test

Alhamisi, 3 Novemba 2016

Mawaziri Wasulubiwa Bungeni


Bunge la Jamhuri ya Muungano jana liliweka kando tofauti zao za kisiasa wakati lilipowaweka kwenye kibano mawaziri watano kutokana na utendaji wao.

 Wabunge wa chama tawala na upinzani walionyesha makali yao wakijadili Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2017/18 na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao, ikiwa ni mwaka mmoja tangu Serikali ya Rais John Magufuli iingie madarakani.

 Mbali na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, mawaziri wengine waliowekwa kwenye hali ngumu ni Ummy Mwalimu, ambaye ni Waziri wa Afya, Angellah Kairuki (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utumishi), Charles Mwijage (Viwanda, Biashara na Uwezeshaji) na Profesa Joyce Ndalichako (Elimu, Sayansi na Teknolojia). 

Mwongozo huo wa mpango wa kuandaa bajeti unaonyesha Serikali itatumia Sh32.9 trilioni kwa mwaka ujao wa fedha, ikiwa ni ongezeko la Sh3.4 trilioni kulinganisha na bajeti ya mwaka huu. 

Mjadala wa wabunge hao ulijielekeza katika kuchambua utendaji wa mawaziri hao na hali ilivyo kwenye wizara zao, hasa kiuchumi ambayo inaelezwa kuwa ngumu kutokana na wananchi kudai fedha zimepotea kwenye mzunguko.

Aliyefungua mashambulizi hayo ni mbunge wa Busega (CCM), Dk Raphael Chegeni aliyesema Dk Mpango ni msomi, lakini ana “kiburi, si msikivu na hataki kushauriwa”. 

Dk Chegeni alisema wabunge walimshauri mambo mengi waziri huyo katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2016/17, lakini hakutaka kusikiliza na ndiyo maana hali imekuwa ngumu kila eneo. 

‘’Dk Mpango unapaswa kuwa msikivu na kuacha kiburi. Tunayokushauri yachukue (kwa kuwa) tunakusaidia ufanye kazi.Tulikuambia mambo mengi, ukatudharau sasa yanatokea, kila kona hakuna unafuu,’’alisema.

Dk Chegeni alisema uchumi ambao anauzungumziwa kwenye mpango wake hauendani na hali halisi ya maisha ya wananchi, akisema hata halmashauri hazijapewa fedha hadi sasa. 

“Wananchi hawana fedha, wabunge hawana fedha. Fedha ambazo Mamlaka ya Mapato (TRA) inaeleza kuwa inakusanya, ziko wapi wakati madeni yameongezeka?”

Alimtaka waziri huyo kutimiza wajibu wake kwa unyenyekevu na kwa kusikiliza ushauri wa wabunge kuhusu wizara yake.

“Umekuwa ni tatizo sana. Hata ukiitwa na jumuiya za wafanyabiashara huendi, ukiitwa na kamati ya Bunge ya Bajeti huendi.Umekuwa mgumu kupatikana, dhamana uliyopewa ni kubwa, usitumie vibaya mamlaka yako,” alisema Dk Chegeni. 

Mbunge mwingine aliyechangia alikuwa John Heche (Tarime Vijijini-Chadema), ambaye alisema mtu wa pili kutumbuliwa na Rais John Magufuli baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga atakuwa Dk Mpango. 

“Kwa sababu gani utakuwa ni wa pili kutumbuliwa? Kwa sababu mambo yanapokwama, mipango yote mliyopanga inapokwama, wewe ndiye unabebeshwa zigo hilo ili yeye aonekane yuko sawa wakati mnakosea wote,” alisema. 

Heche alisema wamesimamisha ajira kutafuta watumishi hewa kwa mwaka mzima, lakini wako vijana waliosomeshwa na baba zao wako mitaani kwa kukosa ajira. 

“Dada zetu wanajiuza, mikopo nayo hakuna, mnatafuta wanafunzi hewa. Kilimo nako mnatafuta wakulima hewa. Cha msingi mseme kuwa Serikali yenu imefilisika na hamuwezi kutekeleza kitu chochote, msaidiwe,” alisema. 

