Wizara
ya Afya ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema ipo katika hatua
za mwisho za kutayarisha mwongozo wa kupiga marufuku matumizi ya uvutaji
wa sigara hadharani ili kudhibiti maradhi yasiyoambukiza yanayotokana
na sigara.
Hayo
yalisemwa na Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo wakati akitoa
ufafanuzi kuhusu uvutaji wa sigara hadharani katika sehemu za mkusanyiko
na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi.
Alisema
tayari Wizara ya Afya imewasilisha muswada wa kulinda afya ya jamii
ambao moja ya kazi yake kubwa ni kupambana na matumizi ya sigara katika
jamii na sehemu za mkusanyiko.
Akifafanua
zaidi, alisema utafiti uliofanywa kuhusu maradhi yasiyoambukiza
unaonesha kwamba upo kwa asilimia 38 ambayo yanahusishwa na uvutaji wa
sigara.
Kombo
alisema mwongozo huo ukikamilika utaletwa mbele ya wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi na wajumbe kutoa maoni yao kabla ya kufanya kazi na kuwa
sheria inayotakiwa kutekelezwa na kusimamiwa.
Alisema
yapo matumizi mabaya ya uvutaji wa sigara hadharani ikiwemo sehemu za
mikusanyiko ya watu kama hospitalini na sehemu za kusubiri usafiri wa
abiria na kusababisha madhara makubwa ambayo hayaonekani kwa mara moja.