Siku
chache baada ya wabunge kueleza kutoridhishwa na Serikali kuhamia
kwenye majengo ya Chuo Kikuu Dodoma (Udom), Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Huduma na Maendeleo ya Jamii nayo imepinga hatua hiyo.
Kamati
hiyo pia imeshauri Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), kuachana na utaratibu wa
kupangia wanafunzi vyuo na ijikite kusimamia ubora wa elimu inayotolewa
na vyuo vikuu nchini.
Mapendekezo
hayo yametolewa bungeni mjini Dodoma na Mwenyekiti wa kamati hiyo,
Peter Serukamba alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa
shughuli za kamati hiyo kwa mwaka 2016.
Serukamba
amesema kamati hiyo ya Bunge inaunga mkono Serikali kuhamia Dodoma,
lakini utaratibu wa Wizara kuhamishia ofisi zao Udom siyo sawa.
Wizara
ambazo zimehamishia ofisi zake Udom kutoka Dar es Salaam ni Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora; Katiba na Sheria; Kilimo, Mifugo
na Uvuvi; Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia
na Ufundi.