fedha kilichopo katika
uchumi kinachojumuisha fedha taslim zilizoko kwenye mzunguko nje ya mabenki na
rasilimali fedha nyingine ambazo
zinaweza kubadilishwa na kuwa fedha taslimu bila kikwazo. Utoshelevu wa ukwasi
katika uchumi hupimwa kwa viashiria mbalimbali vikiwemo ujazi wa fedha,
mwenendo wa mikopo kwa sekta binafsi, kiwango cha mitaji ya mabenki, uwiano
kati ya mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha taslim na amana zinazoweza
kuhitajika katika muda mfupi na upatikanaji wa huduma za kifedha.
19.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi kilichoishia mwezi Machi 2017,
hali ya baadhi ya vigezo vya ukwasi inaonyesha kuwa ujazi wa fedha kwa tafsiri
pana zaidi (M3) ambao unajumuisha sarafu na noti zilizoko katika mzunguko nje
ya mabenki, amana za muda mfupi, muda maalum na amana katika fedha za kigeni
zilizopo katika mabenki, uliongezeka na kufikia shilingi trilioni 22.53 kutoka
shilingi trilioni 21.65 katika kipindi kama hicho mwaka 2016, sawa na ongezeko
la asilimia 4.1. Aidha, sekta ya kibenki iliendelea kuwa imara na himilivu,
ikiwa na viwango vya mitaji na ukwasi ulio juu ya ukomo unaohitajika kisheria
kama ifuatavyo: kwa kutumia kigezo cha uwiano kati ya mali inayoweza
kubadilishwa kuwa fedha taslim na amana zinazoweza kuhitajika kwa muda mfupi
(Liquid Assets to Demand Liabilities), uwiano huu ulikuwa asilimia 35.9 mwezi
Machi 2017 ikilinganishwa na uwiano wa chini unaohitajika kisheria wa asilimia
20. Vile vile, uwiano wa mtaji wa msingi na rasilimali za benki ulikuwa
asilimia 19.0 ambao uko juu ya kiwango cha chini kinachohitajika kisheria cha
asilimia 10. Kadhalika, amana za wateja katika benki za biashara ziliongezeka
kwa asilimia 0.3 kutoka shilingi trilioni 18.84 mwezi Machi 2016 hadi shilingi
trilioni 18.89 mwezi Machi 2017.
20.
Mheshimiwa Spika, takwimu pia zinaonesha kuwa ukwasi wa mabenki
ulianza kutetereka kutokana na kuongezeka kwa mikopo chechefu kutoka asilimia
8.3 mwezi Machi 2016 hadi asilimia 10.9 Machi 2017 ikilinganishwa na kiwango
kinachohitajika cha asilimia 5. Mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kidogo kwa
asilimia 3.7 katika kipindi cha mwaka ulioishia Machi 2017 ikilinganishwa na
ongezeko la asilimia 23.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2016. Kupungua kwa
kiwango cha ukuaji huo kulitokana kwa kiasi kikubwa na kuyumba kwa biashara
duniani ambako kuliathiri nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania. Napenda
kuchukua fursa hii kuyataka mabenki yote nchini kusimamia sawasawa taratibu za
kibenki katika utoaji wa mikopo.
21.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Benki Kuu imechukua hatua
ikiwa ni pamoja na kupunguza riba ambazo benki za biashara hukopa kutoka Benki
Kuu (Discount Rate) ili kuongeza ukwasi katika benki za biashara na hivyo kuziwezesha kukopa kwa gharama nafuu
zaidi. Riba hiyo imepunguzwa kutoka asilimia 16.0 iliyokuwa ikitumika tangu
mwezi Novemba 2013 hadi asilimia 12.0 ambayo imeanza kutumika rasmi tarehe 6
Machi 2017. Aidha, katika kuimarisha zaidi soko la fedha nchini, Benki Kuu
ilipunguza kiwango cha amana ambacho benki za biashara zinatakiwa kuhifadhi
Benki kuu kama dhamana (Statutory Minimum Reserve Requirement – SMR) kutoka
asilimia 10.0 hadi asilimia 8.0 ili kuziwezesha benki za biashara kuwa na
ukwasi zaidi kwa ajili ya kukopesha sekta binafsi. Hatua hii imeanza kutumika
rasmi mwezi Aprili 2017. Ni matumaini ya Serikali kuwa hatua hizi zitaziwezesha
benki za biashara nchini kuongeza ukwasi wa kutosha kuwakopesha wananchi kwa
riba nafuu.
22. Mheshimiwa Spika, katika hatua
nyingine, mwaka 2016/17 benki tatu za biashara zilifungwa kutokana na sababu
mbalimbali. Benki hizo ni Benki ya Twiga, FBME Bank Limited; na Mbinga
Community Bank. Mnamo tarehe 28 Oktoba 2016, Serikali kupitia Benki Kuu ya
Tanzania ilichukua usimamizi wa benki ya Twiga baada ya kubaini
kuwa benki hiyo ilikuwa na upungufu mkubwa wa mtaji
kinyume na matakwa ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za
Fedha ya mwaka 2006
na kanuni zake.
Upungufu huu wa mtaji ulionekana kuhatarisha usalama wa sekta ya fedha
na pia kuendelea kutoa huduma za kibenki kwa benki ya Twiga kungehatarisha
usalama wa amana za wateja wake. Hata
hivyo, baada ya kukamilika kwa zoezi la kutathmini hali ya kifedha ya benki
hiyo, Serikali iliruhusu baadhi ya huduma za benki hiyo ziendelee huku
ikiendelea na mchakato wa kupitia na kuchambua njia mbadala za kutatua tatizo
la mtaji linaloikabili benki ya Twiga. Kwa sasa Serikali inapitia maombi
yaliyoletwa na wawekezaji mbalimbali wanaotaka kununua hisa na kuongeza mtaji
wa benki hiyo.
23. Mheshimiwa Spika, tarehe 8 Mei,
2017 Serikali ilisimamisha shughuli zote za FBME Bank Limited; kufuta leseni
yake ya kufanya shughuli za kibenki; kuiweka chini ya ufilisi; na kuiteua Bodi
ya Bima ya Amana kama mfilisi. Uamuzi huu ulifikiwa kutokana na mwelekeo wa benki hiyo kuwa mashakani
kufuatia mahakama ya Marekani kukubaliana na ombi la Taasisi ya Marekani ya
Kupambana na Uhalifu wa Kifedha (FinCEN) la kuifungia FBME kutumia mfumo wa
kibenki wa Marekani kutokana na tuhuma za kujihusisha na biashara ya
utakatishaji wa fedha haramu. Naomba tena kupitia hotuba hii ya Bajeti ya
Serikali kwa mwaka 2017/18 kuyaonya mabenki yote yatakayobainika kujihushisha
na biashara ya utakatishaji fedha haramu au kufadhili ugaidi au kwenda kinyume
na sheria za nchi kwamba Serikali itachukua hatua kali za kufuta leseni za
kufanya shughuli za kibenki hapa nchini mara moja na hatua nyingine kwa mujibu
wa Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake, na hata
sheria za kimataifa.
24. Mheshimiwa Spika, Serikali
kupitia Benki Kuu ya Tanzania ilichukua hatua nyingine ya kuifunga Mbinga Community Bank Plc, kusitisha shughuli
zake zote za kibenki na kufuta leseni yake ya biashara ya kibenki kuanzia
tarehe 12 Mei, 2017. Benki hiyo iliwekwa
chini ya ufilisi na kuiteua Bodi ya Bima ya Amana kama mfilisi. Uamuzi huu
ulichukuliwa baada ya Serikali kujiridhisha kuwa Mbinga Community Bank Plc ina upungufu mkubwa wa mtaji na ukwasi kinyume
na matakwa ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kanuni
zake. Upungufu huu wa mtaji na ukwasi ungeweza kuhatarisha usalama wa sekta ya
fedha, na wa amana za wateja. Serikali inapenda kuuhakikishia umma wa
Watanzania kuwa itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki
yaliyopo nchini kwa lengo la kulinda utulivu katika sekta ya fedha.
25. Mheshimiwa Spika, wigo wa
utoaji huduma za kifedha kwa wananchi walio wengi zaidi na kwa gharama nafuu umepanuka
sana kutokana na mtandao mkubwa wa mabenki na taasisi nyingine za fedha
zipatazo 64 [benki za biashara 40, benki za maendeleo 3, benki za jumuiya 11,
huduma ndogo za kifedha – (micro finance)
5, taasisi zinazotoa mikopo binafsi (private
credit) 2, na kampuni za huduma za kifedha za kukodisha (lease finance) 3].
Sambamba na hizi, kuna huduma za kifedha na malipo kupitia huduma za benki
zinazohamishika (mobile banking),
mawakala na simu za mkononi. Hivi sasa, inakadiriwa kuwa Watanzania zaidi ya
milioni 17 wanafanya miamala kwenye mfumo wa malipo kupitia simu za mkononi.
Kufungwa kwa Biashara
26.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo lilikuwa likizungumzwa
sana na wananchi na pia hapa Bungeni ni kuhusu kuongezeka kwa kasi ya kufunga
biashara hususan, eneo la Kariakoo katika Jiji la Dar es salaam na katika miji
mingine. Kwa mujibu wa taarifa zilizofikishwa TRA, katika kipindi cha kuanzia
Julai 2016 hadi Machi, 2017 jumla ya biashara 7,277 zilifungwa katika mikoa
mbalimbali nchini. Mwenendo huu kwa ujumla siyo mzuri kwa sababu wananchi
wanapoteza ajira na kipato, Serikali inakosa mapato ya kodi na uchumi
unadorora. Hivyo, ni muhimu pale wimbi la kufungwa kwa biashara linapotokea
jitihada zifanyike kuelewa aina gani za biashara zinafungwa, kwa nini zinafungwa
na hatua gani zichukuliwe kudhibiti hali hiyo.
27.
Mheshimiwa Spika, ziko sababu nyingi zinazoweza kuwa zimepelekea
hali hiyo, ikiwa ni pamoja na ushindani mkali wa kibiashara; usimamizi dhaifu
wa biashara; kuongezeka kwa gharama za kufanya biashara kama vile usafirishaji,
kodi na tozo mbalimbali; na kutozingatia masharti ya kufanya biashara. Lakini
pia, imedhihirika kwamba, wafanyabiashara wengi wameanza mazoea ya kutoa
taarifa kwa Mamlaka ya Mapato mara wanapofunga biashara zao. Hii ilitokana na
elimu iliyotolewa na Mamlaka kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa ambazo zimewafanya
walipa kodi kufahamu kuwa unapofunga biashara bila kutoa taarifa, kodi
inajilimbikiza na wataendelea kudaiwa na TRA.
28.
Mheshimiwa Spika, ni vema kutambua kwamba kufunguliwa au
kufungwa kwa biashara ni jambo la kawaida kabisa katika uendeshaji wa biashara.
Napenda kuliarifu Bunge hili kuwa, katika kipindi hicho hicho cha Julai 2016
mpaka Machi 2017, Mamlaka ya Mapato ilisajili biashara mpya zipatazo 224,738.
Hivyo, picha inayotolewa isiwe ya upande mmoja tu. Ni vema pia kujua kwamba
kufungwa kwa biashara sio kwa Tanzania pekee. Ni jambo ambalo linatokea katika
vipindi mbalimbali katika historia za mataifa na kwa viwango tofauti tofauti.
Watu wengi miongoni mwetu tumesoma kuhusu anguko kuu la biashara lililotokea
katika bara la Ulaya na Amerika kati ya mwaka 1929-1939 likijulikana kama “the Great Depression”. Huko China nako
katika miaka 1980 biashara nyingi zilipigwa na dhoruba ambapo baadhi zilizama
lakini nyingine ziliendelea kukua. Haya yameelezwa vizuri sana katika kitabu
cha Tian Tao na wenzake kinachoitwa Huawei:
Leadership, Culture and Connectivity
kilichochapishwa mwaka 2017. Naomba kunukuu kwa lugha ya kiingereza kutoka
ukurasa wa 43 wa kirumi wa kitabu hicho:
“From
the 1980s onward, China was swept up in the largest wave of commercial
development in human history. Businesses at the time were like ships, each
raised up and carried along by the sheer momentum of the wave. Some, however,
soon capsized and were swallowed up, while most drifted along, going with the
flow. Others crashed against barriers in the sea or got stranded on deserted
islands. Only a few rose atop the crest of the wave and survived, eventualy
sailed towards new lands.”
