Kikosi
maalumu cha kupambana na wizi wa kutumia silaha na wizi wa kutumia
nguvu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kimewakamata watuhumiwa
22 kwa makosa ya kuwapora wenye magari na wapitanjia kwenye mataa ya
kuongozea magari.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi wa Kanda
hiyo, Simon Sirro alisema watuhumiwa hao, wamekuwa wakijiunda kwenye
vikundi na kuwanyang’anya watu wenye magari na watembea kwa miguu mali
zao kama simu za mikononi, kompyuta, saa na fedha.
Alisema
ufuatiliaji ulifanyika na kuwakamata watuhumiwa hao kwa nyakati
tofauti, ambapo Desemba 11 mwaka huu huko Temeke maeneo ya Keko
Magurumbasi na mataa ya Veta na Chang’ombe walikamatwa watuhumiwa 10 kwa
makosa ya wizi kutoka maungoni na wizi kutoka kwenye magari.
Aliwataja
baadhi ya watuhumiwa hao kuwa ni Ayubu Amiri (19), mkazi wa Mtoni
Mtongani, Shabani Fadhili(18) mkazi wa Keko, Herman Francis (26), mkazi
wa Keko Magurumbasi na wenzao saba.
“Katika
mahojiano watuhumiwa wamekiri kujihusisha na makosa mbalimbali yakiwemo
unyang’anyi wa kutumia silaha na kutumia nguvu,” alisema.
Aidha
alisema uchunguzi wa awali umebaini mtuhumiwa Herman Francis
anakabiliwa na tuhuma za mauaji, ambapo Machi 20 mwaka huu alimchoma mtu
kisu na kutoroka kusikojulikana.
Wakati huo huo, Desemba 12 mwaka huu askari waliwakamata watuhumiwa wengine 12 kwa makosa ya wizi kutoka kwenye magari.
Watuhumiwa
hao wametajwa kuwa ni Sande Kassim (18), mkazi wa Keko, Emmanuel Abeli
(21), Paulo Abeli(18), Jafari Nyerere (22), Hamis Salum (22), Hemed
Idrisa(22) wote wakazi wa Keko na wenzao sita.
Katika
tukio lingine, polisi wamewakamata watuhumiwa wanne wanaojihusisha na
wizi kwa kuwarubuni watu kwa kukodi magari yao na baadaye hutumia nguvu
kuwapora.
Watuhumiwa
hao wametajwa kuwa ni Juma Kajeni (35), mkazi wa Tabata, Hamadi Kaganda
(38), mkazi wa Mbagala, Mashaka Ally(62), mkazi wa Yombo na Mshamu Ally
(32), mkazi wa Mtongani.
Alisema watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na upelelezi utakapokamilika watapelekwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.
Pia
aliwatahadharisha wananchi na wamiliki wa magari kuwa makini kwa watu
hao ambao huja kwa nia ya kuwalipa fedha nyingi au kukodi gari kwa
kiwango kikubwa na kisha wanatokomea na gari.
Wakati
huo huo, polisi Kanda Maalum Dar es Salaam kupitia kikosi kazi chake
cha kupambana na wizi wa magari kimekamata magari matatu ya wizi katika
mikoa mbalimbali.
Sirro
alilitaja gari lenye namba T 386 CGY aina ya Verosa rangi nyeusi, mali
ya Abraham Robert wa jijini Dar es Salaam na gari hilo lilikamatwa
mkoani Mbeya likiwa limetelekezwa.
Gari
jingine ni lenye namba T 946 DGH aina ya IST rangi ya fedha ikiwa
inaendeshwa na mtuhumiwa aitwaye Hamadi Saidi (27) mkazi wa Kimara Dar
es Salaam ambalo lilikamatwa huko mkoani Morogoro, gari hilo liliibiwa
maeneo ya Kawe Beach jijini Dar es Salaam.
Alilitaja
gari lingine kuwa ni Mitsubishi Canter lenye namba T 753 CVZ ambazo ni
namba bandia huku namba zake halisi zikiwa ni T.815 DJF mali ya Magreth
iliibiwa maeneo ya Kimara Suka jijini Dar es Salaam.
Alisema mtuhumiwa mmoja aliyekamatwa anaendelea kuhojiwa na upelelezi utakapokamilika atapelekwa mahakamani.
Pia
alisema watuhumiwa wengine waliohusika na wizi wa magari hayo
wanaendelea kutafutwa ili kubaini mtandao mzima wa wizi wa magari na
watuhumiwa wengine wanaotafutwa kwa wizi wa magari hapo nyuma ambao
walikimbia.