Chama
cha Wananchi (CUF) kimesema hakitafanya mazungumzo kusaka suluhu na
mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na Msajili wa
Vyama vya Siasa na kwamba, kipo tayari kwa lolote hata kama kitafutiwa
usajili.
Aidha,
chama hicho kimesema hakijutii kumkaribisha na kumuunga mkono Edward
Lowassa, ambaye aliteuliwa kugombea urais mwaka 2015 kwa tiketi ya
Chadema na kuwakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Hayo
yamesemwa na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Mbarala
Maharagande kujibu madai yaliyotolewa na Profesa Lipumba alipokuwa
akifanya mahojiano na kituo kimoja cha televisheni hapa nchini.
Katika
mahojiano hayo, Profesa Lipumba alidai kuwa mgogoro uliopo ndani ya
chama hicho kwa sasa hautamalizwa na mahakama pekee bali viongozi wa
pande zote mbili wanatakiwa kuzungumza, lakini Maharagande amesema
haiwezekani kwa vile Lipumba alishakwisha kukivuruga chama na hafai tena
kuendelea kuwa kiongozi.
“Lipumba
anasema tukae tulimalize suala hili kwa kuongea sisi wenyewe. Jambo
hilo haliwezekani kwa kuwa kama kupandikiza chuki, uhasama, uharibifu wa
chama miongoni mwa wanachama na viongozi ameshafanya na kufanikiwa hilo
kwa baadhi ya wanachama na viongozi wake na kuharibu taswira ya chama
kwa jamii,” amesema Maharagande.