Mkutano wa Tano wa Bunge umeahirishwa kwa namna yake baada ya muhimili huo wa dola kupata misiba mikubwa miwili.
Misiba hiyo ni wa Spika Mstaafu, Samuel Sitta aliyefariki nchini Ujerumani na Mbunge wa Dimani(CCM) Hafidh Ally ambaye alifariki dunia usiku wa kuamkia leo (Ijumaa) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Dodoma.
Mara baada ya kutangaza kifo cha Hafidh Spika wa Bunge, Job Ndugai alimtaka Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge, Ajira, Kazi, Vijana Jenista kutengua kanuni ili kuwezesha mambo vote kufanyika.
Spika alimtaka Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo Ndogo, Andrew Chenge kuhitimisha hoja yake ya taarifa ya Kamati iliyowasilishwa juzi bila kujadiliwa na wabunge ili Serikali yaweze kufanyia kazi.
Baada ya kufanya hiyo, Spika ameahirisha bunge hadi saa 8.30 mchana kwa ajili ya kikao maalum cha Bunge.
Amesema mara baada kikao maalum cha bunge kumuaga Sitta basi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atatoa hoja yake kuahirisha Bunge kwa kifupi sana tofauti na wakati mwingine.