Dk Mwakyembe ametoa pongezi hizo jana alipokutana na Makonda ofisini kwake jijini Dar es Salaam wakati viongozi wa wizara hiyo walipomtembelea kumpongeza na kuunga mkono jitihada zake katika kuhakikisha wananchi wa Dar es Salaam wanapata haki zao kwa wakati.
“Mkuu wa Mkoa nimekuja hapa hii leo (juzi) na timu yangu kukupongeza na kukuonesha kwamba tunakuunga mkono na tuko pamoja kuhakikisha upatikanaji haki na huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi vinapatikana kwa wakati,” amesema Dk Mwakyembe.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Sifuni Mchome alisema wizara imenufaika na ziara ya Makonda ambayo ilimpatia fursa ya kusikiliza kero, malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi na kuonesha kuwa wananchi wengi wanahitaji msaada wa huduma za kisheria ili kupata haki zao kwa wakati.
Makonda akizungumza katika kikao hicho, alisema uongozi wa mkoa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo wanatarajia kujenga mahakama mpya 20 kuanzia mwaka 2017, kukabiliana na upungufu wa mahakama mkoani humo kwa kuwa mkoa una mahakama za mwanzo 12 wakati mahitaji halisi ni mahakama 102.
Makonda amesema uamuzi wa kujenga mahakama hizo unaenda sambamba na mpango wa kujenga vituo vya polisi katika kila kata ambao ulisaidia kugundua kuwa ili haki itendeke tena kwa wakati kwa wananchi watakaopelekwa katika vituo hivyo vya polisi, ni lazima kuwe na mahakama.
Amesema ziara aliyoifanya mkoani hivi karibuni ilimpatia fursa ya kusikiliza kero za wananchi na kugundua kuwa wananchi wengi wanakabiliwa na tatizo la kutopata haki kwa wakati, uelewa mdogo wa namna ya kupata haki zao hali ambayo inawasababisha wengi wao kukosa haki zao kwa wakati.
Amesema mpaka sasa anao vijana 35 ambao ni wahitimu wa shahada ya sheria ambao wamepatiwa mafunzo maalum na mwanasheria wa mkoa na atawasambaza vijana hao katika wilaya zote za mkoa ili kuwahudumia wananchi kwa kuwapatia msaada wa huduma za kisheria.