Kutokana
na mambo mbalimbali ambayo yanaendelea nchini ikiwepo mikataba mibovu
ya madini viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa wamekuwa wakisema njia
pekee ya kuweza kusaidia nchi kulinda maliasili zake ni kuwa na Katiba
mpya.
Jambo
hili limewaibua Wenezi wawili wa vyama vya siasa akiwepo Katibu wa NEC,
Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole kutoka Chama Cha Mapinduzi na
Katibu mwenezi wa ACT Wazalendo Taifa, Bwana Ado Shaibu ambao
walinyukana kwa hoja juu ya Katiba mpya huku Humphery Pole Pole yeye
akisema kuwa waliofanya katiba ikwame ni viongozi wa upinzani pamoja na
viongozi wa CCM ambao waliweka maslahi binafsi mbele kuliko maslahi ya
wananchi.
Humphery
Pole pole alidai kuwa wao kama Chama Cha Mapinduzi saizi wanajisafisha
ili wawe wasafi ndiyo baadaye waje kuzungumzia suala la Katiba Mpya
wakiwa ni wasafi na kusema anaamini pia vyama vya upinzani ndiyo
vitachelewesha tena kwani wao mikono yao ni michafu lakini haoni dalili
za wapinzani hao kujisafisha.
"Katiba
hatukufanikiwa kwa sababu wengi wa sisi viongozi tena kutoka upinzani
na Chama Cha Mapinduzi tuliweka maslahi yetu mbele tukaweka mbali
maslahi ya wananchi kwa sababu za ubinafsi lakini serikali ya CCM saizi
tunarekebisha hayo. Mimi nilitegemea na vyama vingine vikianza kuosha
mikono yao michafu mno halafu ndiyo tuzungumze katiba, ukizungumza
katiba na una mikono michafu haina tofauti na chakula kipo mezani una
mikono michafu na bado unataka kula haiwezekani" alisema Pole Pole
Kwa
upande wa pili Katibu mwenezi wa ACT Wazalendo Taifa, Bwana Ado Shaibu
alipingana na hoja ya Pole pole na kusema kuwa analeta hoja nyepesi
kwenye jambo la msingi na kusema kuwa katiba ya nchi ni mali ya wananchi
na si mali ya chama fulani cha siasa, hivyo kusema CCM saizi
inajisafisha ikimaliza kujisafisha ndiyo izungumzie katiba si sawa.
"Ndugu
Pole Pole anasema mchakato wa katiba ni sharti tusubiri CCM inawe
mikono, kanuni ya wapi hii? Taratibu za wapi hizi za kidunia za
kutengeneza katiba zinazosema tunasubiri chama tawala kijisafishe,
kinawe mikono kiwe safi ndipo turejee mchakato wetu, taratibu za wapi
hizo zinazosema mpaka vyama vya siasa vinawe mikono ndipo virejee
mchakato wa katiba. Katiba ni mali ya wananchi na wanasiasa wakizungumza
wanazungumza kama sehemu katika jamii, wanasiasa watasema lakini
haiondoi ukweli kwamba katiba ni zao la wananchi, kwa hiyo kusema mpaka
CCM iwe safi ni kurejea katika propaganda" alisema Ado Shaibu
Mbali
na hilo Ado Shaibu alimtaka Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi kutoka CCM
ndugu, Humphery Pole Pole kuwa wazi kwamba kwa CCM ya sasa katiba siyo
kipaumbele chao hivyo wananchi wajue kuliko kufanya propaganda ili hali
anatambua wazi kuwa hata Rais John Pombe Magufuli katiba si ajenda yake
kwa sasa.
"Rais
Magufuli yeye alishaweka wazi kuwa katiba siyo ajenda yake, sasa kuna
dhambi gani wapishi wa propaganda wa CCM kusema kwamba hatutaki katiba
siyo vipaumbele vyetu, wanyooshe tu maelezo na si kupindisha pindisha
ili watu wajue namna ya kupigania katiba yao" alisisitiza Ado Shaibu
Humphery
Pole Pole alikuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa
na Jaji Joseph Warioba ambayo iliwasilisha kwenye Bunge rasmi la Katiba.
0 comments:
Chapisha Maoni