29.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na
Uwekezaji kwa kushirikiana na Wizara yangu inaendelea kufuatilia kwa karibu
mwenendo wa biashara nchini na itachukua hatua stahiki itakapobidi kufanya
hivyo. Wito wa Serikali kwa wafanyabiashara nchini ni kwamba fanyeni biashara
zenu bila hofu kwa kuzingatia sheria kanuni na taratibu za nchi.
Madai ya Kuwa Sekta Binafsi Imepoteza Kujiamini
(Private Sector Confidence)
30.
Mheshimiwa Spika, yamekuwepo madai ya kuwa wafanyabiashara
wamepoteza kujiamini kutokana na matamshi ya viongozi na hatua zilizochukuliwa
na Serikali bila kuwashirikisha wafanyabiashara ambazo zimezua hofu. Napenda
niwahakikishie wafanyabiashara kuwa, Serikali ya awamu ya tano inaamini kwa
dhati kuwa sekta binafsi ndiyo injini ya uchumi na inathamini sana na kupongeza
mchango mkubwa sana wa wafanyabiashara katika uchumi na maendeleo ya Taifa kwa
ujumla. Ni ukweli ulio dhahiri kwamba, sehemu kubwa ya uzalishaji wa bidhaa na
huduma mbalimbali kwa ajili ya matumizi nchini na mauzo nje yanayotupatia fedha
za kigeni unafanywa na sekta binafsi. Lakini pia sekta binafsi ndiyo mwajiri
mkuu na chanzo kikuu cha mapato ya Serikali. Hivyo, sekta binafsi ndiyo mbia
mkuu wa Serikali katika kazi ya kuharakisha maendeleo nchini.
31.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu mkubwa wa sekta binafsi
na wafanyabiashara, Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kujenga mazingira
mazuri ya kufanya biashara. Katika kuboresha mazingira ya biashara na
uwekezaji, Serikali iliendelea na jitihada za kuimarisha utulivu wa uchumi
jumla, kupunguza urasimu, kuharakisha maamuzi, kuimarisha ulinzi na usalama na
kuhakikisha upatikanaji wa miundombinu imara na huduma bora zikiwemo umeme wa
uhakika na mikopo kwa sekta binafsi. Hayo yote ni maeneo ambayo Serikali
iliyapa na itaendelea kuyapa kipaumbele. Aidha, Serikali bado ina dhamira ya
dhati kuendeleza mashauriano na wafanyabiashara kupitia utaratibu wa mikutano
ya Baraza la Taifa la Biashara, Taasisi ya Sekta Binafsi na makongamano
mengine.
32.
Mheshimiwa Spika, tumeanza kuona viashiria bora zaidi katika
eneo hili la kuboresha mazingira ya biashara. Taarifa ya Benki ya Dunia ya
mwaka 2017 ilionesha kuwa, Tanzania ilikuwa nchi ya 132 kwa urahisi wa kufanya
biashara ikiwa imepiga hatua kwa nafasi 12 kutoka nafasi ya 144 mwaka 2016.
Aidha, kwa mujibu wa taarifa ya “Fahirisi ya Uwekezaji Afrika ya mwaka 2016”
(Africa Investment Index, 2016) iliyotolewa na taasisi ya “Quantum Global Research Lab” ya Uingereza, Tanzania ilikuwa nchi ya
kwanza miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki kwa kuvutia uwekezaji na ya nane
kwa Afrika, ikiwa imepiga hatua kutoka nafasi ya 19 mwaka 2015.
33.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuzungumza na
wafanyabiashara ili kupata maoni na ushauri wao kuhusu sera mbalimbali na
mwenendo wa uchumi kwa ujumla na kutatua kero zao. Nia ya Serikali ni
kuhakikisha wanafanya biashara katika mazingira mazuri yanayotabirika ili
biashara hizo zikue na kushamiri, ajira ziongezeke na Serikali ipate kodi
stahiki kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo na huduma za jamii.
Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania itaendelea kuboresha mfumo wa kodi
na kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na kuwawezesha kufanya biashara
zao kwa urahisi. Aidha, Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kushirikiana na taasisi
nyingine za Serikali itaendelea na jitihada za kuelimisha umma juu ya umuhimu
wa kurasimisha shughuli zao za kiuchumi. Pamoja na kutoa elimu, napenda
kusisitiza kuwa, kulipa kodi ni wajibu wa msingi wa kila raia kwa maendeleo ya
Taifa. Lazima Watanzania tulipe kodi. Serikali hii haitavumilia uporaji wa
rasilimali za nchi na ukwepaji kodi kwa kivuli cha kulinda imani (confidence)
ya wafanyabiashara.
34.
Mheshimiwa Spika, napenda nitumie pia fursa hii niwakumbushe
watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwamba, kodi zinatozwa kwa kuongozwa na
sheria na kanuni zake. Matumizi ya vitisho na unyanyasaji kwa walipa kodi,
kuwadai rushwa au kuwazidishia makadirio ya kodi ili kuwakomoa ni mambo ya
hovyo na hayakubaliki hata kidogo! Wale watumishi wa TRA, ambao naamini ni
wachache tu, wanaojihusisha na vitendo hivyo, wakome kabisa kufanya hivyo. Wale
tutakaowabaini tutawachukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria za utumishi wa
umma. Aidha, natoa rai kwa wafanyabiashara wetu na wananchi wazalendo kutupatia
taarifa za ukweli kuhusu mwenendo mbaya wa mtumishi yeyote wa TRA ili zifanyiwe
kazi na Serikali. Nawaomba pia mfanye hivyo hivyo kutupatia taarifa kuhusu
wafanyabiashara wanaokwepa kodi ili tuwashughulikie ipasavyo.
II.
TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA
BAJETI YA MWAKA 2016/17
Mapato
35.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2016 hadi Aprili
2017, mapato kutoka vyanzo vyote yalifikia shilingi bilioni 20,710.5, sawa na
asilimia 70.1 ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 29,539.6. Mchanganuo wa mapato hayo ni kama ifuatavyo:
i.
Mapato ya kodi yalifikia shilingi bilioni 11,644.6 sawa na asilimia 77.1 ya
lengo la mwaka la kukusanya shilingi bilioni 15,105.1;
ii.
Mapato yasiyo ya kodi yalifikia shilingi bilioni 1,611.0 sawa na asilimia
59.8 ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 2,693.0;
iii.
Mapato ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa yalikuwa shilingi bilioni 399.3
sawa na asilimia 60.0 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 665.4 kwa mwaka;
iv.
Mikopo kutoka vyanzo vya ndani ilifikia Shilingi bilioni 4,715.6, sawa
na asilimia 87.7 ya shilingi bilioni 5,374.3 zilizotarajiwa kukopwa kwa mwaka
kutoka katika chanzo hiki; na
v.
Misaada na mikopo yenye masharti nafuu kutoka nje iliyopokelewa hadi
Aprili 2017 ni shilingi bilioni 2,340.1 sawa na asilimia 65.0 ya lengo la
shilingi bilioni 3,600.8 zilizoahidiwa na Washirika wa Maendeleo kwa mwaka
2016/17.
36.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2016/17, Serikali
ilipanga kukopa kiasi cha shilingi bilioni 2,100.9 kutoka kwenye vyanzo vya
kibiashara ili kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo lakini haikuweza
kukopa kutokana na hali ya soko la fedha la kimataifa kutokuwa nzuri. Hata
hivyo, Serikali inakamilisha majadiliano na wakopeshaji ambapo kiasi cha dola
za Marekani milioni 500 kinatarajiwa kupatikana kabla ya mwisho wa mwezi huu wa
Juni 2017.
Kudhibiti upotevu wa mapato
37.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17, Serikali imeendelea
kuchukua hatua mbalimbali katika kudhibiti upotevu wa mapato. Katika kutekeleza
azma hii, baadhi ya taasisi zimeanza kutumia mifumo ya kielektroniki katika
kukusanya mapato. Mfano, Halmashauri zinatumia Mfumo wa Ukusanyaji wa Mapato wa
Serikali za Mitaa (Local Government Revenue Collection System - LGRCS) na Jeshi
la Polisi katika Mkoa wa Dar es Salaam linatumia Mfumo wa Udhibiti wa Vyombo
vya Moto Barabarani (Traffic Management
System). Aidha, Serikali imekamilisha mfumo wa kielektroniki (Government
e-Payment Gateway System-GePGs) utakaotumika katika ukusanyaji wa mapato ya
Serikali. Mfumo utasaidia Serikali kuwa na uhakika wa mapato ya nayokusanywa
kutoka katika vyanzo mbalimbali kwa wakati na kurahisisha ulipaji wa kodi, tozo
na ada mbalimbali. Aidha, tarehe 01 Juni, 2017 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alizindua Mfumo mpya wa
ukusanyaji mapato kwa mjia ya kielektroniki. Mfumo huo unalenga kupata taarifa
sahihi za mlipakodi na mtoa huduma hususan makampuni ya simu, mabenki na
televisheni.
Ukusanyaji wa Kodi ya Majengo
38.
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 iliyopitishwa
na Bunge lako Tukufu inaipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jukumu la
kukusanya kodi ya majengo kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa zote nchini kuanzia
mwaka 2016/17. TRA ilipewa jukumu hili kutokana na kuwa na ufanisi katika
ukusanyaji na mtandao mpana ulioenea nchi nzima. Uamuzi huu haukuwa na maana ya
kupora chanzo hiki cha mapato kutoka katika halmashauri, bali kuongeza ufanisi
katika ukusanyaji wa kodi kutoka katika chanzo hiki.
39.
Mheshimiwa Spika, baada ya kupitishwa kwa Sheria hiyo, hatua
iliyofuata ilikuwa ni kutolewa kwa Tangazo la Serikali No. 276 la tarehe 30
Septemba 2016 lililoitaka TRA kuanza zoezi hilo kwa Halmashauri 30 za awali.
Jukumu la kukusanya kodi ya majengo katika halmashauri zilizobaki liliendelea
kubaki katika halmashauri husika. Katika kipindi hicho, Serikali kupitia TRA
ilifanya maandalizi ya taratibu na mifumo ya ukusanyaji. Maandalizi hayo yalihusisha
kutengeneza kanuni za ukusanyaji, kutengeneza mfumo wa ukusanyaji wa kodi hii,
kuunda kitengo, kuweka wafanyakazi na vitendea kazi kabla ya kuanza ukusanyaji.
40.
Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa taratibu hizo, TRA
ilianza rasmi kukusanya Kodi ya Majengo tarehe 1 Oktoba, 2016 katika majiji,
manispaa na miji 30. Hadi Mei, 2017, TRA imekusanya jumla ya Shilingi milioni
15,134.2. Ni matumaini ya Serikali kwamba kwa mwaka 2017/18, TRA itafanya
vizuri zaidi katika ukusanyaji wa kodi hii ya majengo. Maboresho ya kukusanya
kodi hiyo nitayaeleza baadae. Natoa rai kwa wadau wote wakiwemo wamiliki wa
majengo, viongozi wa halmashauri, wakuu wa wilaya na Mamlaka ya Mapato Tanzania
kushirikiana bega kwa bega kuhakikisha
wanafanikisha zoezi hili la ukusanyaji wa kodi ya majengo kwa maendeleo
ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Matumizi
41.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Aprili,
2017 jumla ya shilingi bilioni 20,036.5 zilitolewa kwa Wizara, Idara
zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kati ya
kiasi hicho, shilingi bilioni 15,480.9 zilizotolewa kwa ajili ya matumizi ya
kawaida sawa na asilimia 87.4 ya lengo la mwaka na shilingi bilioni 4,555.5
zilitolewa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo sawa na asilimia 38.5 ya lengo la
shilingi bilioni 11,820.5 zilizotengwa kwa ajili ya bajeti ya maendeleo kwa
mwaka. Fedha za maendeleo zilizotolewa zinajumuisha fedha za ndani shilingi
bilioni 3,647.7 na fedha za nje shilingi bilioni 907.8. Hata hivyo, baadhi ya
fedha za nje za kugharamia miradi ya maendeleo hazikujumuishwa kwenye matumizi
kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo: kuchelewa kupata thamani halisi ya
vifaa vilivyopelekwa moja kwa moja kwenye miradi kutokana na baadhi ya
Washirika wa Maendeleo kuendelea kupeleka fedha moja kwa moja kwenye miradi
bila kupitia mfumo wa malipo wa Serikali.