Mbunge wa Solwa (CCM), Ahmed Salum aliwataka wabunge wa CCM kumwambia ukweli Dk Mpango kuwa wanakwenda kugonga mwamba katika uchumi.

“Unajiuliza fedha zimekwenda wapi? Unakuja hapa unasema kuwa uchumi umekua, how (kwa vipi)? Twiga imeshakuwa taken over (imeshachukuliwa), CRDB imetangaza hasara na TIB hasara,” alisema. 

Alisema hali hiyo inaonyesha kuwa baada ya miaka miwili benki hizo zinakwenda kufungwa na huo utakuwa ni mgogoro wa kiuchumi nchini. 

Alisema hilo huenda linatokana na mawaziri kutokwenda kuomba kura na hivyo hawafahamu joto la maisha lililopo kwa wananchi majimboni. 

“Mimi natoka Jimbo la Solwa, unaahidi, unadanganya hadi unachoka. Alikuwa JK ameondoka, anakuja Magufuli ataondoka hakuna lililofanyika,” alisema. 

Aliitaka Serikali kurejesha fedha za mifuko ya hifadhi ya jamii ilizoziweka “kabatini” Benki Kuu na mifuko hiyo iziweke fedha hizo kwenye benki za biashara ili fedha zianze kuzunguka.

Aliitaka Serikali kulipa madeni ya ndani ili fedha zianze kuzunguka na kwamba kumekuwa na joto hata ndani ya Bunge, akisema kuna ukata.

Salum alisema makusanyo ya kodi yanayotangazwa na kuonekana kuwa makubwa yanatokana na watu kulipa madeni ya nyuma na mara baada ya kuisha kwa malimbikizo hayo, makusanyo yatabaki kama ilivyokuwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne. 

“Watalipa itafika mahali itakwisha na kubaki na makusanyo ya siku hiyo, cash revenue (fedha taslimu). Hapo ndipo itashuka kutoka Sh1.5 trilioni hadi Sh800 bilioni iliyoachwa na Rais Jakaya Kikwete,” alisema. 

“Haya madeni yakiisha tutarudi kukusanya bilioni. Hatuwezi kufika trilioni hizo za leo. Tuna matatizo. Kipindi cha Kikwete, TRA ilikuwa inakusanya Sh850 bilioni, lakini nchi ilikuwa nzuri na mambo mengi yalienda vizuri kuliko sasa.” 

Alisema Rais Magufuli amekuwa na maono mazuri ya kuifanya nchi kufikia mafanikio ya Thailand, lakini tatizo wasaidizi wake hawamwambii ukweli ama wanaogopa kufukuzwa. 

“Magufuli tulikuwa naye hapa kwa zaidi ya miaka 10, namfahamu. Ukienda na data (takwimu) ukamueleza kukimbiwa na wafanyabiashara bandarini, atakuelewa,” alisema. 

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussen Bashe alisema mipango ya Dk Mpango haifanani na ahadi walizozitoa kwa wananchi kuwa watawaboreshea hali ya uchumi watakapowachagua. 

“Kwa sababu kaka yangu (Dk Mpango) hujaenda kuomba kura? Dunia imebadilika tunaenda kufa tunapaswa kubadilika,” alisema Bashe. 

Alisema miradi mingine kama wa chuma wa Liganga na makaa ya mawe wa Mchuchuma ameanza kuisikia muda mrefu, lakini hajaona utekelezaji. 

Bashe alisema Waziri Dk Mpango anazungumzia bajeti ya Sh33 trilioni na kwamba eneo la kwanza ni makusanyo ya kodi kuongezeka kwa asilimia 16, wakati siyo mazuri. 

Alisema wabunge waliwahi kuwaambia wasiweke kodi kwenye uhamishaji wa fedha, utalii na maeneo mengine, lakini hawakuwasikia. 
 
Ndalichako 
Wakizungumzia hali ya elimu, wabunge walimkosoa Waziri Ndalichako kutokana na hali inavyoendelea, hasa suala la mikopo ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu. 

Akichangia eneo hilo, Heche alianza kwa kukosoa kitendo cha Profesa Ndalichako kwenda kupiga kura katika uchaguzi wa meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni uliofanyika wiki mbili zilizopita jijini Dar es Salaam. 

