Watu
wanne wakiwamo polisi wawili, wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa
wakisafiria kuacha njia na kupindua katika kijiji cha Seruka kata ya
Chipogoro tarafa ya Rudi wilayani Mpwapwa mkoa wa Dodoma.
Ajali
hiyo ilitokea Desemba 19, mwaka huu, saa 11:30 jioni katika kijiji
hicho baada ya gari walilokuwa wakisafiria T517 CDL Toyota Alphat katika
barabara kuu ya Dodoma- Iringa, kuacha njia na kupinduka na kusababisha
vifo vya watu wanne na majeruhi tisa.
Kaimu
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Ernest Kimola, amesema gari hiyo
iliyokuwa ikiendeshwa na Aggrey Lucas, baada ya kufika katika kijiji
hicho, liliacha njia na kupinduka na kusababisha vifo vya askari
Konstebo Mahende na Konstebo Sasi Mwita ambaye ni askari mkoa wa Songwe.
Kamanda Kimola amewataja wengine waliofariki katika ajali hiyo ni mke wa Konstebo Mwita, Pendo Mwita na Emaculata Nyangi.
Amewataja
majeruhi wa ajali hiyo ni Neema Mwita (8), Jenifa Mwita (4), Nyangi
Wambura (23), Konstebo Nashon (23) ambaye ni polisi kituo cha Tunduma na
Baraka Chacha (9).
Wengine
ni Juli Mwita (6), Pc Enock ambaye ni mmiliki wa gari lililopata ajali,
Makongoro Charles na Elizabeth Cosmas ambao wote wamelazwa katika
hospitali ya mkoa wa Dodoma.
Aidha,
kamanda Kimola amesema miili ya marehemu hao waliofariki katika ajali
hiyo, imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali
ya mkoa wa Dodoma.