42.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya mahitaji yaliyopewa kipaumbele
katika utoaji wa fedha za matumizi ya maendeleo kati ya Julai, 2016 hadi
Aprili, 2017 ni pamoja na:-
i.
Ujenzi na ukarabati wa barabara kuu za Mikoa na
Halmashauri (Mfuko wa Barabara) shilingi bilioni 675.9;
ii.
Miradi ya ujenzi wa barabara ikiwemo ulipaji wa
madeni ya wakandarasi na wahandisi washauri shilingi bilioni 540.3;
iii.
Miradi ya uzalishaji wa umeme, uboreshaji wa njia
za kupitisha umeme na usambazaji wa umeme vijijini shilingi bilioni 421.5;
iv.
Mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu shilingi
bilioni 393.2;
v.
Malipo ya awali ya ujenzi wa reli kwa kiwango cha
‘standard gauge’ awamu ya kwanza katika eneo la Dar – Morogoro (Km 205)
shilingi bilioni 300;
vi.
Ununuzi wa ndege mbili na malipo ya awali ya
ununuzi wa ndege nne shilingi bilioni 234.9;
vii.
Usambazaji wa maji mijini na vijijini shilingi bilioni 186.4; na
viii.
Uboreshaji wa huduma za afya katika ngazi zote
shillingi bilioni 170.6 ikiwemo ununuzi wa dawa na vifaa tiba shilingi bilioni
156.1.
43. Mheshimiwa
Spika, utoaji wa fedha za
matumizi ya kawaida unajumuisha shilingi bilioni 5,320.3, sawa na asilimia 80.6
ya lengo la mwaka kwa ajili ya kugharamia mishahara; shilingi bilioni 7,775.5,
sawa na asilimia 97.2 ya lengo la mwaka kwa ajili ya kulipia Deni la Taifa na
shilingi bilioni 2,385.1, sawa na asilimia 76.5 ya lengo la mwaka kwa ajili ya
kugharamia matumizi mengineyo.
44.
Mheshimiwa Spika, maeneo yaliyopewa kipaumbele katika utoaji wa
fedha za matumizi mengineyo ni pamoja na:
i.
Kugharamia shughuli za vyombo vya ulinzi na
usalama shilingi bilioni 591.3;
ii.
Elimu msingi bila malipo shilingi bilioni 203.0;
iii.
Uendeshaji wa mitihani ya kitaifa shilingi bilioni
69.9;
iv.
Mfuko wa Bunge shilingi bilioni 69.1;
v.
Kugharamia balozi zetu nje ya nchi shilingi
bilioni 68.7;
vi.
Posho ya madaktari wanafunzi shilingi bilioni
15.3;
vii.
Ruzuku ya pembejeo shilingi bilioni 15.0;
viii.
Ruzuku ya vyama vya siasa shilingi bilioni 14.2;
na
ix.
Ununuzi wa chakula cha hifadhi ya Taifa shilingi
bilioni 13.0.
Kudhibiti matumizi
45. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2016/17, Sera za Matumizi ya Serikali zililenga kusimamia
nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti Na. 11 ya
mwaka 2015, Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma SURA 348, Sheria ya Fedha ya
Mamlaka za Serikali za Mitaa SURA 290, Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2013
SURA 410 na Kanuni husika, pamoja na miongozo mbalimbali ya Serikali. Lengo kuu
lilikuwa ni kupunguza matumizi yasiyo na tija, kuziba mianya ya ufujaji wa
fedha za umma na kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye maeneo ya kipaumbele.
46.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17 Serikali imeendelea
kudhibiti matumizi katika maeneo mbalimbali ikiwemo: kupunguza safari za nje
kwa kuhakikisha kuwa vibali vinatolewa kwa safari zenye manufaa kwa Taifa;
kudhibiti matumizi ya umeme, simu na maji kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara;
na kuendelea kudhibiti gharama za uendeshaji wa magari ikiwa ni pamoja na
matengenezo, mafuta na vilainishi. Aidha, utaratibu wa kufanya mikutano na makongamano
katika kumbi za Serikali na taasisi za umma umeongeza udhibiti wa matumizi ya
Serikali.
Malimbikizo, uhakiki na
ulipaji wa Madai
47.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Juni, 2016 madai
yaliyokuwa yamewasilishwa na taasisi mbalimbali yalikuwa jumla ya shilingi
bilioni 2,934.4 ambapo jumla ya shilingi bilioni 1,997.9 sawa na asilimia 68.1
zilithibitika kuwa madai halali baada ya uhakiki. Kati ya madai yaliyohakikiwa,
Serikali imelipa jumla ya shilingi bilioni 796.5 hadi mwezi Machi, 2017 na
hivyo kubakia na madai ya shilingi bilioni 1,201.4. Kati ya madai hayo
yaliyolipwa, shilingi bilioni 632.1 ni kwa ajili ya wakandarasi na wahandisi
washauri; shilingi bilioni 78.9 kwa ajili ya wazabuni wa huduma na bidhaa
ikiwemo shilingi bilioni 11.2 za Bohari Kuu ya Madawa (MSD); shilingi bilioni
67.6 kwa ajili ya malimbikizo ya madai ya watumishi; na shilingi bilioni 17.9
ni kwa ajili ya watoa huduma mbalimbali.
48.
Mheshimiwa
Spika, kati ya Julai hadi Desemba 2016, malimbikizo ya madai mapya kutoka
kwenye taasisi mbalimbali yalikuwa jumla ya shilingi bilioni 899.55. Hivyo,
hadi Desemba 2016, madai yote yalifikia shilingi bilioni 2,100.90. Madai hayo
yamegawanyika kama ifuatavyo: shilingi bilioni 910.30 wakandarasi; shilingi
bilioni 890.16 ni wazabuni wa huduma na bidhaa; shilingi bilioni 159.10 ni madai ya watumishi
mbalimbali; shilingi bilioni 75.45 ni ankara za maji,umeme na simu; na shilingi
bilioni 65.89 ni pango la ofisi. Aidha, kati ya madai ya wazabuni wa huduma na
bidhaa, lipo deni la MSD ambalo ni shilingi bilioni 145.89 linalotokana na
malimbikizo ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba vilivyochukuliwa na taasisi
mbalimbali za serikali na havikuwa vimelipiwa.
Deni la Taifa
49.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia Deni la Taifa
kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134. Ili kuhakikisha
kuwa deni la Taifa linaendelea kusimamiwa ipasavyo, Bunge lako Tukufu
lilipitisha marekebisho ya Sheria hiyo mwezi Novemba, 2016. Baadhi ya maeneo
yaliyorekebishwa ni pamoja na: kuongeza masharti kwa Taasisi na Mashirika ya
Umma yanayoomba dhamana ya Serikali ili kudhibiti utoaji wa dhamana hizo;
kuweka utaratibu maalum wa kisheria ambao unahakikisha kwamba fedha zilizokopwa
na Serikali ya Muungano kwa lengo la kugharamia miradi ya maendeleo Zanzibar
inafika kama ilivyokusudiwa; na kuongeza wajumbe kutoka Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar katika Kamati ya Kitaifa ya Kusimamia Deni la Taifa.
50.
Mheshimiwa Spika, Hadi Machi 2017, deni la Taifa lilifikia
shilingi bilioni 50,806.5. Kati ya kiasi hicho, deni la Serikali ni shilingi
bilioni 42,883.6 na deni la sekta binafsi ni shilingi bilioni 7,922.9. Deni la
Serikali limeongezeka kwa asilimia 9.2 kutoka shilingi
bilioni 39,274.6 Machi, 2016 hadi shilingi bilioni 42,883.6 Machi,
2017. Ongezeko la deni la Serikali lilitokana
na mikopo mipya na ya zamani iliyopokelewa katika kipindi cha mwaka 2016/17
kutoka vyanzo vya masharti nafuu na ya kibiashara, malimbikizo ya riba ya deni
la nje kwenye nchi zisizo wanachama wa kundi la Paris ambazo zinatakiwa kutoa
msamaha wa madeni lakini bado hazijatoa pamoja na kushuka kwa thamani ya
shilingi dhidi ya dola za Marekani.
51.
Mheshimiwa Spika, deni la Serikali linajumuisha deni la ndani
la shilingi bilioni 12,073.7 sawa na asimilia 28.1 na deni la nje la shilingi
bilioni 30,809.9 sawa na asilimia 71.9. Deni la nje linajumuisha mikopo ya
masharti nafuu kutoka kwenye mashirika ya fedha ya kimataifa, sawa na asilimia
56.8, mikopo kutoka nchi wahisani ilifikia asilimia 16.3 na mikopo kutoka
mabenki ya kibiashara ya kimataifa ilifikia asilimia 26.9 ya deni lote la
nje. Mikopo hiyo ilitumika kugharamia
miradi ya maendeleo hususan katika sekta za ujenzi (barabara na reli), nishati,
uchukuzi, elimu na maji.
Tathmini ya Uhimilivu wa Deni
la Taifa
52.
Mheshimiwa Spika, matokeo ya tathmini ya uhimilivu wa deni
iliyofanyika mwezi Novemba, 2016 yalibainisha kuwa Deni la Taifa ni himilivu
kwa muda mfupi, wa kati na mrefu. Katika tathmini hiyo, viashiria vinaonesha
kuwa: thamani ya sasa ya jumla ya Deni la Taifa (Present Value of Total Public
Debt) kwa Pato la Taifa ni asilimia 34.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia
56; thamani ya sasa ya Deni la nje (Present Value of External Debt) kwa Pato la Taifa ni asilimia 19.9
ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40; thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 97.7
ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 150; na thamani ya sasa ya deni la nje kwa
mapato ya ndani ni asilimia 145.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 250.
Viashiria hivyo vinapima uwezo wa nchi kukopa bila kuathiri uhimilivu wa deni (solvency
indicators).
53.
Mheshimiwa Spika, kutokana na tathmini ya uhimilivu wa deni la
Taifa, ambayo inapima uwezo wa nchi kulipa deni, uwiano wa ulipaji wa deni la
nje kwa kutumia mapato ya ndani umefikia asilimia 11.5 ikilinganishwa na ukomo
wa asilimia 20 na uwiano wa ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mauzo ya bidhaa
nje ni asilimia 7.8 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20. Kwa kuzingatia
viashiria hivyo, ambavyo vipo chini ya ukomo unaokubalika kimataifa, Tanzania
bado ina uwezo wa kuendelea kukopa kutoka ndani na nje ya nchi ili kugharamia
shughuli zake za maendeleo na pia ina uwezo wa kulipa mikopo inayoiva kwa
kutumia mapato yake ya ndani na nje.
III.
SERA ZA BAJETI KWA MWAKA 2017/18
54.
Mheshimiwa
Spika,
kwa mujibu wa makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,
dhima ya Bajeti ya mwaka 2017/18 ni “kujenga uchumi wa viwanda utakao
chochea ajira na ustawi endelevu wa jamii”. Hii inaendana na msisitizo na
vipaumbele vya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya
kujenga Tanzania ya viwanda.
Shabaha
za Uchumi Jumla
55.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa bajeti ya 2017/18 unalenga
kufikia shabaha za uchumi jumla kama ifuatavyo:
i.
Pato halisi la Taifa kukua kwa asilimia 7.1 mwaka
2017 kutoka asilimia 7.0 mwaka 2016;
ii.
Kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei katika wigo wa
tarakimu moja kati ya asilimia 5.0 na asilimia 8.0 mwaka 2017;
iii.
Mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya halmashauri
kufikia asilimia 15.8 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17, na kuendelea kuongezeka
kufikia asilimia 16.5 ya Pato la Taifa mwaka 2017/18;
iv.
