Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana aliongoza mamia ya waombolezaji kuaga mwili wa marehemu Mzee Xavery Pinda ambaye ni baba mzazi wa Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa Mizengo Pinda.
Akizungumza wakati wa kuaga mwili huo nyumbani kwa Mheshimiwa Pinda kijijini Zuzu, Manispaa ya Dodoma jana Waziri Mkuu alitoa pole kwa wanafamilia na kuwaomba waendelee kumuombea marehemu apumzike mahala pema peponi.
Mzee Xavery alifariki dunia Novemba 27, 2016 saa 9.30 alasiri katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma alikokuwa amelazwa akipatiwa matibabu.
Alisema msiba huo ni mzito, hivyo anawaomba wanafamilia wawe watulivu na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao.
Wakati huo huo Waziri Mkuu alimuhakikishia Mheshimiwa Pinda kwamba Serikali iko pamoja naye katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mzazi wake.
Naye Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dk. Jakaya Kikwete alisema marehemu Mzee Xavery alikuwa mwema sana na alikuwa na upendo kwa watu wote.
“Baba yake Pinda alikuwa baba yangu pia. Alitambua ugumu wa kazi tulizokuwa tunazifanya na alitutaka tuwe wavumilivu,” alisema.
Kwa upande wake Mheshimiwa Pinda aliwashukuru viongozi wa Serikali, vyama vya siasa na wananchi kwa kutenga muda wao na kwenda kumfariji kufuatia msiba huo mzito. “Kuondokewa na baba mzazi au mwanafamilia yeyote si jambo dogo”.
Awali akisoma wasifu wa marehemu, Edward Kyungu ambaye ni mjukuu alisema Mzee Xavery alizaliwa mwaka 1926 katika kitongoji cha Mbede akiwa ni mtoto wa pekee wa Mzee Mizengo Pinda na Mama yake Wakalyate (Umartina).
Mzee Xavery alikuwa Katekista kazi ambayo aliifanya kuanzia mwaka 1951 hadi 1972 alipoamua kustaafu.
“Kazi ya pili ambayo alianza kuifanya kabla na hata wakati wa Ukatekista ni ukulima, jambo ambalo amewarithisha watoto wake wote na ndio maana wameachiwa sifa moja ya kuitwa watoto wa mkulima,”alisema.
Mzee Xavery anatarajiwa kuzikwa leo Alhamisi, Desemba Mosi, 2016 katika kijiji cha Kibaoni wilaya ya Mlele mkoani Katavi. Marehemu ameacha mke, watoto wanane, wajukuu 54 na vitukuu 40.