Kamati ya Utendaji ya CUF imepitisha majina matatu ya wanaowania
kuteuliwa kugombea ubunge katika Jimbo la Dimani, Mkoa wa Mjini Mgharibi
kisiwani Unguja.
Wakati CUF imepitisha majina hayo yatakayokwenda
kwenye mchujo wa kura ya maoni ndani ya chama hicho kupata jina moja,
CCM nao wamepitisha majina matatu ambayo ni Juma Ali Juma, Hussein
Migoda Mataka na Abdalla Sheria yatakayopitia mkondo huohuo.
Uchaguzi
huo utakaofanyika Januari 22, mwakani umetangazwa na Tume ya Uchaguzi
ya Taifa (NEC), kujaza nafasi ya Hafidh Ali Tahir aliyefariki dunia
ghafla mkoani Dodoma hivi karibuni wakati akihudhuria vikao vya Bunge.
CUF itakuwa ikishiriki uchaguzi huo kwa mara ya kwanza baada ya kususa
ule wa marudio uliofanyika Machi 20, kutokana na kitendo cha Mwenyekiti
wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta uchaguzi
uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar,
Nassor Ahmed Mazrui alitaja majina hayo kuwa ni Abdulrazak Khatib
Ramadhan, Asha Hamad Makungu na Ahmed Abass Haji, ambao watapigiwa kura
jimboni huko ili kumpata mmoja atakayeiwakilisha CUF.
Akizungumza baada
ya kikao hicho kilichoongozwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad,
Mazrui alisisitiza kuwa chama hicho hakitazikubali hujuma zote, yakiwamo
masharti hayo ya NEC aliyoyaita ya mfukoni.
Katika hatua nyingine, CUF
imesema inaendelea na mazungumzo na vyama vinavyounda Ukawa kuona
namna bora ya kushiriki uchaguzi mdogo ujao jimboni humo ili kuhakikisha
wanaibwaga CCM.
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Joram Bashange
alisema chama hicho bado ni sehemu ya Ukawa na hakuna mtu yeyote mwenye
uwezo wa kutengua uamuzi huo.
“Suala hilo lilipitishwa na Mkutano Mkuu
wa Taifa uliofanyika tarehe 23 mpaka 27 Juni, 2014 na mkutano mkuu
ndicho chombo cha juu kabisa na chenye maamuzi ya mwisho katika chama,”
alisema.
Kikao hicho kilikuwa na ajenda moja ya maandalizi ya uchaguzi
mdogo wa madiwani 22 Tanzania Bara na ubunge wa Dimani.
Kamati ya
Utendaji ilipitisha ratiba ya uchaguzi wa ndani ya chama kwa ajili ya
kuwapata wagombea wa CUF katika nafasi hizo.
Wakati huo huo, Bashange
amesema Kamati ya Utendaji ya Taifa imeshangazwa na kauli ya
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima kwamba wagombea wa CUF
lazima fomu zao za uteuzi zithibitishwe na kutiwa saini na pande mbili
zinazohasimiana.
“Kailima amekitoa wapi kifungu cha sheria au kanuni,
alichokitumia kuweka sharti hilo la ajabu tena kwa chama kimoja tu,”
alisema na kuongeza:“Huwezi kuwa na sharti linalokihusu chama kimoja tu
katika kuthibitisha uteuzi wa wagombea.”
Alisema fomu za uteuzi wa
wagombea kutoka NEC huthibitishwa na katibu wa chama wa ngazi
inayohusika na kwa ubunge na madiwani ni katibu wa wilaya.