ARUSHA: TAARIFA rasmi kutoka chumba cha Mganga Mkuuwa Hospitali ya Rufaa ya Mt. Meru, Arusha, zimeeleza kuwa hali ya watoto watatu ambao ni wanafunzi wa Lucky Vincent Nursery & Primary School walionusurika kwenye ajali ya Jumamosi iliyopita Karatu, wanaendelea vizuri mpaka sasa.
Akizungumza na Global TV Online, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Arusha, Jackline Urio amesema;
“Watoto watatu tuliowapokea, wawili wa kike na mmoja wa kiume wanaendelea vizuri, wanajifahamu, wanaweza kutambua watu na kujieleza vizuri.”
“Siku ya tukio kuna kikundi cha mishezni walijitokeza na kuomba kuwahudumia watoto hawa pamoja na madaktari wa Taasisi ya Mifupa ya Mumbili (MOI) kufanikisha kuokoa uhai wa watoto hawa, ambao tumesaidizana nao mpaka sasa ambapo tunatarajia muda wowote watoto hawa wanaweza kusafirishwa na kwenda Marekani kwa matibabu zaidi.”
“Tunapenda kuwahakikishia wananchi wa Tanzania kuwa, watoto wako hai na wanaendelea vizuri, wasisikilize maneno ya mitandaoni, waamini kile kinachosemwa na madaktari.”
Naye Kaimu Mganga Mkuu Hospitali ya Rufaa Mt. Meru, Arusha, Dkt. Wonangi Timothy amesema.
“Tayari tumeshaandaa madaktari, wataalam wa saikolojia 17 kutoka wilaya tofauti hapa Arusha na wataalam watatu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, wengine watatu kutoka KKKT kwa ajili ya kusaidia zoezi hili pamoja na kutoa elimu ya saikolojia kwa waathirika wa tukio hili.”
“Tumeshaandaa mpango mkakati wa kuwasaidia hao waathirika, kutoa ushauri shuleni kwa wanafunzi na walimu pamoja na kuzifikia familia za watoto hao sambamba na wakazi wanaoishi karibu na maeneo ya shule hiyo.”
“Bajeti yetu, zitahitajika Tsh. milioni 10.4 kwa ajili ya shughuli nzima vikiwemo vifaa vya kazi, vipeperushi, gharama za maradhi, chakula na mambo mengine yatakayoendana ili kufanikisha zoezi hilo ambalo litafanyika kwa muda wa siku tano na baada ya miezi miwili tutarudi kufanya analysis ya ya mafanikio ya hicho tulichokifanya,” alisema Dkt. Wonangi.
=============================