Mamlaka
ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imebaini makontena mengine 262
yenye mchanga wa dhahabu yaliyokuwa yamehifadhiwa katika bandari kavu ya
MOFED (zamani ZAMCARGO) iliyopo Kurasini jijini Dar es salaam
yakisubiri taratibu za kiforodha kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya
nchi kupitia kitengo cha makontena kinachoendeshwa na kampuni binfasi ya
TICTS.
Kubainika
kwa makontena hayo kumekuja siku tatu tu baada ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kutembelea bandari ya
Dar es salaam na kukagua makontena 20 yenye shehena ya mchanga wa
madini kutoka migodi mbalimbali iliyopo Kanda ya Ziwa.
Mhe.
Rais Magufuli alifika bandarini siku hiyo kukagua utekelezaji wa agizo
lake la kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga wenye madini kutoka
migodini.
Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi
Deusdedit Kakoko, amesema makontena hayo yaliyokuwa katika hatua za
mwisho kukamilisha taratibu za kiforodha yamebainika leo tarehe 25
Machi, 2017 katika msako mkali unaoendeshwa na Mamlaka yake.
Mhandisi
Kakoko amesema makontena yote hayo yalikuwa na lakiri (seals) za
Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), na yalikuwa yanashughulikiwa na
kampuni ya usafirishaji wa mizigo ya Freight Forwarders Tanzania Limited
iliyopo Dar es salaam.
Mhandisi
Kakoko amesema jumla ya makontena 256 yalikuwa katika bandari kavu ya
MOFED, wakati makontena mengine sita yalikuwa tayari yameshaingizwa
bandarini tayari kwa kusafirishwa.
Ametoa
wito kwa makampuni yote ya madini yenye shehena za mchanga yajitokeze
yenyewe na kuonesha mizigo yao popote ilipo nchini kabla haijabainika
katika msako kabambe unaondeshwa na vyombo vya ulinzi na usalama katika
maeneo mbalimbali nchi nzima.
Orodha
ya makontena hayo yaliyobainika inaonesha yalifika bandarini hapo
katika nyakati tofauti kutoka migodi ya Buzwagi na Pange Mines.
Kamanda
wa Polisi Kikosi cha Bandari Bw. Ramadhani Mungi amesema bandari zote
nchini ziko salama na kwamba ulinzi na usalama umeimarishwa kwa kuwekwa
askari na vifaa vya kisasa vya ulinzi zikiwemo kamera.