Mapato ya kodi yanakadiriwa kuongezeka kufikia
asilimia 14.2 ya Pato la Taifa mwaka 2017/18 kutoka matarajio ya asilimia 13.3
ya Pato la Taifa mwaka 2016/17;
v.
Matumizi ya Serikali yanatarajiwa kuongezeka
kufikia asilimia 26.2 ya Pato la Taifa mwaka 2017/18 kutoka matarajio ya asilimia 23.7 ya Pato la Taifa
mwaka 2016/17;
vi.
Nakisi ya bajeti inatarajiwa kupungua kufikia
asilimia 3.8 ya Pato la Taifa kutoka asilimia 4.5 ya Pato la Taifa mwaka
2016/17;
vii.
Nakisi katika urari wa malipo ya kawaida inatarajiwa
kuwa asilimia 7.0 ya Pato la Taifa mwaka
2017/18; na
viii.
Kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayotosheleza
mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua
miezi minne.
Sera
za Mapato
56.
Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuongeza na kuimarisha
ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kutekeleza sera zifuatazo:
i.
Kuendelea kusimamia kikamilifu matumizi ya vifaa
na mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ili kuongeza ufanisi na
kudhibiti upotevu wa mapato;
ii.
Kuendelea kupanua wigo wa walipa kodi ikiwa ni
pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iweze kuingia katika mfumo wa kodi;
iii.
Kuimarisha ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi na
kuboresha usimamizi wake;
iv.
Kuendelea kufanya uthamini wa majengo na kusimamia
ulipaji ili kuongeza mapato yatokanayo na kodi ya majengo;
v.
Kurasimisha miliki za ardhi kwa lengo la kuongeza
mapato; na
vi.
Kuendelea kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi
isiyo na tija.
57.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18,
Serikali itaendelea kupanua soko la fedha la ndani ili kuwa na washiriki wengi
kutoka ndani na nje ya nchi kwenye soko watakaowezesha Serikali kupata fedha za
kuziba nakisi kwenye bajeti kwa riba nafuu. Serikali itahakikisha kuwa,
mchakato wa upatikanaji wa fedha za mikopo yenye masharti ya kibiashara
unaharakishwa kwa kuzingatia maslahi ya Taifa na kuhakikisha fedha
zitakazopatikana zinaelekezwa katika miradi ya maendeleo.
58.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za Serikali kutaka kuimarisha
ushirikiano kati yake na Washirika wa Maendeleo, na kuhakikisha fedha
zinazoahidiwa zinatolewa kwa wakati, Serikali na Washirika wa Maendeleo
walitafuta Washauri Elekezi Huru. Timu hiyo iliongozwa na Dkt. Donald P.
Kaberuka, aliyekuwa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika. Washauri Elekezi
walipewa kazi ya kutathmini na kutoa mapendekezo ya kuimarisha ushirikiano kati
ya Serikali na Washirika wa Maendeleo na muundo wa utoaji fedha.
59. Mheshimiwa Spika, baadhi ya mapendekezo
ya Washauri Elekezi katika kuimarisha ushirikiano yanajumuisha:
i.
Kuanzisha
Majadiliano Thabiti: Majadiliano hayo yanalenga kufanya mapitio na
kuimarisha Mchakato wa Mapitio ya Matumizi ya Umma (PER), kupata matokeo kwenye
ngazi ya kisekta pamoja na namna ya kushughulikia masuala nyeti pasipo kuathiri
mchakato wa Bajeti.
ii.
Kujenga
Uwezo wa Kitaasisi: Lengo ni kujenga ujuzi wa kiwango cha juu
kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo namna ya kufanya majadiliano ya kuvuna
maliasili, masuala ya usimamizi wa fedha, sera za biashara, usimamizi wa deni
la nje na utafiti na uchambuzi wa sera.
iii.
Kugharamia
Azma ya Serikali Kuleta Maendeleo: Hii itahusisha kutafuta
fedha kupitia ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya Umma. Misaada na Mikopo ya
Kibajeti (GBS) bado inaweza kutumiwa katika maeneo mahsusi kama vile kulipia
madeni ya Serikali.
60. Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza
kufanyia kazi mapendekezo ya Washauri Elekezi kwa kukamilisha Mwongozo wa
Ushirikiano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo. Mwongozo huu unaainisha
masuala mbalimbali ikiwemo: Misingi ya ushirikiano; muundo wa majadiliano; na
mifumo ya misaada inayoendana na mahitaji ya nchi. Ni matarajio ya Serikali
kwamba, hatua hii itasaidia kuimarisha ushirikiano na hivyo kuwawezesha
Washirika wa Maendeleo kutimiza ahadi zao kwa kutoa fedha kwa wakati.
Sera za Matumizi
61.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Serikali itaendelea
kuhakikisha kuwa fedha zinaelekezwa kwenye maeneo ya vipaumbele ili kutekeleza
kikamilifu Mpango wa Maendeleo wa Mwaka. Nidhamu ya hali ya juu katika matumizi
lazima isimamiwe kwa nguvu zote ili kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana.
Ili kufikia azma hiyo, Serikali itafanya yafuatayo:
i.
Kuendelea kuhakikisha kuwa Mashirika ya Umma
yaliyoundwa kwa lengo la kujiendesha kibiashara, yanajiendesha kwa faida bila
kutegemea ruzuku ya Serikali;
ii.
Kuhakikisha mikataba inayoingiwa na Serikali na
Taasisi zake inakuwa katika shilingi za Kitanzania isipokuwa kwa mikataba
inayohusisha biashara na huduma za
kimataifa;
iii.
Kuendelea kudhibiti matumizi ya umeme, simu na
maji ikiwa ni pamoja na kutumia teknolojia zinazopunguza gharama katika
matumizi hayo;
iv.
Kuendelea kudhibiti ulipaji wa mishahara kwa
kulipa watumishi wanaostahili; na
v.
Kutumia
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kufanikisha mawasiliano
katika shughuli za Serikali.
62.
Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti ulimbikizaji wa madeni, Serikali itachukua hatua
zifuatazo:
i.
Kutokufanya matumizi pasipokuwa na kasma
iliyoidhinishwa kwenye bajeti ya Fungu husika;
ii.
Kuhakikisha kuwa uagizwaji wa bidhaa unafanyika
baada ya kutolewa kwa hati ya ununuzi (LPO) kwenye mfumo rasmi wa malipo
(IFMS);
iii.
Kuhakikisha kuwa ahadi (Commitment) inafanyika
baada ya kupatikana kwa fedha na kutoingia mikataba bila kuwa na ridhaa ya
matumizi; na
iv.
Kuhakikisha kuwa makubaliano ya kukopa yanafanyika
baada ya kupata kibali cha maandishi kutoka kwa Waziri wa Fedha na Mipango kama
ilivyoelekezwa kwenye Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134 pamoja na
marekebisho yake.
Maeneo
ya vipaumbele kwa mwaka 2017/18
63.
Mheshimiwa Spika, Mpango
wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2017/18 ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa
Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2016/17 – 2020/21. Kama nilivyoeleza kwenye hotuba ya Hali ya Uchumi
kwa mwaka 2016, maeneo ya kipaumbele yanaakisi Mpango wa Miaka Mitano, hususan:
i.
Kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda;
ii.
Kufungamanisha uchumi na maendeleo ya watu;
iii.
Kujenga mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara
na uwekezaji; na
iv.
Kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa Mpango.
64. Mheshimiwa Spika, Mpango huu umeweka
msisitizo katika kufanikisha utekelezaji wa Miradi Mikubwa ya Kielelezo, ambayo ni:-
Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Standard
Gauge; Kuhuisha Shirika la Ndege Tanzania; Miradi ya Chuma Liganga na Makaa
ya Mawe Mchuchuma – Njombe; Uanzishwaji wa Kanda Maalum za Kiuchumi; Mradi wa
Gesi Kimiminika (Liquefied Natural Gas
- LNG); Kituo cha Biashara cha Kurasini; Shamba la Kilimo na Uzalishaji
Sukari Mkulazi; na Kusomesha Vijana wa Kitanzania kwa wingi kwenye fani na
ujuzi maalum kwa ajili ya maendeleo ya watu na viwanda na kukuza sayansi,
teknolojia na ubunifu.
IV.
HATUA ZA MAPATO NA MABORESHO
YA MFUMO WA KODI, ADA NA TOZO MBALIMBALI
A. Hatua za Kisera na Kiutawala
65.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuchukua
hatua mbalimbali za kisera na kiutawala ili kuimarisha na kurahisisha
ukusanyaji mapato. Hatua hizo ni pamoja na:-
i.
Kuimarisha
mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa kutumia vifaa na mifumo ya kielektroniki ili
kuzuia uvujaji wa mapato ya Serikali.
Mfumo uitwao “Government e-payment Gateway System” uko tayari kwa ajili
ya matumizi ya Wizara, Idara na Taasisi za Serikali. Wizara, Idara na Taasisi
zote za Serikali zinaagizwa zianze kutumia mfumo huu;
ii.
Serikali
imezindua mfumo mpya wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki (Electronic
Revenue Collection System (e-RCS)) ambao utadhibiti udanganyifu unaofanywa na
maafisa wa Serikali kwa kushirikiana na walipa kodi katika kukadiria kodi
sahihi. Aidha, mfumo huu utawasaidia walipa kodi kwa kuwa na uhakika wa kiasi
cha kodi wanayopaswa kulipa. Mfumo huo wa e-RCS utaanza rasmi katika mwaka huu
wa fedha kwa usimamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa upande wa Bara na Mamlaka ya Mapato Zanzibar
(ZRB) kwa upande wa Zanzibar;
iii.
Katika mwaka wa fedha 2017/18, Serikali itaendelea na ukusanyaji wa kodi
ya majengo (yaliyothaminiwa na yasiyothaminiwa) kwenye halmashauri zote nchini.
Jukumu hili litasimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Mamlaka ya
Mapato Tanzania. Serikali
itatoza Kodi ya Majengo kwa nyumba zote kwa viwango vitakavyopangwa na Waziri
na Fedha na Mipango. Nyumba ambazo hazijafanyiwa uthamini zitatozwa kwa kiwango
maalum (flat rate) cha
shilingi elfu kumi (10,000) kwa nyumba na shilingi elfu hamsini (50,000) kwa
nyumba za ghorofa kwa kila ghorofa;
iv.
Kuwatambua rasmi wafanyabiashara wadogo wadogo wasio rasmi na wanaofanyia biashara katika
maeneo yasiyo rasmi mfano mama lishe, wauzaji mitumba wadogo, wauza mazao ya
kilimo wadogo kama mboga mboga, ndizi, matunda, na
kadhalika kwa kuwapatia vitambulisho maalum vya kazi wanazozifanya;
v.
Kuendelea kusimamia na kuhimiza
matumizi ya mashine za kielektroniki (EFDs) kwenye Wizara, Idara, Taasisi za Serikali na kwa wafanyabiashara;
vi.
Serikali itafungua akaunti maalum (Escrow
Account) kuanzia mwezi Julai 2017 ili kurahisisha na kuhakikisha kwamba
marejesho ya Ushuru wa Forodha wa ziada (Additional Import Duty) wa asilimia 15
unaolipwa na waagizaji wa sukari ya viwandani yanafanyika kwa wakati. Hatua hii
itaiwezesha Mamlaka ya Mapato kufanya marejesho kwa wakati kwa wazalishaji
wanaotumia sukari hiyo katika kuzalisha bidhaa mbalimbali; na
vii.
Serikali
kutoruhusu usafirishaji wa madini kutoka migodini na kupeleka moja kwa moja nje
ya nchi. Aidha, Serikali itaanzisha maeneo maalum (clearing houses) katika
viwanja vya kimataifa, migodini, na kadhalika ambapo madini hayo
yatathibitishwa na kupewa kibali cha kusafirisha madini hayo ambacho kitatozwa
ada ya asilimia moja (clearing fee) ya thamani ya madini hayo.
B.
Maboresho ya Mfumo wa Kodi, Ada na Tozo
Mbalimbali
66.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua za kisera na
kiutawala za kuboresha ukusanyaji wa mapato, napenda kuwasilisha mapendekezo ya
kufanya marekebisho ya mfumo wa kodi ikiwemo kurekebisha baadhi ya viwango vya
kodi, tozo na ada chini ya sheria mbalimbali. Aidha, marekebisho haya yanalenga
pamoja na mambo mengine, kuongeza mapato ya Serikali; kuchochea kasi ya ukuaji
wa uchumi hususan katika sekta ya viwanda, kilimo, usafirishaji na kukuza
ajira. Aidha, kama nilivyoeleza awali, marekebisho haya hayataathiri kwa
kiwango kikubwa utulivu na utabirifu wa mfumo wa kodi. Marekebisho hayo ni
pamoja na Sheria zifuatazo:-
a.
Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA
148;
c.
Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147;
d.
Sheria
ya Usalama Barabarani, SURA 168;
e.
Sheria ya
Fedha ya Serikali za Mitaa, SURA 290;
f.
Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki ya mwaka 2004;
g.
Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya
Sheria za Kodi na Sheria nyingine mbalimbali; na
h.
Marekebisho ya Ada na Tozo mbalimbali
zinazotozwa naWizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea.
a)
Sheria ya Kodi ya
Ongezeko la Thamani, SURA 148
67.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho
kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura 148 kama ifuatavyo:-
i.
Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye bidhaa za mtaji (capital goods) ili kupunguza
gharama za ununuzi/uagizaji wa mashine na mitambo ya kuzalishia na hivyo
kuvutia uwekezaji katika sekta ya viwanda. Aidha, hatua hii itahusisha viwanda vya mafuta ya kula, nguo, ngozi,
madawa ya binadamu na mifugo. Lengo la hatua hii ni kuvutia uwekezaji katika
sekta za viwanda, kilimo cha mazao na mifugo, na kukuza ajira na uchumi wa
nchi. Aidha, hatua hii itawezesha viwanda vidogo na vya kati kupata unafuu wa
gharama za kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa mashine na mitambo
watakayonunua kwa ajili ya kusindika na kutengeneza bidhaa mbalimbali. Mitambo
na mashine zote zitakazosamehewa Kodi ya Ongezeko la Thamani zitaainishwa kwa
kutumia HS Codes;
ii.
Kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa
kiwango cha asilimia sifuri katika
huduma zinazotolewa kwenye usafirishaji wa bidhaa/mizigo nje ya nchi (ancillary transport
services). Lengo la hatua hii ni
kupunguza gharama za usafirishaji katika bandari zetu kwa kuifanya Tanzania kuwa njia bora zaidi ya kupitisha bidhaa zinazotoka nje
ya nchi kwenda nchi nyingine
hususan zisizo na bandari (landlocked countries). Hatua hii itahamasisha wasafirishaji kutoka nchi jirani
kupitisha mizigo yao kwa wingi kwenye bandari zetu na hivyo kukuza uchumi
wa nchi kutokana na kuongezeka kwa mapato ya bandari. Vile vile kukua kwa sekta ya bandari
kutachangia kuongezeka kwa ajira nchini;
iii.
Kusamehe
Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye vyakula vya mifugo (compounded animal feeds)
vinavyotengenezwa hapa nchini vinavyotambulika kwenye HS Code 2309. Lengo la
hatua hii ni kupunguza gharama za kununua vyakula hivyo kwa wafugaji; na
iv.
Kufanya
marekebisho kwenye sehemu ya kwanza ya jedwali la misamaha ya kodi kipengele
cha 3(13) ili kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye mayai ya kutotolesha
vifaranga (fertilized eggs for incubation). Lengo la hatua hii ni kupunguza
gharama za uzalishaji wa vifaranga na kukuza sekta ndogo ya ufugaji ili iweze
kuongeza mchango wake katika pato la Taifa.
Hatua
hizi zote za Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa ujumla wake zinatarajiwa kupunguza
mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi
milioni 48,034.1.
b)
Sheria ya Kodi ya Mapato,
SURA 332
68.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho
kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura
332 kama ifuatavyo:-
i.
Kufanya marekebisho kwenye aya ya nne ya Jedwali la Kwanza la Sheria ya
Kodi ya Mapato ili kurekebisha muda uliotolewa katika kutoza kodi mbadala
(Alternative Minimum Tax) kwa kampuni zinazopata hasara kwa miaka mitatu
mfululizo badala ya miaka mitano mfululizo. Lengo la hatua hii ni kuoanisha na
aya ya nne ya kifungu cha nne cha sheria hiyo kinachotamka kwamba kodi hiyo
inatozwa kwa miaka mitatu mfululizo;
ii.
Kufanya
marekebisho kwenye Jedwali la Tatu la Sheria ya Kodi ya Mapato ili kuongeza kiwango cha juu
kinachotumika kama gharama ya kukokotoa uchakavu wa magari yasiyo ya kibiashara (non-commercial motor vehicles) kutoka shilingi milioni 15 hadi shilingi
milioni 30. Lengo la hatua hii
ni kufanya/kuhuisha gharama za magari hayo ziendane na gharama za halisi za soko. Marekebisho haya yamezingatia kwamba kiwango cha sasa cha shilingi milioni 15 ni
cha muda mrefu na hakiakisi bei halisi ya magari kwa sasa katika soko;
iii.
Kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato ili kupunguza kiwango cha Kodi ya Mapato ya Makampuni (Corporate Income Tax) kutoka asilimia 30 mpaka asilimia 10 kwa miaka mitano kuanzia mwaka mwekezaji atakapoanza uzalishaji, kwa waunganishaji (assemblers) wa magari, matrekta na boti za uvuvi. Lengo la hatua hii ni kuongeza ajira, kuongeza mapato ya Serikali na pia kuhamasisha uhaulishaji wa teknolojia (technology transfer). Aidha, Serikali itaingia mkataba wa makubaliano na utekelezaji (Performance Agreement) na kila muunganishaji ambao utaainisha wajibu wa kila upande; na
iv.
Kuanza kutoza Kodi ya Zuio (Withholding Tax) kwa kiwango cha asilimia 5
kwenye bei ya kuuzia (total market value) ambayo itakua ni Kodi ya Zuio ya
mwisho (final Withholding Tax) kwa wachimbaji wadogo wadogo wa madini ya aina zote. Lengo la hatua hii ni kuiwezesha Serikali kupata
mapato stahiki kutoka katika sekta ya madini.
Hatua
hizi za Kodi ya Mapato kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali
kwa kiasi cha shilingi milioni 88.5.
c)
Sheria ya Ushuru wa
Bidhaa, SURA 147
69.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho
kwenye Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147 kama ifuatavyo: -
i.
Kufanya marekebisho ya viwango maalum vya ushuru (specific duty rates)
vinavyotozwa kwenye bidhaa zisizo za petroli kwa kiwango cha mfumuko wa bei cha
asilimia 5. Sababu yake ni kuwa pale ambapo Ushuru wa Bidhaa unatozwa kwa
viwango maalum (specific rates) ushuru huo hauakisi mfumuko wa bei na hivyo
hupunguza mapato. Njia bora inayotumika kuondoa mapungufu hayo ni kurekebisha
viwango maalum vya ushuru ili kuendana na kiwango cha mfumuko wa bei. Utaratibu
huu ni tofauti na pale ambapo Ushuru wa Bidhaa hutozwa kwa kiwango cha asilimia
ya thamani ya bidhaa (advalorem rates) ambapo hapana sababu ya kurekebisha
viwango vya ushuru kwa kuwa thamani ya bidhaa inazingatia mfumuko wa bei. Aidha, marekebisho haya ninayopendekeza ni
kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Bidhaa Kifungu cha 124(2) inayoelekeza kuwa
marekebisho ya viwango vya ushuru yanaweza kufanyika kila mwaka ili
kuviwianisha na mfumuko wa bei na viashiria vingine vya uchumi jumla. Hata
hivyo, kwa kuzingatia Mkakati wa Taifa wa kukuza uchumi wa viwanda, baadhi ya
bidhaa zinazozalishwa nchini hazitafanyiwa marekebisho hayo. Mabadiliko
ninayopendekeza ni kama ifuatavyo:-
a.
Ushuru wa Bidhaa kwenye vinywaji baridi kutoka shilingi 58 kwa lita hadi
shilingi 61 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 3 kwa lita;
b.
Ushuru wa Bidhaa kwenye maji ya kunywa yaliyosindikwa kwenye chupa
yaliyoagizwa kutoka nje kutoka shilingi 58 kwa lita hadi shilingi 61 kwa lita
ikiwa ni ongezeko la shilingi 3 kwa lita. Aidha, Ushuru wa Bidhaa kwenye maji
yanayozalishwa nchini utabaki kuwa shilingi 58 kwa lita;
c.
Ushuru wa Bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda
yanayozalishwa hapa nchini (local juices) utashuka kutoka shilingi 9.5 kwa lita
na kuwa shilingi 9.0 kwa lita;
d.
Ushuru wa Bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda
ambayo hayazalishwi hapa nchini (imported juices) kutoka shilingi 210 kwa lita
hadi shilingi 221 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 11 kwa lita;
e.
Ushuru wa Bidhaa kwenye bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini na
ambayo haijaoteshwa (Beer
from Local Unmalted Cereals) kutoka shilingi 429 kwa lita hadi shilingi 450 kwa lita ikiwa ni ongezeko
la shilingi 21 kwa lita;
f.
Ushuru wa Bidhaa kwenye bia nyingine zote kutoka shilingi 729 kwa lita hadi
shilingi 765 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 36 kwa lita;
g.
Ushuru wa Bidhaa kwenye bia zisizo za kilevi, ikijumuisha vinywaji vya
kuongeza nguvu kutoka shilingi 534 kwa lita hadi shilingi 561 kwa lita ikiwa ni
ongezeko la shilingi 27 kwa lita;
h.
Ushuru wa Bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa
ndani ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 75, utashuka kutoka shilingi 202
kwa lita na kuwa shilingi 200 kwa lita;
i.
Ushuru wa Bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje
ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, kutoka shilingi 2,236 kwa lita
hadi shilingi 2,349 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la shilingi 113 kwa lita;
j.
Ushuru wa Bidhaa kwenye vinywaji vikali vinavyoagizwa kutoka nje kutoka
shilingi 3,315 kwa lita hadi shilingi 3,481 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la
shilingi 166 kwa lita. Aidha,Ushuru wa Bidhaa kwenye vinywaji vikali
vinavyozalishwa nchini utabaki kuwa shilingi 3, 315 kwa lita;
k.
Ushuru wa Bidhaa kwenye sigara zisizo na kichungi zinazotengenezwa kutokana
na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 11,854
hadi shilingi 12,447 kwa kila sigara elfu moja, ikiwa ni ongezeko la shilingi
593 kwa kila sigara elfu moja;
l.
Ushuru wa Bidhaa kwenye sigara zenye kichungi zinazotengenezwa kutokana na
tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 28,024
hadi shilingi 29,425 kwa kila sigara elfu moja, ikiwa ni ongezeko la shilingi
1,401 kwa kila sigara elfu moja;
m.
Ushuru wa Bidhaa kwenye sigara zenye sifa tofauti na (k) na (l) kutoka
shilingi 50,700 hadi shilingi 53,235 kwa kila sigara elfu moja ikiwa ni
ongezeko la shilingi 2,535 kwa kila sigara elfu moja;
n.
Ushuru wa Bidhaa kwenye tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara (cut
filler) kutoka shilingi 25,608 hadi shilingi 26,888 kwa kilo, ikiwa ni ongezeko
la shilingi 1,280 kwa kilo; na
o.
Ushuru wa Bidhaa wa ‘cigar’ unabaki kuwa asilimia 30.
ii.
