WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wananchi kuacha tabia ya kuhifadhi fedha
nyingi majumbani na badala yake wajenge utamaduni wa kuzipeleka benki
kuepusha kuhatarisha usalama wao.
Ametoa
ushauri huo jana (Jumatatu, Desemba 5, 2016) wakati akifungua tawi la
benki ya Biashara ya Uchumi lililopo wilayani Karatu mkoani Arusha akiwa
katika ziara yake ya kikazi mkoani hapa.
Alisema
tabia ya baadhi ya wananchi kuhifadhi kiasi kikubwa cha fedha majumbani
si nzuri kwa sababu wanahatarisha usalama wao, hivyo ni vyema wakatumia
benki mbalimbali zilizoko kwenye maeneo yao kwa ajili ya kutunza fedha
zao.Akizungumzia kuhusu kufunguliwa kwa tawi la benki ya Uchumi wilayani
Karatu, Waziri Mkuu alisema unaashiria ukuaji wa uchumi wa wilaya hiyo
kwa kuwa benki ni kichocheo cha maendeleo.
Katika
hatua nyingine Waziri Mkuu aliushauri uongozi wa benki ya Uchumi
kuangalia uwezekano wa kupunguza kiasi cha riba wanachokitoza katika
mikopo wanayoitoa ili kuwawezesha wananchi kukopa na kupata tija.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo Bw. Wilson
Ndesanjo alisema benki hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo
ya mtaji mdogo jambo linalowasababisha washindwe kufungua matawi katika
mikoa mingine.
“Changamoto
nyingine ni baadhi ya wateja kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati,
ambapo hatua za kisheria zikichukuliwa wanakimbilia mahakamani. Matukio
haya yanadhoofisha kasi ya utoaji wa huduma kwani kesi zinachukua muda
mrefu,” alisema.
Bw.
Ndesanjo alisema kuna baadhi ya kesi zimechukua miaka sita bila ya
kumalizika hivyo kuzuia fedha ambazo kama zingerejeshwa kwa wakati
zingezungushwa kwa wananchi wengine.
Benki
ya Uchumi ilianzishwa Septemba 22, 2005 ikiwa na mtaji wa sh. milioni
372. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2016 mtaji huo umefikia sh.
bilioni 5.4 hivyo umeongezeka mara 14.5 zaidi ya ule wa awali
uliokuwepo wakati wa uanzishwaji wake.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMANNE, DESEMBA 6, 2016.