Hayo yalisemwa jana jijini humo na Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda wakati akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Temeke akiwa katika ziara ya siku mbili wilayani humo. Alisema watumishi wengi wamekuwa mizigo na wanasubiri kuchukua mishahara bila kuifanyia kazi hivyo ni bora kuwasimamisha kwa manufaa ya umma.
“Nafikiri kuna haja ya kuwapunguza watumishi serikalini hakuna wanachofanya zaidi ya majungu na umbea, asilimia 20 ndio wanaofanya kazi, tayari nimeongea na Rais na kuna taratibu nakamilisha na tutachukua hatua,” alisema Makonda.
Aidha Makonda alisema watumishi wengi wa umma wanaishia kula fedha za miradi na matokeo yake wanatengeneza miradi mibovu ambayo imekuwa ikichukuwa muda mfupi kuharibika.
Makonda aliwashangaa watumishi wanaoshindwa kufanya kazi na kudai hawana bajeti wakati wana uwezo wa kuzungumza na wadau na kupata fedha nyingi na kuendesha miradi.
“Tumechoka kusikia kelele za kukosa bajeti, yapo mambo hayahitaji bajeti lakini hamfanyi tangu kuteuliwa kwangu nimeweza kufanya miradi ya zaidi ya Sh bilioni 30 ambayo sio ya bajeti, lakini nyinyi mnapiga kelele za bajeti, tukiona hamuwezi kubadilika tutawastafisha tunataka watu wanaofikiria nje ya boksi,”alisema Makonda.