“Leo elimu ni majanga. Mimi nilikuwa nakuheshimu sana Profesa Ndalichako ukiwa Katibu wa Baraza (la Mitihani la TaifaNecta). Umewahi kuonyesha watu wamechora mazombi kwenye mitihani,” alisema. 

“Wewe umepewa wizara hii, umechora Zombie kubwa kuliko wale waliochora kwenye mitihani, sijui hata wizi wa mitihani utazuiaje kama wewe Profesa ulitoka hapa kwenda kuiba kura Kinondoni.” 

 Alisema hivi sasa Bunge wamelifanya kama idara fulani ya Ikulu inayohusika na umwagiliaji maji katika maua. 

Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Wataira alisema Ndalichako alipiga kura za kuwachagua mameya wa halmashauri za manispaa za Kinondoni na Ilala. 

“Ulikuwapo juzi kwenye uchaguzi wa meya Kinondoni wakati ulishapiga kura katika umeya wa Ilala, Profesa mzima unahusika katika wizi wa kura,” alisema. 

Mwijage
Pia Waziri Mwijage alikuwa kwe- nye kikaangio hicho. Akichangia suala la mpango wa Serikali kuifanya Tanzania iwe nchi ya viwanda, Dk Chegeni alisema Mwijage ni “mzee wa sound” ambaye anafanya porojo. 

“Waziri wetu anajulikana kama mzee wa porojo, sijui hiyo Tanzania ya viwanda tutafika lini. Acheni maneno maneno na kusigana wenyewe kwa wenyewe. Mnatofautiana kauli, kila mmoja anaongea lake.  Fanyeni kazi kwa pamoja kila wizara itoe maoni yake katika huo Mpango,”alisema Dk Chegeni. 

Naye Heche alisema hata kwa Watanzania wanamjua Mwijage kwa jina la “Mzee wa Sound”. “Ukikutana naye hapo nje ukamsimamisha waziri, anauliza ‘vipi unataka nikupe kiwanda’ na kutoa mkono mfukoni. 

Anataka kuchomoa kiwanda mfukoni? Mpango wenu hamjajenga kiwanda hata kimoja,” alisema. 

Alisema kiwanda ndicho kitaajiri watu wengi wakiwemo mamantilie, wahasibu wahandisi na wengine wengi, lakini hadi sasa hakuna kiwanda hata kimoja. 

Kairuki 
Akizungumzia suala la watumishi hewa, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo) Zitto Kabwe alionyesha kushangazwa na kitendo cha mawaziri kutoa taarifa zinazotofautiana. 

 “Monthly Economic Review (taarifa ya uchumi ya mwezi) ya Agosti 2015 inaonyesha kwamba wages and salaries (mishahara) ambazo Serikali ililipa Juni mwaka 2015 zilikuwa Sh456 bilioni. 

"Monthly Economic Review ya Agosti 2016 inaonyesha kwamba wages and salaries ambazo Serikali imelipa kwa mwezi Juni 2016 ni Sh534 bilioni,” alisema Zitto.

“Kwamba kuna nyongeza ya gharama za mishahara ya kila mwezi ya Sh78 bilioni. Waziri wa Utumishi jana ameeleza wanaokoa Sh19 bilioni kila mwezi kwa kuondoa watumishi hewa. Taarifa ya Benki Kuu inaonyesha kuwa tangu Serikali hii iingie madarakani, gharama za watumishi kwa mwezi zimeongezeka kwa Sh78 bilioni.”

 Zito alisema pamoja na watumishi hewa kuondolewa, ajira mpya kuzuiwa na nyongeza ya mishahara kusimamishwa, gharama za mishahara zimeongezeka kwa Sh78 bilioni. “Haiekeweki. 

Kuna mmojawapo kati ya hawa wawili (Waziri Kairuki na BOT) anadanganya umma. Ama zoezi la watumishi hewa ni publicity stunt (la kujitafutia umaarufu) au Serikali inatumia fedha kwa matumizi mengine, halafu BOT inasema ni mishahara,”alisema Zitto.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx