Raia
watatu wa China wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya kumteka na kumjeruhi raia mwenzao,
Liu Hong.
Washitakiwa
hao, Chen Chuw Bao (34), Wang Yong Jim (37) na Zheng Pa Jin (40)
wamefikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu
Mkazi Mfawidi, Cyprian Mkeha.
Wakili
wa Serikali, Hellen Moshi alidai kuwa Oktoba 21, mwaka huu katika
maeneo ya Palm Beach Ilala, Dar es Salaam Wachina hao walimteka raia
mwenzao wa China, Liu Hong ili kumuweka kizuizini.
Alidai
kuwa siku hiyo katika maeneo hayo ya Palm Beach, washitakiwa
walimshambulia Hong katika sehemu za mwili na kusababisha apate maumivu
ya misuli.
Baada ya kusomewa mashitaka Bao alikiri kutenda makosa yote, huku Jim akikiri kosa moja na Jin alikana mashitaka yote.
Wakili
Moshi alidai kuwa amepokea taarifa kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa
wa Kipolisi Ilala, Dar es Salaam, SSP Salum Ndalama akiiomba Mahakama
isitoe dhamana kwa washitakiwa hao.
Wakili
Moshi alidai SSP Ndalama ametoa zuio hilo kwa kuwa washitakiwa hao ni
raia wa China, pia hawana kazi wala hati za makazi ya kudumu.
Aidha,
kuna taarifa za kuaminika kwamba washitakiwa hao na watuhumiwa wengine
ambao hawajakamatwa wanapanga njama za kujihusisha na vitendo vya
kihalifu ukiwemo utekaji.
Alidai
washitakiwa hao na wengine ambao hawajakamatwa wana mpango wa kulipiza
kisasi na endapo wakipata nafasi ya kupewa dhamana, wanaweza kwenda
kupoteza ushahidi.
Wakili
huyo, aliongeza kuwa rai ya SSP Ndalama ni kuwa, washtakiwa hao
waendelee kubaki rumande hadi kesi hiyo itakapoisha ili kumlinda
majeruhi pamoja na ushahidi. Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mkeha
aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 11, mwaka huu.