Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amewahakikishia Watanzania kuwa licha ya Mamlaka ya udhibiti wa huduma
za Nishati, Maji na Mafuta (EWURA) kuridhia ombi la TANESCO la
kupandisha bei ya umeme kuanzia Januari mosi,2017 bei ya umeme
haitapanda.
Rais
Dkt. Magufuli amezungumza hayo leo Jumapili ya Januari Mosi, 2016
wakati wa Ibada katika Kanisa la Bikira Maria Mama Mwenye Huruma,Kanisa
Kuu Jimbo Katoliki la Bukoba anapoanza rasmi ziara ya kikazi ya siku
mbili Mkoani Kagera.
Rais
Magufuli ameshangazwa na kitendo cha watendaji waliopandisha bei ya
umeme bila hata ya kushauriana na yeye, Makamu wa Rais,Waziri Mkuu au
Waziri mwenye dhamana ya Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo na
hivyo kumshukuru Waziri Muhongo kwa kutengua maamuzi hayo.
''Ninamshukuru
sana Waziri wa Nishati na Madini kwa maamuzi ya kusitisha hayo kwa hiyo
umeme hakuna kupanda bei,haiwezekani unapanga mikakati ya kujenga
viwanda na hasa katika mikakati mikubwa ya nchi ya kusambaza umeme mpaka
vijijini,na umeme huu unaenda kwa watu masikini walioumbwa kwa mfano wa
Mungu halafu mtu pekee kwa sababu ya cheo chake anapandisha bei,hili
haliwezekani'' Alisema Rais Dkt. Magufuli.'
Aidha,
Rais Dkt Magufuli ameendelea kuwataka watanzania katika mwaka huu mpya
2017 kuendelea kufanya kazi kwa bidii kama maandiko matakatifu
yanavyoelekeza kuwa asiyefanya kazi na asile badala ya kulalamika kuwa
fedha zimepotea.
Kwa
upande wake,Askofu Msaidizi Jimbo Katoliki la Bukoba,Askofu Methodius
Kilaini,akitoa mahubiri kwa waumini waliohudhuria ibada hiyo amempongeza
Rais Dkt Magufuli kwa uongozi wake imara,huku akisema kupungua kwa
urasimu katika ofisi za umma kunatokana na utendaji kuongezeka na
kuwataka wana Kagera na Watanzania kwa ujumla kumuunga mkono Rais
Magufuli kwa kufanya kazi kwa bidii na uaminifu.
Mara
baada ya Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo
Katoliki la Bukoba,Askofu Desderius Rwoma,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt John Pombe Magufuli aliwatakia heri ya mwaka mpya waumini
wa kanisa hilo na watanzania kwa ujumla.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kagera.
01 Januari, 2017