Baadhi ya waumini wa makanisa ya Anglikana Dar es Salaam, nusura wazichape jana.
Hiyo
ni baada ya mapadri wao kutaka kusoma waraka wa Halmashauri ya Kudumu
ya Dayosisi ya Dar es Salaam unaomtetea Askofu wa Dayosisi hiyo, Dk.
Valentino Mokiwa, ambaye ametakiwa kujiuzulu kwa sababu ya kashfa
mbalimbali.
Waraka
huo uliokuwa unasomwa jana ulilenga kujibu uliotolewa na Askofu Mkuu
wa Kanisa hilo nchini, Dk. Jacob Chimeledya, ambao uliorodhesha tuhuma
zilizokuwa zikimkabili Dk. Mokiwa ukisema kwa sasa dayosisi hiyo itakuwa
chini ya Askofu Mkuu.
Baadhi
ya makanisa ya Dar es Salaam, Januari 8, mwaka huu yalisomewa waraka
huo wa Askofu Mkuu, Dk. Chimeledya huku mengine yakiwa hayajasomewa
licha ya kutakiwa kufanya hivyo na ngazi ya taifa.
Jinsi ilivyokuwa
Katika
baadhi ya makanisa, jana vurugu zilizuka mapadri walipoanza kusoma
waraka wa Halmashauri ya Kudumu ya Dayosisi ya Dar es Salaam.
Hapo
ndipo baadhi ya waumini walipogoma wakisema wanataka kwanza kusomewa
ule wa Askofu Mkuu wajue tuhuma zinazomkabili Dk. Mokiwa.
Katika
Kanisa la Mtakatifu Batholomayo Ubungo, hali ilikuwa mbaya zaidi
baada ya baadhi ya waumini kupiga kelele na kwenda kumzimia kipaza
sauti Padri wa Kanisa hilo, James Hiza, huku wengine wakinyanyuka kwenye
viti wakimtaka kutokuusoma waraka huo wa Mokiwa.
Kutokana
na kelele hizo ndani ya kanisa, mmoja wa waumini hao alikwenda kuzima
mfumo wa umeme na kusababisha vipaza sauti kutofanya kazi.
Hata hivyo, hatua hiyo haikusaidia kwa kuwa Padri huyo alikuwa akiendelea kusoma waraka huo.
Kuona hivyo, baadhi ya waumini walisikika wakisema ‘kama unasoma huo hakikisha unasoma waraka zote mbili’.
Hapo
Katibu wa Kamati Tendaji ya Kanisa, John Mapunda, alisimama akiwa
ameshikilia waraka wa Askofu Mkuu nao kumtaka ausome mbele ya waumini
na kuuacha aliokuwa akiusoma.
Hata hivyo, Padri huyo aliendelea kusoma waraka aliokuwa nao na kutowajali waliokuwa wakimtaka kuacha kusoma waraka huo.
Mbali na katibu huyo wa kanisa, pia mzee wa makamo alikwenda kumsihi Padri huyo kutosoma waraka huo.
Lakini
juhudi zao hazikuzaa matunda kwani alisoma waraka huo mpaka mwisho
ingawa waumini waliendelea kupiga kelele muda wote bila kumsikiliza.
Baada ya kumaliza kusoma waraka huo Padri, Hiza alirudi na kukaa katika nafasi yake huku akiwataka waumini kutulia.
Waondoka na sadaka
Baada
ya kumaliza kusoma waraka huo na vurugu kutulia, baadhi ya waumini
ambao hawakuridhika na yaliyotokea walionekana kususa shughuli nyingine
ikiwa ni pamoja na kutoa sadaka.
Waumini
hao licha ya kuwa na bahasha maalumu ambazo hutumika kutolea sadaka,
muda wa matoleo ulipofika, waliendela kukaa kwenye viti vyao wakiwa na
bahasha zao.
Pia wengine walisusa kushiriki Meza ya Bwana ingawa wahudumu waliwasihi wasifanye hivyo.
“Tusimfanyie hasira Mungu, hata kama mmekasirika vumilieni tuendelee na ibada yaani hata kupokea mwili hamtaki?” aliwauliza mhudumu wa kanisani humo.
Baada
ya ibada, Katibu wa Kamati Tendaji, Mapunda aliwaambia waandishi wa
habari kuwa walikuwa wamefanya kikao na kukubaliana kutosoma waraka
wowote kwa sababu Jumapili iliyopita hawakuusoma ule uliotolewa na
Askofu Mkuu. Dk. Chimeledya.
“Waraka wa Baba Askofu Chimeledya hakuusoma wiki iliyopita, alisema hajaupata kumbe ulikuwapo.
“Siku chache badaye na Askofu Mokiwa ambaye ameshafukuzwa katoa waraka wake.
“Huo
ndiyo alitaka kuusoma tukamwambia kwa kuwa ule wa kwanza haukusomwa
kanisani na huu usiusome au usome zote ili tusiingie katika mgogoro
huu. Alikubali lakini kafika madhabahuni akatugeuka,” alisema Mapunda.
Padri Hiza alipofuatwa na waandishi kuzungumzia suala hilo alisema, “Hili suala limefikia ngazi ya juu ya dayosisi, mimi siwezi kuliongelea kwa kuwa si msemaji wa dayosisi.”
Wakati hayo yakiendelea, polisi walikuwa wametanda nje ya kanisa hilo.
Baada
ya vurugu kutulia kanisani, polisi hao walionekena wakizungumza na
Katibu wa Kamati ya Utendaji ya Kanisa, Mapunda na baadaye wakaondoka
kwenye eneo hilo.
Hali
ya sintofahamu ilitokea pia katika Kanisa la Hollyghost Kimara Mbezi
ambako mgogoro wa kutaka kusoma waraka wa Dk. Mokiwa au usisomwe,
uliibuka na mwisho Padri akaamua kuacha kuusoma.
Kabla ya Padri kuacha kuusoma, zilizuka vurugu za hapa na pale kiasi cha watu kufikia hatua ya kutaka kupigana.
Katika
Kanisa la Mtakatifu Mariam Padre wa kanisa hilo alitaka kuusoma waraka
wa Mokiwa lakini waumini walikuja juu na kuusoma wa Askofu Mkuu Dk.
Chimeledya.