Kufuta Ada ya Mwaka ya Leseni ya Magari (Annual Motor
Vehicle Licence Fee) iliyokuwa inalipwa hata kwa magari ambayo hayatumiki
ambayo imekuwa ikilalamikiwa kwa muda mrefu, badala yake ada hiyo itatozwa kwa
magari yanayotembea tu, kwa sababu hiyo, Ushuru wa Bidhaa kwenye mafuta ya
petroli, dizeli na taa utaongezeka kwa kiasi cha shilingi 40 kwa lita moja
kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 339 kwa lita hadi shilingi 379 kwa lita
kwa mafuta ya petroli, kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 215 kwa lita hadi
shilingi 255 kwa lita kwa mafuta ya dizeli na kutoka kiwango cha sasa cha
shilingi 425 kwa lita hadi shilingi 465 kwa lita kwa mafuta ya taa. Lengo la
hatua hii ni kuwaondolea wananchi usumbufu wa kudaiwa ada hii hata kwa magari
ambayo hayatumiki.
Hatua
za Ushuru wa Bidhaa kwenye bidhaa zisizo za petroli kwa ujumla wake
zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 27,801.8.
d)
Sheria ya Usalama Barabarani, SURA 168
70.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho
kwenye Sheria ya Usalama Barabarani, Sura 168 kama ifuatavyo;
i.
Kufuta Ada ya Mwaka ya Leseni ya Magari (Annual Motor
Vehicle Licence Fee) ili
ada hii ilipwe mara moja tu gari linaposajiliwa na baada ya hapo iendelee
kulipwa kupitia Ushuru wa Bidhaa kwenye mafuta ya petroli na dizeli kwa
kuongeza Ushuru wa Bidhaa kwenye mafuta ya petroli, dizeli na taa kama
ilivyoainishwa katika aya ya 69(ii). Aidha, Serikali
inatoa msamaha wa kodi, riba na adhabu zinazoambatana na madeni yote (Tax
Amnesty) ya ada hiyo yaliyolimbikizwa kwa miaka ya nyuma.
Inapendekezwa pia kuongeza Ada ya
Leseni ya Magari wakati wa usajili mara ya kwanza (Annual Motor Vehicle Licence
Fee on first registration). Ongezeko la Ada ya Leseni ya Magari wakati wa
usajili ni kama ifuatavyo;
a.
Gari
lenye ujazo wa injini ya 501-1500 cc kutoka kiwango cha sasa cha shilingi
150,000 hadi shilingi 200,000, ikiwa ni ongezeko la shilingi 50,000;
b.
Gari
lenye ujazo wa injini ya 1501-2500 cc kutoka kiwango cha sasa cha shilingi
200,000 hadi shilingi 250,000, ikiwa ni ongezeko la shilingi 50,000; na
c.
Gari
lenye ujazo wa injini ya 2501 cc na zaidi kutoka kiwango cha sasa cha shilingi
250,000 hadi shilingi 300,000, ikiwa ni ongezeko la shilingi 50,000.
Hatua
hizi kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 77,603.5.
e)
Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, SURA 290
71.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho
kwenye Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290 ili kupunguza Ushuru wa
Mazao (Produce Cess) unaotozwa na Halmashauri za Wilaya kutoka kiwango cha sasa
cha asilimia 5 ya thamani ya mauzo (Gross Value) hadi asilimia 3 kwa mazao ya
biashara na asilimia 2 kwa mazao ya chakula. Aidha Mtu anayesafirisha mazao
yake kutoka Halmashauri moja kwenda nyingine yasiyozidi tani moja (1) asitozwe
Ushuru. Lengo la hatua hii ni kuwawezesha wakulima kulipwa bei stahiki ya mazao
yao na hivyo kuboresha mapato yao. Hatua hii inatarajiwa kuhamasisha uzalishaji
wa mazao.
f)
Sheria ya Forodha ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004
72.
Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki walifanya kikao cha maandalizi ya Bajeti tarehe 6 Mei, 2017
mjini Arusha, Tanzania. Kikao hicho kilipendekeza kufanya marekebisho ya
viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha (EAC- Common External Tarrif “CET”) na
Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Customs Management Act,
2004) kwa mwaka wa Fedha 2017/18. Mapendekezo hayo yanalenga kwa kiwango kikubwa
katika kukuza viwanda ndani ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
kwa lengo la kuongeza ajira na kunufaisha watu wote.
73.
Mheshimiwa Spika, maeneo yaliyopendekezwa kufanyiwa marekebisho kwenye
viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha ni kama ifuatavyo:-
i.
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango
cha asilimia 10 badala ya asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye ngano
inayotambuliwa katika HS Code 1001.99.00 na HS Code 1001.99.90. Hatua hii
itahusu viwanda vinavyotumia bidhaa hii
katika uzalishaji (duty remission). Aidha, imezingatia kwamba uzalishaji wa
bidhaa hii katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni mdogo na
hivyo hautoshelezi mahitaji. Pia inatoa unafuu kwa viwanda na wazalishaji wa
bidhaa na vyakula vinavyotumia ngano na kuimarisha utulivu wa bei wa bidhaa
zinazozalishwa kwa kutumia ngano hiyo;
ii.
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 0 badala
ya asilimia 10 kwenye malighafi inayotumika katika kutengeneza sabuni (LABSA)
inayotambuliwa katika HS Code 3402.11.00; HS Code 3402.12.00 na HS Code
3402.19.00 kwa kipindi cha mwaka mmoja. Hatua hii itahusu viwanda
vinavyotumia malighafi hii katika
uzalishaji (duty remission). Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu wa gharama za
uzalishaji kwa viwanda vidogo na vya kati vya kutengeneza sabuni na hivyo
kuweza kuongeza uzalishaji na ajira;
iii.
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango
cha asilimia 10 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye viunganishi vya
pikipiki. Hatua hii itahusu viwanda vinavyotumia viunganishi hivyo katika kuunganisha pikipiki
(duty remission for Motorcycle Assemblers). Lengo la hatua hii ni kuendelea
kuhamasisha uunganishaji wa pikipiki
katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wakati wataalam wanaanda orodha ya
viunganishi ambavyo vitastahili kupata msamaha wa Ushuru wa Forodha na ambavyo
havitastahili. Baada ya kuainisha orodha ya viunganishi visivyostahili kupata
msamaha wa Ushuru wa Forodha, waunganishaji watahamasishwa kuvitengeneza ndani
ya Nchi Wanachama wa Jumuiya;
iv.
Kuendelea kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwenye
mafuta ghafi ya kula (crude palm oil) yanayotambulika katika Hs Code 1511.10.00
kwa mwaka mmoja. Hatua hii inalenga katika
kuhamasisha kilimo cha mbegu za mafuta hapa nchini na kukuza viwanda vya
kutengeneza mafuta ya kula. Aidha, inazingatia mkakati maalum wa kuendeleza na
kulinda viwanda vya kuzalisha mafuta ya kula yanayotokana na mbegu
zinazozalishwa hapa nchini na kutumia fursa ya soko kubwa katika Jumuiya ya
Afrika Mashariki. Tanzania ina nafasi kubwa ya kuweza kuongeza uzalishaji wa
mbegu za mafuta;
v.
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au
kiwango maalum cha dola za kimarekani 250 kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwa
kila tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa za chuma (Flat rolled Iron
or non alloy Steel) kwa mwaka mmoja zinazotambuliwa katika HS Codes: 7210.41.00; 7210.49.00; 7210.61.00; 7210.69.00;
7210.70.00; 7210.90.00; 7212.30.00; 7212.40.00; 7212.50.00; na 7212.60.00.
Hatua hii inalinda uzalishaji wa bidhaa za chuma zinazozalishwa na viwanda vya
ndani dhidi ya ushindani wa bidhaa za aina hiyo zinazoingizwa kutoka nje ya
nchi;
vi.
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia
25 au dola za kimarekani 200 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kutegemea
kiwango kipi ni kikubwa kwenye bidhaa za chuma (Steel Rods and Bars and Hot
rolled Angles, Sections) zinazotambuliwa katika HS Codes 7213.10.00;
7213.20.00; 7214.10.00; 7214.20.00; 7214.30.00; 7214.91.00; 7214.99.00;
7216.10.00; 7216.21.00; 7216.22.00; na 7216.50.00. Hatua hii inatekelezwa ili
kulinda uzalishaji wa bidhaa hizo za chuma kutokana na ushindani unaosababishwa
na uingizaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi. Aidha, hatua hii inahamasisha
uwekezaji na kuongeza ajira;
vii.
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 0 badala ya
asilimia 25 au dola za kimarekani 200 kwa tani ya chuma (HS Code
7228.20.00) kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwa wazalishaji wa springi za
magari (leaf spring). Hatua hii itahusu viwanda vinavyotumia bidhaa hii katika uzalishaji (duty
remission). Kiwango cha asilimia 25 au dola za kimarekani 200 kiliwekwa mwaka
2016/17 kulinda wazalishaji wa bidhaa za vyuma hapa nchini wakati
wazalishaji wa springi za magari
walikuwa wanahitaji kutumia bidhaa hizo kama malighafi;
viii.
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 au dola
za kimarekani 125 kwa tani moja ya ujazo kutegemea kiwango kipi ni kikubwa
kwenye bidhaa za chuma (Flat-rolled products of iron or non alloy steel of a
width of 600mm or more, cold rolled or cold reduced) kwa mwaka mmoja
zinazotambuliwa chini ya HS Codes 7209.15.00; 7209.16.00; 7209.17.00;
7209.18.00; 7209.25.00; 7209.26.00; 7209.27.00; 7209.28.00 na 7209.90.00. Lengo
la hatua hii ni kulinda viwanda vyetu kutokana na ushindani wa bidhaa
zinazoingizwa kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki;
ix.
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia
0 kwenye malighafi za kutengeneza chujio
za hewa za magari (air filters). Hatua
hii itahusu viwanda vyote vinavyotumia
bidhaa hii katika uzalishaji wa chujio hizo (duty remission) katika Nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha
uzalishaji wa bidhaa hiyo na kukuza ajira;
x.
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala
ya asilimia 0 kwenye Gypsum Powder
inayotambuliwa chini ya HS Code 2520.20.00 kwa mwaka mmoja. Lengo la hatua hii
ni kulinda viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo hapa nchini na kuhamasisha
wawekezaji watumie gypsum
inayopatikana hapa nchini katika kuzalisha gypsum
powder na kwa kufanya hivyo tutaongeza ajira na mapato;
xi.
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango
cha asilimia 10 badala ya kuongeza kiwango hicho hatua kwa hatua hadi kufikia
asilimia 25 mwaka 2018/19 kwenye sukari inayotumika viwandani. Hatua hii
itahusu viwanda vyote vinavyotumia sukari hiyo katika uzalishaji wa bidhaa
mbalimbali (duty remission). Hatua ya kutoongeza Ushuru wa Forodha imezingatia
kuwa sukari inayotumika viwandani ni malighafi ya maana katika kuzalisha
chakula, vinywaji na madawa ambavyo ni muhimu kwa mahitaji ya binadamu;
xii.
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 0 badala
ya asilimia 10 kwenye mashine za kielektroniki za kukusanya mapato ya hazina
(Electronic Fiscal Devices) zinazotambuliwa chini ya HS Code 8470.50.90 kwa
mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha wafanyabiashara na walipa kodi
kutumia mashine hizo katika kufanya mauzo na kuongeza ufanisi katika usimamizi
na udhibiti wa kodi;
xiii.
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia
25 badala ya asilimia 10 kwenye bidhaa za karatasi zinazotambulika chini
ya HS Codes 4804.11.00; 4804.19.90;
4804.21.00; 4804.29.00; 4804.31.00; 4804.29.00; 4804.41.00; 4804.51.00;
4804.59.00; 4805.11.00; 4805.12.00; 4805.19.00; 4805.24.00; 4905.25.00;
4805.30.00; 4805.91.00 na 4805.92.00. Hatua hii imeendelea kutekelezwa ili
kuvilinda viwanda vya ndani vinavyozalisha karatasi hizo kutokana na ushindani
wa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi;
xiv.
Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha
asilimia 0 badala ya asilimia 25 kwenye malighafi na vifaa vinavyoagizwa nje ya
nchi kwa ajili ya kuunganisha na kutengeneza vifaa (inputs for assembling of
equipments) ambavyo ni mahsusi kwa ajili ya matumizi ya walemavu. Aidha, hatua
hii itahusu waunganishaji wa vifaa hivyo tu (duty remission). Hivyo
waunganishaji (assemblers) wa vifaa hivyo watanufaika na punguzo la ushuru huo.
