Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameugiza
uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), kumpelekea nyaraka
zote zilizotumika katika kumhamisha faru maarufu kwa jina la John katika
hifadhi hiyo ifikapo Desemba 8, 2016.
Majaliwa
amesema ana taarifa kuwa walimhamisha Faru John Kreta kwa siri na
kumpeleka V I P Grumet Serengeti Disemba 17, 2015 na waliahidiwa
kupewa sh. milioni 200 ambapo na wamepewa sh. milioni 100 kwa ahadi ya
kumaliziwa sh. milioni 100 nyingine baadaye.
Amesema
hayo Desemba 6, 2016 alipotembelea Ofisi za makao makuu ya NCAA,
zilizoko wilayani Ngorongoro mkoa Arusha wakati akizungumza na
watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafugaji ikiwa
ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani hapa.
“Naomba
niletewe nyaraka zote zilizotumika kumuomba na kumuondoa faru huyo na
barua zilizotumika kujadili suala la faru John. Nasikia amekufa naomba
pembe ziletwe ofisini na iwapo itathibitika aliondoka bila ya kufuata
taratibu wahusika wote watachukuliwa hatua kali za kisheria,”.
Aidha,
Majaliwa amepiga marufuku tabia ya baadhi ya watumishi wa mamlaka hiyo
ambao wanawakabidhi watoto kupeleka ng’ombe wao ndani ya kreta. “
Watumishi wa Ngorongoro ndiyo wanaopeleka ng’ombe ndani ya kreta na si
wenyeji. Sasa marufuku na tutakayemkuta hatutakuwa na msamaha naye,”.
Amewataka
watumishi hao kuhakikisha wanakuwa waadilifu na wanafanyakazi kwa
kufuata misingi ya kiutumishi na kuacha tabia za kuendekeza rushwa na
wizi.
Wakati
huo huo Waziri Mkuu amemsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa NCAA, Sezzary
Simfukwe kutokana na tuhuma za ubadhilifu wa fedha zinazomkabili na
tayari anahojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU).
“Haiwezekani
mtumishi awe anachunguzwa na TAKUKURU halafu aendelee kuwa ofisini si
atavuruga uchunguzi. Asimamishwe kazi kuanzia leo mpaka hapo uchunguzi
utakapokamilika na aikibainika kwamba hana hatia atarudi kazini,”
alisema.