Mambo
aliyohoji wakati akifanya majumuisho ya ziara yake mkoani Arusha ni
juzi, Faru John aliumwa lini, aliumwa nini, daktari gani aliyemtibu na
zilipo taarifa za matibabu yake.
Pia
aliagiza mwili wa faru huyo kufukuliwa na kutazama kama vinasaba vyake
vinaendana na watoto wake 26 ambao bado wapo katika Creta ya Ngorongoro.
Akizungumza
na mwandishi wetu jana, mmoja wawahifadhi wa Sasakwa Grumet aliyeomba
kutotajwa jina ili kutoathiri uchunguzi wa tukio hilo, alisema kitaalamu
wanyama ambao wanakufa bila kuwa na magonjwa ya mlipuko katika maeneo
ya hifadhi hawazikwi.
“Faru
John baada ya kufa aliondolewa pembe zake na kutupwa ili kiwe chakula
cha wanyama wengine wanaotegemea mizoga, lakini kuna mifupa yake,”
alisema.
Alisema
faru huyo aliombwa na Grumet kwenda kupanda faru waliopo katika eneo
hilo, hasa baada ya dume aliyekuwapo huko kuuliwa na tembo.
“Baada ya kuonekana kuna haja ya kutafuta dume, ndipo tuliomba kupata faru dume na tukaletewa na baadaye alikufa,” alisema.
Eneo
hilo la Sasakwa Singita Grumet ni mali ya mfanyabiashara mkubwa raia ya
Marekani, bilionea Tudor Jones ambaye amewekeza katika maeneo kadhaa ya
uhifadhi.
Akifafanua
hatua zinazochukuliwa baada ya mnyama kufa katika hifadhi, mhifadhi
Peter Isango alisema kwa kawaida huzikwa au kuchomwa moto pale tu
wanapobainika kuwa na magonjwa kama kimeta.
Kauli
hiyo iliungwa mkono na mkurugenzi mkazi wa shirika la uhifadhi la
kimataifa la Frankfurt Zoological Society, Gerald Bigurube ambaye
alisema kwa kawaida wanyama wanaokufa hifadhini huwa hawazikwi.
Bigurube
ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa
(Tanapa) alisema kwenye kanuni za uhifadhi kitu chochote, kinachokufa
ndani ya hifadhi huachwa kwa ajili ya kulinda ikolojia na bionuwai.
“Mnyama ambaye anakufa kwa kifo cha kawaida mzoga wake unapaswa kuachwa kuoza na kutumiwa na wanyama wengine,” alisema.
Alisema
hata wanyama wa kawaida kama swala na wengine wanapoumwa huwa
hawatibiwi tofauti na wanyama kama tembo, faru na wengine wakubwa ambao
hutibiwa.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu Faru John, Bigurube alisema taasisi yake haikuwahi kushiriki katika suala hilo.
Wapata dhamana
Katika
hatua nyingine, Polisi imewaachia kwa dhamana maofisa watano wa Mamlaka
ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Tanapa waliokuwa wanashikiliwa kwa
tuhuma za kumhamisha Faru John kutoka Creta ya Ngorongoro na kumpeleka
Sasakwa Grumet.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema jana kuwa licha ya dhamana hiyo, uchunguzi unaendelea.
Watuhumiwa
hao ni Israel Naman ambaye alikuwa kaimu mkuu wa idara ya hifadhi
wakati faru huyo akiondolewa, Cuthbert Lemanya aliyekuwa mkuu kanda ya
Creta, Dk Athanas Nyaki ambaye ni daktari wa mifugo wa mamlaka hiyo.
Wengine ni aliyekuwa kaimu mkuu idara ya maendeleo ya jamii, Kuya Sayaleli na kaimu mkuu idara ya ikolojia, Patrice Mattey.
Kabla
ya kukamatwa, maofisa hawa walikiri kushiriki kumhamisha Faru John
kutoka Creta ya Ngorongoro hadi Sasakwa kwa maelezo kuwa ilikuwa ni
kuendeleza uhifadhi wa faru na pia kutokana na ukorofi wa Faru John
kuhodhi majike yote ndani ya Creta kuua madume wengine waliozaliwa.
Akiwa
katika ziara ya kikazi mkoani Arusha, Waziri Mkuu alitoa taarifa za
kifo cha faru John huku akiwatuhumu baadhi ya watendaji wa NCAA kuhusika
na njama za kumuuza kwa Sh200 milioni ambazo alisema walishapokea
malipo ya awali ya Sh100 milioni.
Baada
ya maelezo hayo, Waziri Mkuu alitaka kupewa taarifa kamili za tukio
hilo, pamoja na pembe za faru huyo, ambazo alikabidhiwa Desemba 8 na
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na kaimu
mkurugenzi wa msaidizi kitengo cha kupambana na ujangili, Robert Mande
ambaye alimweleza kuwa taratibu zilifuatwa katika kumhamisha.