Aidha, lengo la kuchukua hatua hii ni kuhamasisha uwekezaji katika kuzalisha
vifaa hivyo muhimu ndani ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kukuza
ajira;
xv.
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala
ya asilimia 0 kwenye muundo wa aluminiamu (aluminium structure) inayotambuliwa
kwenye HS Code 7610.90.00 kwa mwaka mmoja. Hatua ya kuweka kiwango hiki cha
Ushuru inalenga katika kutofautisha vifaa vyenye kufanana lakini vina ubora
tofauti (steel and aluminium) hali ambayo inasababisha ukwepaji kodi;
xvi.
Kufanya marekebisho katika uandishi wa HS Code
4911.99.20 ili kujumuisha karatasi zinazotumika kwenye Shule katika kujibu
maswali (examination answer sheet) ili nazo ziweze kutozwa Ushuru wa Forodha wa
asilimia 0 kama vile karatasi za maswali (question papers) zinavyotozwa. Hatua
hii itapunguza gharama za kutoa elimu nchini; na
xvii.
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 0 kwenye
vifaa vinavyotumika katika ujenzi na uunganishaji wa meli (inputs for use in
the manufacture/assembling of ships). Hatua hii itawahusu wajenzi na
waunganishaji wa meli (duty remission). Lengo ni kutoa unafuu wa gharama katika
kutengeneza meli au kuunganisha. Aidha hatua hii itahamasisha uvuvi, kuimarisha
usafiri wa majini na kuongeza ajira.
74.
Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa Nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya pia marekebisho kwenye
Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC- Customs Management Act,
2004) kama ifuatavyo:-
i.
Kufanya marekebisho katika kifungu B cha Jedwali la Tano la Sheria ya
Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kufuta aya ya 25 ili kuondoa msamaha
wa Ushuru wa Forodha kwenye taa zinazojulikana kama Compact Fluorescent Bulbs
(CFL) na Light Emitting Bulbs (LEI). Hatua hii imezingatia kwamba msamaha huo
hauna tija hivi sasa kwa kuwa bidhaa hizo ni zile ambazo zimetengenezwa kwa
kiwango kilicho kamilika kwa matumizi (finished goods) na hivyo zinastahili
kutozwa Ushuru wa Forodha wa asilimia 25;
ii.
Kufanya marekebisho katika sehemu ya
203 ya Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki na kuongeza adhabu (fine) kutoka dola za kimarekani 10,000
hadi dola za kimarekani 20,000 au asilimia 50 ya kodi iliyostahili kulipwa
kutegemea kiwango kipi ni kikubwa. Lengo ni kuweka adhabu kali kwa makosa
(offences) yanayofanywa na waagizaji mizigo kama vile kuwasilisha nyaraka
zisizo sahihi, taarifa zisizo sahihi, kukwepa kodi kwa njia ya kughushi, na
kadhalika. Hatua hii imezingatia adhabu ya juu inayotozwa hivi sasa ni dola za
kimarekani 10,000 ambazo ni ndogo na haziwezi kupunguza makosa ya namna hiyo;
iii.
Kufanya marekebisho katika kifungu cha 218 cha Sheria ya Forodha ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki ili kumpa mamlaka Kamishna wa Forodha kumrejeshea mlipa
kodi bidhaa ambazo zilikuwa zimezuiliwa badala ya utaratibu wa sasa unaotoa
mamlaka hayo kwa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; na
iv.
Kufanya marekebisho katika aya ya 30 ya Jedwali la Tano la Sheria ya
Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuongeza “usambazaji wa mafuta na
gesi” katika misamaha inayotolewa kwenye miradi ya gesi na mafuta. Hatua hii
ina lengo la kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye miradi ya mabomba ya
mafuta inayotekelezwa na Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hatua hizi za Ushuru wa Forodha
kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 16,053.9.
g)
Marekebisho madogo madogo
katika baadhi ya Sheria za Kodi na Sheria
nyingine mbalimbali
75.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho
mengine madogo madogo yasiyo ya kisera katika sheria mbalimbali za kodi pamoja
na sheria nyingine mbalimbali ili ziwe sanjari na azma ya kurahisisha
utekelezaji wake. Marekebisho hayo yataainishwa katika Muswada wa Sheria ya
Fedha ya mwaka 2017 na Matangazo ya Serikali (Government Notices).
h)
Marekebisho ya Ada na Tozo mbalimbali
zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea
76.
Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya viwango vya ada na tozo mbalimbali
zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea ili kuvihuisha kulingana
na hali halisi ya ukuaji wa uchumi. Aidha, marekebisho hayo yataainishwa katika
Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2017 na Matangazo ya Serikali (Government
Notices). Marekebisho hayo yatajumuisha:-
i.
Kufuta ada ya ukaguzi wa viwango, ada ya
ukaguzi wa mionzi na ada ya wakala wa vipimo kwenye mbolea inayotozwa na
Shirika la Viwango Tanzania, Tume ya Mionzi Tanzania na Wakala wa Vipimo
Tanzania. Lengo la hatua hii ni kuwapunguzia wakulima gharama za pembejeo na
hivyo kuongeza tija katika uzalishaji;
ii.
Kufuta ada ya ukaguzi wa viwango kwa
mazao ya biashara kama pamba, chai, korosho na kahawa inayotozwa na Shirika la
Viwango Tanzania. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za uzalishaji kwa
viwanda vinavyosindika mazao haya na pia kuongeza mapato kwa wakulima;
iii.
Kufuta Ushuru wa Huduma (Service Levy)
kwenye nyumba za kulala wageni ambazo zinatozwa Guest House Levy;
iv.
Kufuta Ushuru wa Mabango kwa mabango
yanayoelekeza mahali huduma za jamii (Shule na Hospitali au Zahanati)
zinapopatikana. Aidha, kuanzia tarehe 1 Julai, 2017 Mamlaka ya Mapato Tanzania
itaanza kukusanya Ushuru wa Mabango ya Matangazo kwa nchi nzima;
v.
Kufuta ada ya vibali vinavyotolewa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa mfano vibali vya machinjio (isipokuwa ada ya
machinjio na ada ya ukaguzi wa nyama), ada ya vibali vya kusafirisha mifugo na
ada ya vibali vya kuanzisha maduka ya dawa;
vi.
Kufuta ada ya makanyagio minadani; na
vii.
Kufanya marekebisho ya kiwango cha
faini kwa makosa ya watakaoenda kinyume na masharti ya Sheria ya Fedha za
Serikali za Mitaa kutoka kiasi kisichozidi shilingi 50,000 na kifungo
kisichozidi miezi 12 hadi kiasi kisichopungua shilingi 200,000 na kisichozidi
shilingi 1,000,000 au kifungo kisichopungua miezi 12 na kisichozidi miaka miwili.
77.
Mheshimiwa Spika, Serikali
itaendelea kufanya uchambuzi na tathmini ya tozo na ada zinazotozwa na
mashirika, taasisi na wakala mbalimbali ili kuendelea kuweka mazingira bora ya
kufanya biashara/kuwekeza na kuondoa kero kwa wananchi. Hii itajumuisha kupitia
upya na kuvisawazisha viwango vya tozo na ada hizo na pia kuondoa tozo na ada
za usumbufu.
i)
Tarehe ya Kuanza
Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi
78.
Mheshimiwa
Spika, hatua hizi za kodi zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1
Julai, 2017, isipokuwa pale ilipoelezwa vinginevyo.
V.
SURA YA BAJETI KWA MWAKA 2017/18
79.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia shabaha na sera za bajeti kwa
mwaka 2017/18, Sura ya Bajeti inaonesha kuwa jumla ya shilingi bilioni 31,712.0 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika
kipindi hicho. Jumla ya mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya Halmashauri
yanatarajiwa kuwa shilingi bilioni 19,977.0, sawa na asilimia 63.0 ya bajeti yote.
Kati ya mapato hayo, Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya
shilingi bilioni 17,106.3 sawa na asilimia 85.6 ya mapato ya ndani. Aidha,
mapato yasiyo ya kodi ni shilingi bilioni 2,183.4 na mapato kutoka vyanzo vya
Halmashauri ni shilingi bilioni 687.3.
80.
Mheshimiwa Spika, Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia
shilingi bilioni 3,971.1 ambayo ni asilimia 12.5 ya bajeti yote. Misaada na
mikopo hii inajumuisha miradi ya maendeleo shilingi bilioni 2,473.8; mifuko ya
pamoja ya kisekta shilingi bilioni 556.1; na misaada ya kibajeti (GBS) shilingi
bilioni 941.2.
81.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatarajia kukopa shilingi bilioni
7,763.9 kutoka soko la ndani na nje kwa masharti ya kibiashara. Mikopo ya ndani
inatarajiwa kuwa shilingi bilioni 6,168.9, ambapo shilingi bilioni 4,948.2 ni
kwa ajili ya kulipia dhamana za Serikali zinazoiva (rollover) na shilingi
bilioni 1,220.7 sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa ni mikopo mipya kwa
ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Ili kuongeza kasi katika ujenzi wa
miundombinu, Serikali inatarajia kukopa shilingi bilioni 1,595.0 kutoka soko la
nje.
82.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Serikali itaongeza
jitihada za ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na mikopo ya ndani na nje ili
kutekeleza miradi ya maendeleo. Miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo awamu
zinazofuata za ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge, na uboreshaji wa bandari mbalimbali nchini,
vitatekelezwa kulingana na mpangokazi kutegemea mwenendo wa mapato ya ndani na
nje utakaojidhihirisha baada ya kufanya
mapitio ya utekelezaji wa bajeti kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2017.
Aidha, mara baada ya ridhaa ya Serikali kupatikana, utaratibu wa kutoa
hatifungani maalum (special non-cash bond) utatekelezwa ili kusaidia kupunguza
madeni yaliyohakikiwa ya Serikali kwa mifuko ya hifadhi ya jamii.
83.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Serikali inapanga
kutumia jumla ya shilingi bilioni 31,712.0. Kati ya fedha hizo,
shilingi bilioni 19,712.4 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida,
ikijumuisha shilingi bilioni 7,205.8 za mishahara na shilingi bilioni 9,461.4
kwa ajili ya kulipia deni la umma na huduma nyinginezo. Aidha, matumizi ya
maendeleo yatakuwa shilingi bilioni 11,999.6 sawa na asilimia 38 ya bajeti
yote, ambapo shilingi bilioni 8,969.7 ni fedha za ndani na shilingi bilioni
3,029.8 ni fedha za nje. Kiwango hiki kimezingatia wigo wa asilimia 30 hadi
asilimia 40 ya bajeti yote iliyoidhinishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa
wa Miaka Mitano, 2016/17 – 2020/21.
84.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mfumo wa bajeti kama nilivyoeleza, sura ya bajeti kwa
mwaka 2017/18 ni kama inavyooneshwa katika Jedwali
A.
