Tangulia Spika wa Bunge la Wananchi
Hotuba ya ndugu Kiongozi wa ACT Wazalendo katika Kikao Maalumu cha Bunge cha Mazishi ya Spika Mstaafu, Samwel John Sitta Ndugu Spika,
Ndugu Wabunge,
Mama Magreth Sitta,
Watoto wote wa Mzee Samwel John Sitta, Ndugu, Jamaa na Marafiki,
Ndugu zangu Watanzania,
Leo kikao maalumu cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Mkutano wake wa Tano kinamuaga mtoto wa Mzee John Sitta na Hajjat Zuwena Said Fundikira. Nami nimepewa nafasi niseme maneno machache kuhusu mzee wetu huyu tunayemuaga.
John Samwel Sitta anayo mengi, lakini Tanzania itamkumbuka kama mtu aliyejaribu kuboresha kila alichokabidhiwa kama jukumu, shujaa wa wote wanaoamini katika Uwajibikaji wa kitaasisi, Mwanasiasa aliyepanda na kushuka na kisha kupanda na kubakia kileleni, taswira ya mkoa wake wa Tabora, sio tu mdhamini wa klabu ya Simba, bali pia Mwanasimba aliyeipeleka klabu Brazil na kuwezesha kuifunga Yanga mabao mengi zaidi ambayo hayajapata kulipwa na wapinzani wetu hata kwa kuungakuunga, Mwanamageuzi wa Bunge na Spika wa mioyo ya Watanzania.
Hata katika kifo chake, Samwel John Sitta ameweka rekodi nyengine – kwa Bunge kufanya kikao maalumu kuenzi mmoja wa wajumbe wake mahiri kati ya mwaka 1975 – 2015 isipokuwa tu kwa kipindi cha 1995 – 2005. Rekodi hii itaendelea kwa wengine wote watakaofuata baada yake.
Ni mtu wa namna gani wewe Samwel Sitta? Spika wa Kasi na Viwango, unayeweka rekodi hata ukiwa umelala ndani ya Jeneza lako lililopambwa na Bendera ya Taifa letu ukielekea nyumbani kwako Urambo kwenye nyumba yako ya milele. Ulikuwa hushindwi ukiwa hai, umeonyesha umahiri wako hata ukiwa kwenye umauti. Kweli wewe ni Spika wa Watu (The Peoples Speaker).
Tuliokupenda tunajua. Ulikuwa Baba mlezi. Ulikuwa Mume mwema. Ulikuwa Babu. Ulikuwa Kiongozi. Nadhani hata kwa uliokwaruzana nao hapa na pale wanajua hilo. Leo sote tuna majonzi makubwa. Umeliunganisha Taifa katika kukukumbuka ewe Spika wa Watu.
Ulikuwa na vyeo vingi; Mbunge, Naibu Waziri, Waziri, Mkuu wa Mkoa, Waziri tena, Mkurugenzi Mtendaji, Spika, Waziri tena na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba. Lakini, wala, tunakuita Spika Sitta tu. Kwanini? Kwa sababu ‘Legacy’ yako ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sio kwamba umeanzisha Bunge wewe, la hasha. Lakini ulipopokea Uspika wa Bunge letu, kama ilivyo jadi yako, uliliboresha, uliwezesha kutunga kanuni mpya, uliimarisha Mhimili huu na kuuweka katika nafasi yake ya Kikatiba.
Nakumbuka siku moja ulimwomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aongee na baadhi yetu, ilikuwa mwaka 2006. Mimi nikiwa nina miaka 29 tu. Tukakutana na Rais ukumbi wa Msekwa. Baada ya kikao kilichofanikiwa kumshawishi Rais kuhusu mabadiliko uliyoyataka uliniambia;
“Babu, mimi sasa alasiri, ninyi ndio saa nne asubuhi. Nawawekea misingi tu na kuliweka Bunge katika nafasi yake ya kikatiba”.
Kilichofuata ni mabadiliko makubwa ya Kanuni za Bunge, kuandikwa upya kwa Sheria ya Bunge (National Assembly Administration Act, 2008) na kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Majimbo, Constituencies Development Catalyst Fund (CDCF).
Samwel Sitta, bado tunasikia mwangwi wa sauti yako nene kutoka kwenye kiti cha Spika ukiwataka Mawaziri wajibu maswali kwa ufasaha. Hukuisahau Tabora yako. Damu ya kichifu wa Unyanyembe ya Fundikira kutoka mama yako Zuwena ilikusambaa kwenye mishipa yako. Ukiona kuna swali linalohusu mkoa wako wa Tabora hukusita kuwaambia Mawaziri wajibu vizuri (haswa kuhusu barabara), au ukiamsha jeshi lako (akina Lucas Lumambo Selelii nk) wakisema “mheshimiwa Spika, wewe leo ukipata dharura Urambo unafikaje!”. Yote hiyo kutilia nguvu umuhimu wa maendeleo ya mkoa wako.
Wewe ni kielelezo cha Demokrasia ya Vyama vingi bungeni. Ulitoa nafasi kwa wabunge wote wa kambi zote ndani ya Bunge. Hatusemi hukubagua, la hasha, uCCM wako ulikuwa pale pale. Lakini walio wengi walishinda na walio wachache walisikika. Ndio Demokrasia hiyo.
Sitta ulikuwa Muungwana. Nakumbuka siku ile unamwomba radhi Mzee John Momose Cheyo katika kamati ya Uongozi (baada ya kuwa ulimtoa kwa makosa bungeni), eti msongo wa mawazo ulikujaa kwani watu wanapitapita Jimboni. Lakini uliwashinda. Unyenyekevu wako wa kuomba radhi unapokosea ni somo kubwa sana kwa Viongozi wengine tuliobakia.
Wabunge wenzangu, tunataka kumuenzi Spika wa Watu – Samwel John Sitta? Basi hakuna kumuenzi bora zaidi kama kuimarisha uhuru na heshima ya Bunge letu.
Tuendeleze Jahazi.
Samwel Sitta anakwenda kwenye nyumba yake ya milele akiongozwa na imani yake kubwa kwa Mungu na uzalendo wake usio na mawaa kwa nchi yake Tanzania. Angalau bado ataendelea kuwa nasi kwa kutuachia mafundisho makubwa kutokana na Maisha yake, mambo mema aliyoyafanya kwa nchi yetu, ndoto aliyoiishi ya Tanzania imara na yenye heshima, na malezi kwa viongozi wengi vijana aliowafunda na kuwalea kiuongozi.
Ni dhahiri umeishi maisha yako Babu. Kama isemavyo biblia, 2 Timotheo 4:7 “Nimepigana Vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda”.
Tangulia Spika wa Watu (The Peoples’ Speaker) Samwel John Sitta.
Mola akulaze pema.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Novemba 11, 2016
Dodoma