test

Jumamosi, 13 Mei 2017

Lowassa aelezea masikitiko yake ya kuzuiwa kwa kongamano la vyama vya siasa


Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward Lowassa amelaani kitendo cha Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam cha kuzuia kongamano la vyama vya siasa lililotarajiwa kufanyika leo Mei 13, 2017 katika Ukumbi wa Anatoglo, na kudai kuwa kitendo
hicho kinaminya uhuru wa demokrasia. 
Kongamano hilo lililenga kuwakutanisha viongozi wa vyama vya siasa, wachumi, wasomi, wafanyabiashara na taasisi za kijamii, kujadili hali ya kisiasa iliyopo nchini. Lakini  lilizuiliwa kwa sababu ya ukumbi huo kutaka kufanyiwa kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam, hata hivyo kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya kongamano hilo, Makongoro Mahanga anasema kikao hicho hakikufanyika.
Lowassa ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali yaliyotokea hapa nchini, ofisini kwake jijini Dar es Salaam. Ambapo amesema anasikitishwa kwa kuzuiliwa kufanya ziara ya kuwashukuru wananchi waliompigia kura katika uchaguzi mkuu uliopita, ilhali Rais John Magufuli akionekana katika baadhi ya mikoa akiwashukuru wananchi waliompigia kura.
 “Dhima ya kongamano hilo ni kuwaleta watanzania kwa pamoja kuzungumza demokrasia. Nawaomba wenzangu ndani ya CCM wajue kwamba iko siku nchi itatawaliwa na watu wasio katika chama chao,kuwaghasi wengine kwa sababu wako upinzani ni vibaya na nasikitika kuona jambo hili halikemewi, waasisi hawakemei,” amesema Lowassa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kongamano hilo.
Ameongeza kuwa “Kumetokea mtindo chama cha Chadema kinaandamwa sana kinasingiziwa kwamba kitaleta fujo, na watu wanaotuunga mkono wanaghasiwa kwa sababu wanaunga mkono chadema. Tusifikashane hapa tujenge nchi yetu kwa demokrasi kusiwe na malumbano.”
Aidha, Lowassa amezungumzia athari za mafuriko zilizokumba wananchi pamoja na uharibifu wa miundombinu ikiwemo barabara katika baadhi ya mikoa, ambapo ameitaka serikali kutoa pole kwa waathirika wa mafuriko hayo pamoja na kuchukua hatua.
“Kuna mafuriko makubwa nchini, yamefuatana na kipindi cha ukame mkubwa na wananchi wameathirika kwa ukame ule, pamoja na mafuriko kwa kiasi kikubwa, nachosikitika siuoni mkono wa serikali katika mafuriko yale wala kuwapa matumaini, kutoa pole kwa waathirika. Nadhani ni muhimu hoja ya mafuriko ikajadiliwa na serikali ili kueleza itafanya nini. Hii mvua haijanyesha kwa muda mrefu, kubwa zaidi hali ya chakula imekuwa ngumu bei ni kubwa, kwa mara ya kwanza bei ya mahindi imekuwa kubwa kuliko mchele, kipi serikali inakwenda kufanya kuhusu hili,” amesema.
Kuhusu Rais Magufuli kutohudhuria msiba wa wanafunzi zaidi ya thelathini wa shule ya Awali na Msingi ya Lucky Vincent iliyoko Mkoani Arusha, amesema kitendo hicho cha rais kutohudhuria pasina kutoa maelezo hadharani kimewasononesha na kuwahuzunisha wakazi wa mkoa huo na kumtaka kufika ili kutoa pole.
“Hili suala nalieleza kama mkazi wa Arusha, wiki iliyopita kulitokea msiba mkubwa yalifanyika mazishi baada ya kuaga maiti nilichosikitika na wakazi wengi wa Arusha wamesikitika pia, ni kitendo cha rais kutohudhuria mazishi ya msiba ule badalake alimtuma makamu wa rais, sina mgogoro na Samia lakini nasema kuna baadhi ya shughuli hatumwi mtoto, hii haikuwa shughuli ya kumtuma mtoto, amiri jeshi mkuu ndio mfariji mkuu,” amesema.
Kuhusu watumishi wa umma zaidi ya 9,000 waliofukuzwa kazi shauri ya kugushi vyeti, amesema “Ukisoma na kusikiliza hotuba za viongozi zinatisha na kutia hofu, mfano kuwafukuza wafanyakazi 9932, kwa wakati mmoja, sisemi wako sawa na siwatetei  bali nauliza ubinadamu wao, watu hawa elfu tisa wananyimwa mshahara wao na mafao, anakwenda wapi huyo mtu, hata kama wamefanya kosa inahitaji moyo wa huruma, natetea ubinadamu wake, wawafikirie hao vijana wazee waliojitoa kulitumikia taifa hili kwa uaminifu.”
Lowassa alimaliza kwa kushukuru wananchi wanaotumia mitandao ya kijamii kuelimisha wananchi ambapo amesema kuwa, jambo hilo litasaidia kuongeza uelewa wa wananchi na kuwapa mwamko wa kudai haki zao.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx