test

Jumanne, 8 Novemba 2016

Rais Magufuli Alitaka Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) Liongeze Kasi ya Uzalishaji wa Mazao ya Chakula


Shirika la uzalishajimali lililo chini ya Jeshi la Kujenga Taifa (Suma – JKT) litaanza kutekeleza mpango wa kufuga samaki kwa kutumia vizimba (Cages) katika bahari ya Hindi baada ya mpango huo kuonesha mafanikio makubwa katika mito na maziwa mbalimbali hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa JKT Meja Jenerali Michael Isamuhyo muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Meja Jenerali Isamuhyo amesema ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba umepata mafanikio makubwa katika maeneo mbalimbali nchini hususani katika ziwa Viktoria na kwamba ili kupanua ufugaji huo Suma-JKT inajielekeza kufuga samaki katika bahari ya Hindi.

Ameongeza kuwa pamoja na ufugaji wa Samaki, Rais Magufuli ameliagiza Jeshi la Kujenga Taifa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na shughuli zilizotajwa katika misingi ya uanzishaji wa jeshi hilo ili Serikali isipate gharama za kununua chakula kwa ajili ya vijana wanaokwenda kupata mafunzo ya JKT na pia kupata chakula cha ziada ambacho kitatumika kutatua tatizo la uhaba wa chakula katika maeneo yatakayokumbwa na uhaba.

Meja Jenerali Isamuhyo ameongeza kuwa Rais Magufuli ameitaka JKT kujenga mabwawa kwa ajili ya kuanzisha kilimo cha umwagiliaji katika maeneo yanayofaa kwa kilimo hicho.

Aidha, Mkuu huyo wa JKT amebainisha kuwa JKT itahakikisha inasimamia utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais na kuongeza kuwa kazi hii itakwenda sambamba na utekelezaji wa majukumu mengine ya JKT yaliyoainishwa katika uanzishwaji wake mwaka 1963 ikiwemo ujenzi kwa gharama nafuu.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Jenerali Mstaafu George Marwa Waitara Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

08 Novemba, 2016

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx