Na Nuru Juma-MAELEZO
Serikali
inamkakati wa kuhakikisha inajenga Magereza katika maeneo yenye
uzalishaji mkubwa wa kilimo ambayo pia yana ukubwa wa kutosha ili kazi
ya kuwarekebisha wafungwa iwe rahisi kufanyika huku shughuli za
uzalishaji zikiwa zinaendelea.
Hayo
yamesemwa leo Bungeni Mjini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi
Mhe. Mwigulu Nchemba alipokuwa akijibu swali la Mhe Devotha Minja Mbunge
wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro.
“Magereza
hayo yatajengwa katika maeneo yenye Kilimo na yatakuwa ni kwa ajili ya
watu waliokwisha hukumiwa huku yale Magereza ya mijini yawe kwa ajili ya
mahabusu tu ili wawe karibu na Mahakama,”alisema Mwigulu.
Aliongeza
kuwa mkakati huo wa Serikali ni wa muda mrefu na wanahitaji kufanya
hivyo ili kurahisisha shughuli za maendeleo zinazofanywa na wafungwa na
pia kupunguza msongamano wa wafungwa katika Magereza.
Hili
pia linatokana na tamko la Mh.Rais Dkt John Pombe Magufuli alilowahi
kulitoa hivi karibuni kuwa wafungwa wako katika kutumikia adhabu hivyo
wanatakiwa kufanya kazi hasa za kilimo ili kwanza kujipatia chakula na
sio kukaa tu bure na kusubiri kila kitu wafanyiwe na serikali.
Aliongeza
kuwa Serikali ina mkakati wa kutumia bajeti inayotengwa na nguvu kazi
wanayoipata kutoka kwa wataaalam walionao kwa upande wa askari Magereza
na wafungwa ili kukarabati Magereza chakavu na kujenga nyumba za askari.
Aidha
alibainisha kuwa suala la kukatwa kwa umeme katika Magereza, nyumba za
askari,pamoja na maeneo na maeneo mengine ya kambi za Jeshi la Polisi na
Magereza limeshafanyiwa kazi na serikali kwa kupitia hazina
imekwishatoa fedha kwa ajili ya kutatua tatizo hilo.
Mheshimiwa
Waziri aliliambia Bunge kuwa sheria zimeainisha baadhi ya haki za
mfungwa zikiwemo huduma za afya kwa wakati,kupewa chakula, uhuru wa
kutembelewa na ndugu zake na kupata mawasiliano kwa kusoma
magazeti,kusikiliza taarifa za habari na kuandikiwa barua na ndugu
zao,haki ya kukata rufaa ikiwa hakuridhika na hukumu yake, malazi safi
na yakutosha pamoja na kushiriki michezo mabalimbali.
0 comments:
Chapisha Maoni