Jedwali
A: Mfumo wa Bajeti ya Mwaka 2017/18
|
||
|
|
Shilingi Milioni
|
|
Mapato
|
2017/18
|
A.
|
Mapato ya Ndani-Serikali
Kuu
|
19,289,695
|
|
(i) Mapato ya Kodi (TRA)
|
17,106,336
|
|
(ii) Mapato yasiyo ya
kodi
|
2,183,359
|
B.
|
Mapato ya Halmashauri
|
687,306
|
C.
|
Mapato na Mikopo nafuu
kutoka nje
|
3,971,103
|
|
(i) Misaada na Mikopo nafuu -GBS
|
941,258
|
|
(ii)Misaada na Mikopo
nafuu ya Miradi
|
2,473,770
|
|
(iii)Misaada na Mikopo
nafuu ya Kisekta
|
556,075
|
D.
|
Mikopo ya Ndani na Nje
yenye Masharti ya Kibiashara
|
7,763,882
|
|
(i) Mikopo ya Nje
|
1,594,985
|
|
(ii) Mikopo ya Ndani
|
1,220,668
|
|
(iii)Mikopo ya Ndani-
Rollover
|
4,948,229
|
|
JUMLA YA MAPATO YOTE
(A+B+C+D)
|
31,711,986
|
|
|
|
|
Matumizi
|
|
E.
|
Matumizi ya Kawaida
|
19,712,394
|
|
|
|
|
o/w (i) Deni la Taifa
|
9,461,433
|
|
-Malipo ya Riba Ndani
|
1,025,546
|
|
-Malipo ya Mtaji Ndani
(Rollover)
|
4,948,229
|
|
-Malipo ya Mtaji Nje
|
1,182,651
|
|
- Malipo ya Riba Nje
|
673,492
|
|
- Michango ya Serikali kwenye
Mifuko ya Hifadhi za Jamii
|
1,195,882
|
|
-Matumizi Mengine ya Mfuko Mkuu
|
435,633
|
|
(ii) Mishahara
|
7,205,768
|
|
(iii)Matumizi Mengineyo (OC)
|
3,045,193
|
|
- Matumizi yanayolindwa (protected expenditure)
|
1,985,245
|
|
- Matumizi ya Halmashauri
|
274,922
|
|
- Matumizi Mengine ya kuendesha ofisi
|
785,025
|
|
|
|
F.
|
Matumizi ya Maendeleo
|
11,999,592
|
|
(i) Fedha za Ndani
|
8,969,747
|
|
o/w Matumizi ya Halmashauri
|
412,384
|
|
(ii)Fedha za Nje
|
3,029,845
|
|
JUMLA YA MATUMIZI YOTE
(E+F)
|
31,711,986
|
|
NAKISI YA BAJETI
(ASILIMIA YA PATO LA TAIFA)
|
3.8%
|
Chanzo: Wizara ya Fedha
na Mipango
VI.
HITIMISHO
85.
Mheshimiwa Spika, hatua zilizopendekezwa kwenye bajeti hii
zinalenga kujenga msingi madhubuti wa uchumi wa viwanda na kupanua fursa za
ajira na biashara. Dhamira yetu sote ni kufikia kiwango cha uchumi wa kipato
cha kati ifikapo 2025. Ili kushiriki katika mafanikio hayo, ni lazima kila mmoja
wetu ashiriki katika shughuli halali ya uzalishaji na afanye hivyo kwa juhudi
na maarifa ili kuleta tija.
86.
Mheshimiwa Spika, kufanikiwa kwa Bajeti hii kunahitaji nidhamu
ya hali ya juu katika usimamizi wa mapato na matumizi. Ili kufikia azma hii, juhudi
za pamoja kati ya Serikali na wadau wote zinahitajika ikiwa ni pamoja na
kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi kwa kuwekeza zaidi katika
maeneo ya kipaumbele. Natoa rai kwa kila Mtanzania kutimiza wajibu wake ili
Bajeti hii iweze kutekelezwa kama ilivyopangwa.
87.
Mheshimiwa Spika, mojawapo ya masharti ambayo nchi yetu haina
budi kuyatimiza ili Tanzania ifanikiwe kufanya mapinduzi ya kiuchumi na kijamii
kwa haraka, ni pamoja na kuwa na viongozi wenye sifa za kuleta na kusimamia
mabadiliko. Sifa za viongozi wa aina hiyo ni zifuatazo:
i.
Wanafanya jitihada kuwa binadamu wema, wanaojali
na kusaidia watu wengine hasa wanyonge, wenye maadili mema, waaminifu na
kutenga muda wao kutafakari juu ya utumishi wao kwa umma;
ii.
Wanakuwa na dira kuhusu wapi pa kuipeleka nchi
kutoka ilipo sasa na kujiwekea malengo makubwa;
iii.
Wanaweka viashiria vya mafanikio kwa kila programu
na mradi utakaotekelezwa;
iv.
Wanasimamia kidete muda wa utekelezaji;
v.
Wanatoa maamuzi magumu na maelekezo thabiti kwa
kutambua kuwa hakuna mchezo usio na maumivu sambamba na kuandaa na kuwawezesha
viongozi watakaopokea kijiti; na
vi.
Wanateua kwa umakini na kufanya kazi pamoja na
timu hiyo madhubuti ya ushindi.
88.
Mheshimiwa Spika, mimi naamini, na Bunge lako Tukufu na
Watanzania walio wengi watakubaliana nami kuwa, Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anazo sifa zote hizi.
Ni kiongozi mzalendo, anayependa na kujivunia nchi yake ya Tanzania; ni
kiongozi ambaye amejielekeza kuijenga Tanzania mpya; ana moyo thabiti, nia
njema na kujifunga kuwatumikia Watanzania wote na hasa wanyonge; ana msimamo
thabiti usioyumba; anayo dhamira ya dhati ya kusimamia utendaji uliotukuka;
anachukia rushwa, ubadhirifu, ufisadi na wizi wa rasilimali za umma; ana
uthubutu wa kufanya mambo mapya tofauti, yenye maslahi kwa Taifa kinyume na
mazoea, hata kama hayawapendezi baadhi ya watu.
89.
Mheshimiwa Spika, sasa Watanzania wote tumeanza kuona matokeo.
Ndani ya kipindi kifupi cha miezi 18 ya uongozi wake, Mheshimiwa Rais amefanya
mambo mengi makubwa sana! Mengi yamefufua matumaini na ari ya wananchi walio
wengi lakini kwa wachache yamekuwa machungu. Naomba niyarejee baadhi kama
ifuatavyo: Kutengua uteuzi wa viongozi
mbalimbali ambao aliona hawaendi na dhamira na kasi yake; Kukamata makontena
yaliyoondolewa bandarini bila kulipa kodi stahiki; Kuondoa Serikalini watumishi
wasio na sifa/vyeti halali na wanafunzi hewa; Kuimarisha matumizi ya fedha za
umma; Kudhibiti mishahara na madai hewa; Kuerejesha nidhamu kwa Wizara, Idara
na taasisi za Serikali kulipa madeni ya umeme, maji na huduma nyingine;
Kugharamia elimu msingi bila malipo; Kuongeza ukusanyaji wa kodi kutoka wastani
wa shilingi bilioni 800 kwa mwezi hadi wastani wa shilingi trilioni 1.2;
kuthubutu kutekeleza uamuzi wa muda mrefu wa kuhamishia makao makuu ya Serikali
Dodoma; Kumtaka kila Mtanzania afanye kazi; Kuanza utekelezaji wa kujenga Standard Gauge Railway (SGR); Kununua
ndege mbili mpya na kufanya malipo ya awali kwa ndege nyingine nne ili kufufua
shirika la ndege na kuinua utalii; Kushawishi Serikali ya Uganda kuridhia mradi
mkubwa wa bomba la mafuta lijengwe kutoka Hoima - Uganda hadi bandari ya Tanga
katika mazingira ya ushindani mkali; Kuendelea na ujenzi na ukarabati wa
barabara mbalimbali nchini ikiwemo flyover
pale TAZARA, interchange Ubungo; na
ujenzi wa miradi ya miundombinu ya umeme, maji, na meli mpya mbili katika Ziwa Nyasa. Aidha, katika uongozi wake agenda
ya kujenga uchumi wa viwanda imepata mwitikio mkubwa wa sekta binafsi nchini na
hususan ukanda wa Pwani.
90.
Mheshimiwa Spika, ninafurahi kuwaambia Watanzania wenzangu kuwa
hatua hizo ni uwekezaji wa lazima na wa busara (sensible investment). Bajeti
hii ya 2017/18 itaendelea kuimarisha matokeo haya na kuchukua hatua zaidi ili
tuende mbele. Ukiona vinaelea, ujue vimeundwa! Rai yangu kwa Watanzania
wenzangu, na hasa sisi viongozi na wananchi wote ni lazima tujitoe kuijenga
Tanzania, tumuunge mkono Rais wetu kwa vitendo kwa kila mtu kufanya kazi kweli
kweli tukijielekeza kutekeleza Dira na malengo ya Serikali ya awamu ya tano ya
kujenga ustawi wa uchumi imara unaotengeneza ajira, fursa mpya na mgawanyo wa
haki na usawa wa rasilimali za Tanzania kwa wananchi wote. Tulinde umoja na
amani yetu kama mboni ya jicho na tena, letu liwe moja katika masuala yote
yenye maslahi kwa taifa letu. Naomba nichukue nafasi hii kwa niaba ya Serikali
kuwashukuru na kuwapongeza kwa dhati kabisa wananchi wote ambao wanalipa kodi
stahiki ambao ndiyo wamefanikisha maendeleo hayo niliyoyataja. Serikali
inawaahidi kutumia vizuri mapato yatokanayo na kodi zenu kuwaletea maendeleo.
Wale mnaojaribu kukwepa kodi, mkono wa sheria utachukua mkondo wake.
91.
Mheshimiwa Spika, ninapokaribia kumaliza hotuba hii, naomba
kuwatambua na kuwashukuru Washirika wetu wa Maendeleo wanaotarajia kuchangia
Bajeti ya Serikali jumla ya shilingi bilioni 3,971.1 kwa mwaka 2017/18 kama
ifuatavyo, (kiasi walichoahidi kuchangia
katika bajeti ya 2017/18 kikiwa katika mabano):Benki ya Maendeleo ya
Afrika (shilingi bilioni 410.9); Abu Dhabi/OPEC (shilingi bilioni 20);
AFD/French (Shilingi bilioni 27.3); Badea (shilingi bilioni 10); Ubelgiji
(shilingi bilioni 13.7); Denmark (shilingi bilioni 47); DFID (Shilingi bilioni
364.4); Jumuiya ya Ulaya (shilingi bilioni 150.3); Finland (shilingi bilioni
25.7); Ujerumani (shilingi bilioni 58.4); Global Fund (shilingi bilioni 431.2);
IFAD (shilingi bilioni 45.3); India (shilingi bilioni 80); Ireland (shilingi
bilioni 18.3); JICA/Japan (shilingi bilioni 57.4); Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait
(shilingi bilioni 20); Norway (shilingi bilioni 22.3); OPEC Fund (shilingi
bilioni 8.5); Poland (shilingi bilioni 61.1); Sweden (shilingi bilioni 172.5);
Korea ya Kusini (shilingi bilioni 20); Uswisi (shilingi bilioni 12.1); UNICEF
(shilingi bilioni 27.2); USAID (shilingi bilioni 3.4); na Benki ya Dunia
(shilingi bilioni 1,862.3). Fedha zilizoingizwa kwenye Bajeti hii zinazingatia
historia ya utoaji wa fedha za kugharamia miradi kutoka kwa Washirika wetu wa
Maendeleo.
92.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kutambua uhusiano mzuri tulionao
na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) chini ya Mpango wa Ushauri wa Kisera
(Policy Support Instrument - PSI). Ni matumaini yetu kuwa Bodi ya Shirika la
Fedha Duniani itakubali kuendeleza awamu nyingine ya mpango wa PSI baada ya
mwezi Desemba 2017. Rai yangu kwa marafiki wote wa nchi yetu ni kuwa: Endeleeni
kuiunga mkono Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli hususan
katika azma yake ya kujenga uchumi wa viwanda. Watanzania wamesikia kiasi cha
fedha mlizoahidi na nawaomba mtimize ahadi zenu kwa wakati nasi tunawaahidi
kutumia michango yenu adhimu kwa ufanisi na uwazi.
93.
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, naomba nihitimishe kwa
kumshukuru kwa namna ya pekee kabisa, mke wangu na rafiki yangu mpenzi, mama
Mbonimpaye Mpango pamoja na watoto na wajukuu wetu wote kwa kunitunza na kuniombea
kwa Mungu kila siku ili niweze kutekeleza vema dhamana niliyopewa ya
kuwatumikia Watanzania. Aidha, kwa heshima kubwa, ninawashukuru sana ndugu
zangu, wana wa Wilaya ya Buhigwe na wananchi wa mkoa wa Kigoma kwa ujumla kwa
upendo na kunitakia heri ili niendelee kutekeleza wajibu wangu ipasavyo.
Mlinilea na kunifundisha kupenda kufanya kazi. Nami nawaahidi kuwa nitakuwa
mwaminifu, sitawaangusha! Asanteni sana Waheshimiwa Wabunge, viongozi na
wananchi wote kwa kunisikiliza.
MUNGU
IBARIKI TANZANIA!
0 comments:
Chapisha Maoni