Wakati
Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli akitekeleza masuala mbalimbali
aliyowaahidi Watanzania, ikiwa ni pamoja na kurejesha uwajibikaji na
kupambana na ufisadi, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amesema
hashtushwi na utendaji huo wa rais, kwani amekuwa akitumia baadhi ya
hoja na mikakati ya Chadema kuongoza nchi.
Akizungumza
wakati wa kumnadi mgombea wa udiwani katika kata ya Isagehe wilayani
Kahama, Sumaye ambaye alijiunga Chadema Agosti mwaka juzi baada ya
kuachana na CCM, alisema mengi anayofanya rais ni sera za Chadema ila
chama hicho cha upinzani hakikuwa na sera ya kubana fedha.
Hata
hivyo, Sumaye ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya Chadema hakuweka wazi
hoja na mikakati ya Chadema inayotekelezwa na Rais Magufuli ambaye tangu
aingie madarakani ameweka msimamo katika suala la kubana matumizi ya
Serikali, kudhibiti watumishi hewa na safari za ndani na nje zisizo na
tija na rushwa.
Katika
mkutano huo ambao pia Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa alihutubia,
Sumaye alisema kama wananchi, wangemchagua Lowassa kuwa Rais,
angewaletea neema ya hali ya juu kwa kuwa angekuwa na misingi katika
sera anazozitekeleza.
“Mmechagua
Rais mzuri (Magufuli), lakini anafuata sera za chama chetu (Chadema)
ambazo tungezitumia kama tungekuwa madarakani. Wananchi wa Kanda ya Ziwa
mnatakiwa kumtumia Rais Magufuli ili kufanikisha malengo yetu,” alisema huku akisisitiza kuwa hata Lowassa wananchi wangeweza kumtumia kufanikisha malengo yao.
Huku
akimnadi mgombea udiwani wa kata hiyo, John Luzinga, Sumaye aliwataka
wananchi kutofanya makosa tena ya kuichagua CCM, ili wasije kujuta kwa
maelezo kuwa watalazimika kuchagua diwani mwingine mwaka 2020.
Alisema
Chadema kinaendeshwa kwa kufuata misingi ya demokrasia, huku akikosoa
vyama kubanwa wakati nchi iriuridhia mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Akizungumzia
sababu za kuhama CCM, alisema kulitokana na nchi kukumbwa na hali mbaya
ya uchumi sambamba na kukosekana kwa utawala bora.
“Serikali
pamoja na kubana matumizi, hali ya uchumi imekuwa mbaya. Inatakiwa
kuachia fedha ili kuwafikia wananchi waweze kumudu ugumu wa maisha
unaowakabili kwa sasa. Haiwezekani kila Serikali isijifunze katika hili
wakati hata wataalamu wanazungumza na kushauri masuala mbalimbali,” alisema Sumaye.
Alisema
kitendo cha halmashauri tatu za wilaya ya Kahama kuongozwa na CCM, huku
diwani mmoja tu ndio akiwa wa Chadema, kitawafanya wananchi hao kukosa
watu sahihi wa kuwasemea mambo yao.
Uchaguzi katika kata hiyo utafanyika Januari 22 sambamba na kata nyingine 21 katika maeneo mbalimbali nchini.