Dodoma, Jumamosi, 4 Februari, 2017:
Serikali
imesisitiza kuwa, utekelezaji wa Bajeti kwa kipindi cha robo ya kwanza
yanaakisi dhamira ya kimageuzi iliyoanza kutekelezwa na Serikali ya
Awamu ya Tano.
Wakijibu
hoja zilizotokana na mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti
na maoni ya Wabunge Bungeni leo, Mawaziri wa sekta mbalimbali
wamesisitiza kuwa kuna mabadiliko makubwa katika kuwaletea wananchi
maendeleo.
Dhamira ya Rais Iko Wazi
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. January Makamba, amesema kuwa
ikiwa ni miezi 15 tu madarakani, kuna mabadiliko makubwa katika kila
eneo la utendaji wa Serikali ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Alisema hali hiyo inatokana na dhamira safi na ya wazi ya Mhe. Rais
Magufuli kuenzi misingi aliyoiacha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere.
Waziri
Makamba amesema miezi 15 baadaye, na Bunge likiwa linajadili takwimu za
robo ya kwanza tu ya Bajeti ya sasa, hata kama wapo watu ambao huenda
wameumizwa na mageuzi yanayoendelea, kwa vyovyote vile, hakuna hoja wala
ushahidi wa kulalamika kuwa nchi inarudi nyuma.
Biashara Zashamiri
Wizara
ya Fedha imetoa takwimu kuonesha kuwa biashara nchini zinashamiri
tofauti na baadhi ya watu wanaotumia takwimu za kufungwa kwa baadhi ya
biashara hizo. Wakichangia hoja, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Phillip Mpango na Naibu wake, Mhe. Dkt Ashatu Kijaji, wamefafanua kuwa
mapato ya Serikali yameongezeka na hali ya biashara inakwenda vyema.
Akifafanua
kuhusu kushamiri kwa biashara nchini, Naibu Waziri Dkt. Ashatu amesema
wakati takwimu zinaoonesha kuwepo kwa biashara 4,183 tu zilizofungwa,
watanzania wengi zaidi wamefungua biashara. Amesema kuwa takribani
biashara 139,554 zimefunguliwa katika mwaka mmoja uliopita.
Idadi ya Watalii Yaongezeka
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Mhe. Prof. Jumanne Maghembe amesema
kuwa,ubunifu wa kodi mpya zilizoanzishwa na Serikali haujapunguza idadi
ya wataliinchini. Alisema sekta hiyo inayochangia asimilia 17.5 ya pato
la Taifa kwa mwaka
baada ya kuanza kukata kodi mpya ya ongezeko la thamani katika sekta hiyo.
“Mheshimiwa
Spika pamoja na Tanzania kuanza kutoza kodi hii mpaka sasa ninayofuraha
kuwajulisha kuwa hatujaona ushahidi wa kodi hii kupunguza idadi ya
watalii wanaokuja nchini,” alisema Prof. Maghembe.
Mfumo Mpya wa Mbolea
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mhe. William Tate
Ole-Nasha, amesema Serikali itaanzisha mfumo mpya utakaosaidia
kuboresha upatikanaji na usambazaji wa mbolea nchini.
Amedokeza
kuwa, katika mfumo mpya, Serikali itaanza kununua mbolea kwa ununuzi wa
pamoja kama ilivyo katika ununuzi wa mafuta. Ameongeza kuwa pia
Serikali imebaini changamoto ya kuwepo kwa tozo nyingi katika sekta ya
kilimo na kuahidi kuwa itawasilisha Bungeni hoja ya kupunguza baadhi ya
kodi hizo.
Imetolewa na:
Idara ya Habari-MAELEZO.