Rais
wa Jamhuri ya Afrika ya Kusini Mhe. Jacob Gedleyihlekisa Zuma
amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali yake ya
Awamu ya Tano kwa kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa
(Standard Gauge) na ameahidi kuunga mkono ujenzi huo.
Mhe.
Rais Zuma ametoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo rasmi na alipokuwa
akizungumza na wananchi wa Tanzania na Afrika Kusini kupitia vyombo vya
habari Ikulu Jijini Dar es Salaam, ikiwa ni katika ziara yake rasmi ya
kiserikali ya siku mbili hapa nchini kwa mwaliko wa Mhe. Rais Magufuli.
Mhe.
Rais Zuma amesema anatambua kuwa ujenzi wa reli ya kati utaleta manufaa
makubwa kwa Tanzania na nchi za maziwa makuu na hivyo amekubali ombi la
Mhe. Rais Magufuli la kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa
Afrika ya Kusini kushirikiana na Tanzania kufanikisha mradi huo mkubwa.
Wakiwa
katika Mazungumzo rasmi viongozi hao wamezindua rasmi Tume ya Pamoja ya
Marais (Bi-National Commission-BNC) kwa kufanya kikao cha kwanza cha
tume hiyo tangu ianzishwe mwaka 2011 ambapo wamepokea makubaliano
yaliyofikiwa katika kikao cha tume ngazi ya mawaziri.
Kabla
ya kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari Mhe. Rais Magufuli
na Mhe. Rais Zuma wameshuhudia utiaji saini wa hati tatu za ushirikiano
kati ya Tanzania na Afrika Kusini ambazo ni Muhtasari wa makubaliano ya
mkutano wa tume ya pamoja ya Marais, Makubaliano ya ushirikiano katika
masuala ya bioanuwai na uhifadhi na makubaliano ya ushirikiano katika
sekta ya uchukuzi.
Akizungumzia
makubaliano na mazungumzo yao Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais
Zuma kwa kuitikia mwaliko wake na kukubali kuendeleza na kuongeza zaidi
ushirikiano na uhusiano kati ya nchi yake na Tanzania hususani
kuwahimiza wawekezaji na wafanyabiashara kuja kuwekeza nchini Tanzania
katika sekta mbalimbali zikiwemo Kilimo, ujenzi wa miundombinu, utalii,
madini na afya kwa kutumia uwezo mkubwa uliopo Afrika Kusini.
Mhe.
Rais Magufuli amesema hivi sasa biashara kati ya Tanzania na Afrika
Kusini kwa mwaka ni Shilingi Trilioni 2.4, uwekezaji wa Afrika Kusini
hapa nchini ni Dola za Marekani Milioni 803.15 uliozalisha ajira 20,916
na kwamba kiwango hicho kinaweza kuongezeka zaidi endapo ushirikiano
utaimarishwa zaidi.
“Na
ili tufanikiwe kukuza biashara tumekubaliana kuondoa vikwazo na
kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa nchi zetu mbili kutumia
fursa ya uhusiano na ushirikiano mzuri wa kirafiki na kidugu uliopo kati
ya nchi zetu kufanya kazi pamoja” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe.
Dkt. Magufuli ameongeza kuwa Tanzania itapeleka walimu wa lugha ya
Kiswahili ambayo inazungumzwa na watu takribani milioni 120 ili
wakafundishe lugha hiyo katika vyuo vya Afrika ya Kusini na hivyo
kuimarisha zaidi ushirikiano.
Kwa
upande wake Mhe. Rais Zuma amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumualika
kufanya ziara rasmi ya kiserikali hapa nchini na amesema nchi yake
itahakikisha makubaliano yote ya Tume ya Pamoja ya Marais yanatiliwa
mkazo na kutekelezwa kwa kuzingatia muda uliopangwa.
Mhe.
Rais Zuma amesema Afrika Kusini inatambua na kuheshimu mchango wa
mkubwa wa Tanzania kwa ukombozi wa nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo
Afrika Kusini ambayo Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere
alishirikiana na Waasisi wa Taifa hilo walioongozwa na Hayati Mzee
Nelson Mandela kupigania ukombozi na uhuru na kwamba anafurahi kuona
Tanzania bado inatoa mchango mkubwa kupigania amani katika bara la
Afrika.
“Mhe.
Rais Magufuli naomba nikuhakikishie kuwa Afrika Kusini itaendeleza na
kuimarisha zaidi uhusiano wake na ndugu na marafiki zake Tanzania katika
kujenga uchumi kwa manufaa ya wananchi na pia kupigania amani kwa kuwa
bila amani na usalama hakuna maendeleo” amesema Mhe. Rais Zuma.
Pamoja
na kufanya mazungumzo rasmi, viongozi hawa watashiriki mkutano wa
wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini (Business Forum)
unaofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere na jioni Mhe.
Rais Zuma atahudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na
mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam kabla ya
kurejea Afrika Kusini baadaye leo.