Serikali
imesema itatoa eneo linalomilikiwa na Shirika la Madini la Taifa
(STAMICO) Buhemba, Mkoani Mara kwa wachimbaji Wadogo wa Madini baada ya
kufanyika kwa tathmini na taratibu za kumilikishwa eneo ili wachimbaji
hao wafanye shughuli hizo kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu
ikiwemo kulipa kodi.
Kauli
hiyo imetolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
leo tarehe 18 Februari,2017, wakati wa ziara yake katika mgodi huo ili
kuangalia shughuli za uokoaji zinazoendelea katika mgodi huo,
kufuatia ajali ya kufukiwa na kifusi kwa Wachimbaji 18 iliyotokea
tarehe 13 Februari,2017, ambapo wachimbaji 13 waliokolewa siku hiyo hiyo
Prof.
Muhongo amesema kuwa, wachimbaji hao hawakuwa na leseni wala vibali
halali vilivyotolewa kwao kufanya shughuli za utafutaji dhahabu na
kwamba eneo hilo linamilikiwa kisheria na STAMICO kwa leseni PL N0.
7132/2011, na kuongeza kuwa, wachimbaji hao walivamia eneo hilo ambapo
ni kosa kisheria na wanatambulika kama wavamizi.
Ameongeza
kuwa, shughuli za uchimbaji katika eneo hilo zilifungwa tangu mwaka
1971 ambapo awali eneo hilo lilikuwa chini ya wakoloni kabla ya kuwa
chini ya uangalizi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Kampuni ya Meremeta
na baadaye kuwa chini ya umiliki wa STAMICO.
Aidha,
amezuia shughuli zote za uchimbaji kufanyika katika eneo hilo na kusema
kinachofanyika sasa ni kuutafuta mwili wa mchimbaji mmoja ambaye bado
haujatolewa. ''Hadi sasa wachimbaji 15 wamekwisha okolewa, bahati mbaya
wawili walitolewa wamefariki na sasa tuendelee na zoezi la kutafuta
mwili uliobaki,"ameongeza Prof. Muhongo.
Pia
Prof Muhongo amewshauri wachimbaji hao kujiunga katika vikundi na
kusajili vikundi hivyo ili kuwezesha shughuli zao kufanyika kwa
kuzingatia taratibu za uchimbaji. "Jiungeni katika vikundi , lakini ni
marufuku kwa familia moja kuwa na kikundi,"amesisitiza Prof. Muhongo
Kwa
upande wake Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Viktori Mashariki
Mhandisi Juma Sementa amesema kuwa, tayari Kanda hiyo imeshatoa maeneo
yapatayo 35 kwa wachimbaji wadogo katika eneo la Lwabasi, mkoani humo na
kueleza kuwa, leseni zote katika eneo hilo zinamilikiwa na
wachimbaji wadogo na hivyo kuwataka kufanya shughuli za uchimbaji kwa
kuzingatia usalama na ikiwemo kulipa kodi.
Mmoja
wa wachimbaji waliokolewa katika ajali ya kifusi akimweleza Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) jinsi ajali hiyo ya
kufikiwa na kifusi wachimbaji 18 ilivyotokea. Katikakti anayesikiliza ni Kaimu Kamishna wa Madini Mhandisi Ally Samaje.
Mmoja
wa wachimbaji wadogo akishuka chini ya shimo la kuingilia katika mgodi
kwa ajili ya kusaidia shughuli za uokoaji kufuatia ajali ya kufukiwa na
kifusi wachimbaji 18 katika eneo la Buhemba mkoani Mara.
Baadhi
ya Wafanyakazi wa Mgodi wa North Mara (ACACIA) ambao walishiriki
katika zoezi la uokoaji wa wachimbaji wadogo kwa kutoa msaada wa mashine
ya kuvuta maji na tope ili kuwezesha zoezi la ufukuaji kuendelea
Sehemu
ya Wachimbaji wakifuatilia mkutano wa Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo wakati wa ziara yake katika mgodi wa
Buhemba unaomilikiwa na STAMICO.
Mmoja
wa wachimbaji wadogo anayeshiriki zoezi la uokoaji katika eneo la
Buhemba akimweleza Waziri wa Nishati na Madini , Profesa Sospeter
Muhongo na wananchi waliokuwa eneo hilo kuhusu hali ilivyo ndani ya
mgodi huo.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akiongea na wachimbaji
wadogo katika eneo la Buhemba ambapo ajali ya wachimbaji wadogo
walifukiwa na kifusi tarehe 13 Februari,2017.