Rais
wa Tanzania Dkt. John Magufuli amezuia serikali kupeleka chakula cha
msaada wilayani Misenyi mkoani Kagera kwa madai kuwa wilaya hiyo haina
sababu ya kukumbwa na tatizo la njaa.
Rais Magufuli amekataa serikali kupeleka chakula cha msaada katika wilaya hiyo na kusema haikubaliki kwa eneo hilo lenye mvua za kutosha na hali nzuri ya kilimo na kwamba haiwezekani kulia njaa wakati kuna uwezekano wa kuzalisha kwa ajili ya chakula.
Amesema
hayo wakati akiweka jiwe la msingi katika kituo cha afya cha kata ya
Ishozi Wilayani Misenyi Mkoani Kagera ambapo yupo kwa ziara ya kikazi ya
siku mbili mkoani humo kukagua maendeleo mbalimbali.
Katika
hatua nyingine Rais Magufuli, amesema kuwa serikali haitaweza kujenga
makazi ya kila mwathirika wa tetemeko mkoani Kagera kwa kuwa ina jukumu
la kujenga miundombinu itakayokuwa na manufaa kwa jamii nzima kama
Zahanati, Shule na barabara.
Amesema
kuwa kuna baadhi ya watu ambao nyumba zao hazikuharibika kiasi kikubwa
lakini wakadanganywa na baadhi ya watu kuwa watajengewa hivyo
wakazibomoa kwa kutaka kujengewa nyumba mpya.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipiga
makofi mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika Kituo cha Afya cha
Kabyaile Misenyi Mkoani Kagera.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akikagua
maeneo ya ujenzi wa kituo hicho cha Afya cha Kabyaile kilichopo Misenyi
mkoani Kagera.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza
na wananchi katika eneo la mradi wa ujenzi wa kituo hicho cha Afya cha
Kabyaile kilichopo Misenyi mkoani Kagera.