Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa ameiomba Serikali ya Uingereza ihamasishe
wawekezaji zaidi kutoka nchini humo ili waje kuwekeza kwenye sekta ya
viwanda.
Ametoa
kauli hiyo jana (Jumanne, Novemba 8, 2016) wakati akizungumza na Balozi
wa Uingereza hapa nchini, Bibi Sarah Cooke alipokutana naye ofisini
kwake Bungeni, mjini Dodoma.
“Mheshimiwa
Balozi utusaidie kualika wawekezaji wengi zaidi kwenye maeneo ya
kilimo, viwanda vya usindikaji mazao ya wakulima, wavuvi na wafugaji,
sekta ya mafuta na gesi, nishati na ujenzi wa makazi hasa kwa mkoa wa
Dodoma ambako hivi sasa ni Makao Makuu ya Serikali,” alisema.
Alimweleza
Balozi huyo kwamba Tanzania imedhamiria kuwa nchi ya uchumi wa kati na
hivyo imejipanga kuwa na viwanda vya kutosha ili iweze kusindika mazao
yake hapa nchini na itoe ajira kwa wananchi wake.
Waziri
Mkuu alitumia fursa hiyo pia kuishukuru Serikali ya Uingereza kwa
msaada wake mkubwa wa ujenzi wa nyumba za walimu na shule mkoani Kagera
zilizoathiriwa na tetemeko la ardhi lilitokea Septemba 10, mwaka huu.
Kwa
upande wake, Balozi Cooke ambaye alifika kujitambulisha rasmi, amesema
ameguswa na juhudi zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na
masuala ya ufisadi na rushwa. “Kaulimbiu yenu kwamba rushwa haikubaliki
(zero tolerance on corruption) inaonyesha jinsi mlivyodhamiria kupambana
na baa hili,” alisema.
Alisema
Uingereza inaongoza miongoni mwa nchi zenye wawekezaji wengi hapa
nchini na kwamba inaendeleza mpango wake wa uwekezaji ambao unalenga
maeneo makuu manne ambayo ni gesi na mafuta; kilimo; nishati jadidifu na
uimarishwaji wa mazingira ya kufanya biashara.
Balozi
Cooke alitumia fursa hiyo kutoa pole kwa Serikali kutokana na msiba wa
Spika Mstaafu wa Bunge la Tisa na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Urambo,
Tabora, Mheshimiwa Samwel Sitta kilichotokea usiku wa kuamkia Novemba 7,
mwaka huu katika hospitali ya Technical University of Munich nchini
Ujerumani alikokuwa akipatiwa matibabu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,