Wakati Serikali ikiahidi kufanya
uchunguzi wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu katika kutimua
Watanzania nchini Msumbiji, mwanamke mmoja amesema alibakwa na askari
watatu kabla ya kuwekwa mahabausu ambako alikaa siku tatu bila kula.
Mwanamke huyo, aliyejitambulisha kwa jina la Halima (si jina lake
halisi) ni mmoja kati ya zaidi ya Watanzania 180 ambao wamekuwa
wakitimuliwa nchini Msumbiji tangu mwanzoni mwa wiki na wengi wakidai
wana hati halali za kuishi nchi hiyo jirani na wengine kulalamikia
vitendo vya ukiukwaji haki wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo.
Tayari Serikali imesema kuwa itafanya uchunguzi wa madai hayo, ambayo
yanaweza kuharibu uhusiano wa muda mrefu wa Tanzania na Msumbiji.
Halima anasema
walianza kufukuzwa usiku wa Jumamosi ya Februari 11, muda ambao askari
hao waliutumia kumfanyia kitendo hicho.
Halima anasema kuwa alisikia
watu wakivunja geti la nyumba waliyokuwa wakiishi na kudhania ni
majambazi, kumbe walikuwa ni askari ambao waliwalazimisha kutoa nyaraka
zao zote za kuishi Msumbiji pamoja na pesa.
“Niliwasikia wakivunja geti
nikamwambia mume wangu watakuwa ni majambazi kumbe askari, mume wangu
akajificha chini ya uvungu, lakini wakamtoa na baadaye kututoa ndani na
kuanza kutupiga.”
Anasema baada ya kipigo walilazimishwa kuzoa mali
zao kutoka ndani na zikawekwa kwenye gari la polisi na kisha kuwafunga
mikono na baadaye kuwapeleka mahabusu.
“Cha kushangaza tulibebeshwa vitu
wenyewe kuweka kwenye gari pasipo kuelezwa sababu baada ya hapo askari
akanivuta nyuma ya nyumba na kuniingilia kimwili. Nikajua ni mmoja,
lakini waliendelea hadi wakafikia watatu,” alisema.
“Ninaona aibu
walinibaka kwa njia ya kawaida tofauti na taarifa za wengine wanaosema
tulibakwa kinyume na maumbile, si kweli. Nawaomba waelewe hatukubakwa
kinyume na maumbile kama wanavyosema ilikuwa kawaida.”
Hata hivyo
anaeleza baada ya hapo waliwekwa mahabusu kwa siku tatu pasipo kula,
hali iliyowalazimu kunywa maji yaliyokuwa yamewekwa chooni.
“Tulikaa
mahabusu siku tatu, hamna kula wala kunywa, chooni tulienda kwa mtutu
tukalazimika kunywa maji ya chooni kwa sababu hakukuwa na jinsi na njaa
ilizidi. Kwa hiyo inabidi useme unakwenda chooni ili ukanywe maji,”
alisema Halima.
Kutokana na hali hiyo, Halima anashangazwa na kauli ya
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Susan Kolimba kwamba waliorudishwa
hawakuwa na nyaraka huku kaimu balozi wa Tanzania nchini Msumbiji
akiwatangazia wengine kuondoka ndani ya siku tano.
“Kweli mtu utathubutu
vipi kuishi nchi ya watu bila kibali? Hata kaimu balozi na yeye
anatukana, kwamba hatujaingia na documents (nyaraka)? Ilibidi atutetee
lakini katukana. Mungu atatulipia,” alisema.
Mwanamke mwingine
aliyewekwa mahabusu kabla ya kurudishwa nchini, Mary Makundi anasema
askari wa kiume walimwambia awape fedha na alipowajibu kuwa hana,
walimpekua na kuzikuta.
Anasema walizichukua fedha hizo pamoja na simu
kabla ya kumpiga na kutaka kumbaka.
“Walivunja mlango wakanikuta.
Wakaniambia niwape nyaraka zangu. Nikawapa nikijua wanazikagua tu na
kuniacha, lakini cha kushangaza walizichana mbele yangu na kunitaka
niwape pesa na simu. Nikawaambia sina wakanipiga na kunikagua hadi
sehemu za siri na kuchukua pesa na simu,” alisema Mary.
“Baada ya hapo
walinipiga kwanza kabla ya kunifunga mkono. Askari mmoja akataka
kunibaka, nikamwambia kuwa hata kama hawatutaki nchini kwao, hawawezi
kuniingilia bila kinga.
“Nilipoona hali imekuwa mbaya, nilisema wacha
nigombane nife kwa silaha, lakini si kubakwa.”
Mtanzania mwingine
Mohamedi Said ni mmoja wa wafanyabiashara walioambiwa waondoke pasipo
kuchukua chochote na anadai kuacha mali zake zote pamoja na nyumba
aliyojenga.
“Polisi walikuja ghafla wakatuambia wageni wote tunatakiwa
tuondoke. Hapa nina vibali vyote mpaka leseni ya biashara, lakini
imebidi niondoke kwa sababu ya usalama wangu,” alisema Said.
“Hakuna
anayejua sababu mpaka sasa. Nimekuja nyumbani kufuatilia haki yangu kwa
sababu mpaka kibali cha kujengea ninacho.
“Mpaka sasa amekuja kaimu
balozi kutoka ubalozi wa Tanzania na amesema kwa ripoti aliyopewa
ametupa siku tano tuondoke. Hatujui kwanini siku tano. Utahamishaje vitu
kwa siku tano au kumtafuta mnunuzi wa nyumba kwa siku tano kwa sababu
imenibidi niache duka kubwa na gari,” alisema Said.
Akizungumzia tukio
hilo, mwenyekiti wa Kijiji cha Kilambo kilichopo mpakani na Msumbiji,
Mohamed Mkama alisema wananchi wa kijiji chake wamekuwa wakishirikiana
na wanakijiji wa vijiji jirani vya Msumbiji, lakini tukio hilo
limewashangaza.
Amesema mara nyingi wamekuwa wakitembeleana na hata
wengine kutoka upande wa Msumbiji kuja kutibiwa Tanzania kutokana na
ujirani mwema uliopo.
“Kijiji changu kina vitongoji vitano ambavyo
tumekuwa tukishirikiana na kijiji cha upande wa pili kwa muda mrefu na
wengine wana vitambulisho vya uraia mwema, lakini tunashangaa kwanini
wanarudishwa pasipo kuelezwa sababu,” alisema Mkama.
Ofisa uhamiaji Mkoa
wa Mtwara, Rose Mhagama alisema idadi ya Watanzania waliorudi na
kusajiliwa katika mpaka wa Kilambo ni watu 221 hadi kufikia jana mchana.