UZALISHAJI katika kiwanda cha saruji cha Dangote kilichopo Mtwara umesimama kwa muda kutokana na hitilafu za kiufundi zilizojitokeza katika mitambo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dangote Tanzania, Harpreet Duggal alisema jana kwamba mafundi wa Dangote wapo kazini na shughuli za uzalishaji zitarejea katika siku chache zijazo.
Alisema kiwanda kinachomilikiwa na bilionea namba moja Afrika, Alhaji Aliko Dangote wa Nigeria kilianza uzalishaji wa kibiashara mwaka huu na kama ilivyo kwa kiwanda kingine kama hicho, jambo lolote linaweza kutarajiwa hasa katika miezi ya mwanzo.
Alisisitiza, “hitilafu hizi ni za kawaida na uzalishaji utarejea katika kipindi kifupi kijacho.”
Akizungumzia gharama za uzalishaji, Duggal alisema uendeshaji nchini uko juu huku miongoni mwa sababu ikiwa ni matumizi ya jenereta za dizeli katika kuendesha kiwanda.
Hata hivyo, alisema serikali inaangalia suala hili la gharama na jinsi ya kutafuta njia ya kuwapunguzia mzigo.