TUME
ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza ratiba ya uchukuaji wa fomu za kujaza
nafasi zilizo wazi ya Mbunge na Madiwani katika maeneo mbalimbali hapa
nchini.
Imesema
kuwa inatarajia kuendesha Uchaguzi Mdogo katika Jimbo la Dimani , Mkoa
wa Mjini Magharibi ,Tanzania Zanzibar kufuatia kifo cha Mbunge wa Jimbo
hilo.
Kwa
mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo jijini Dar es
salaam na Tume hiyo, hatua hiyo itanatokana na vifungu vya 37(1)(b) na
46(2) vya sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Vifungu vya 13(3)
na 48(2) vya Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura 292.
Aidha
,Tume hiyo pia itaendesha Uchaguzi Mdogo wa kujaza nafasi za wazi za
Udiwani katika kata 22 kwenye baadhi ya Halmashauri za Tanzania Bara
zilizokuwa wazi kutokana na sababu mbalimbali.
Imezitaja
Kata hizo Ng’hambi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma,
Ihumwa ya Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, Kiwanja cha Ndege ya
Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Igombavanu na Ikweha za Halmashauri
ya Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa pamoja na Ngarenanyuki iliyopo
Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mkoani Arusha.
Kata
nyingine ni Kijichi ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Mkoani Dar es
Salaam, Kata ya Kinampundu ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mkoani
Singida, Isegehe ya Halmashauri ya Mji wa Kahama Mkoani Shinyanga,
Kasansa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Mkoani Katavi, Malya na
Kahumulo Mkoani Mwanza, Maguu na Tanga Mkoani Ruvuma pamoja na Kata ya
Kimwani Mkoani Kagera.
Imeongeza
kuwa Kata nyingine ni pamoja na Nkome Mkoani Geita, Kata ya Lembeni
Mkoani Kilimanjaro, Mkoma ya Mkoani Mara, Duru ya Mkoani Manyara,
Mwamtani ya Mkoani Simiyu, Misugusugu ya Mkoani Pwani pamoja na Mateves
ya Mkoani Arusha.
Tume
hiyo imesema kuwa zoezi la kutoa fomu za uteuzi litaanza Desemba 10
hadi 22 na kufuatia kwa zoezi la uteuzi wa wagombea siku ya tarehe 22
mwezi Desemba na Desemba 23 hadi Januari 21 mwakani itakuwa ni kipindi
cha kampeni ambapo Januari 22 mwakani itakuwa siku ya kupiga kura.