Mradi
wa kuweka mashine mpya za kisasa za kukagua mizigo katika Bandari ya
Dar es Salaam ambazo zina uwezo wa kusoma na kupeleka taarifa na picha
za mizigo mubashara kwenye mifumo ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari
(TPA) na Mamlaka ya Mapato (TRA) umekamilika.
Kukamilika
kwa mradi huo kunatokana na maagizo aliyoyatoa Rais John Magufuli kuwa
TPA na TRA zishirikiane kuendesha mashine za kukagua mizigo zinazotoa
taarifa na picha mubashara, pamoja na kufanya kazi pamoja ili
kuhakikisha Serikali haipotezi mapato na kupitisha mizigo haramu.
Kuwepo
kwa mashine hizo kutazisaidia TPA na TRA kubaini shehena zilizoko
kwenye makasha yanayofikishwa bandarini hapo kupelekwa na kutoka nje ya
nchi kama inawiana na nyaraka za mzigo huo; na hivyo kutozwa ushuru
sahihi kwa mzigo stahiki. Lengo la kufunga mashine hizo ni kuongeza
mapato kwa serikali.
Meneja
wa Mradi huo, Zhang Sheng alisema jana kuwa mradi huo umekamilika na
sasa wako katika hatua ya pili ya mafunzo na skana hiyo mpya inaweza
kutumika muda wowote mara baada ya kukamilisha mafunzo.
Kwa
mujibu wa Meneja huyo kutoka China, skana hiyo ina uwezo wa kusoma na
kupeleka taarifa na picha za mizigo mubashara kwenye mifumo ya TPA na
TRA kwa wakati mmoja bila kuchelewa. Kutokana na kukamilika kwa mradi
huo, TRA na TPA zimeanza kuwapa mafunzo watumishi wao namna ya kutumia
mashine hizo.
Jana
Watumishi 20 wa mamlaka hizo kutoka Dar es Salaam na Tanga walihudhuria
mafunzo yanayolenga kuwajengea uwezo ili wamudu kutumia skana hiyo
inayotumia teknolojia ya kisasa.
“Nazipongeza
Serikali za Tanzania na China kwa kuwezesha mradi huu kukamilika.
Tunatarajia mafunzo hayo yatawaongeza uwezo wafanyakazi, ufanisi wa
bandari pamoja na kuongeza mapato ya Serikali,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko wakati akifungua mafunzo hayo ya siku tano.
Aliwaagiza
washiriki kuhakikisha watakapokuwa wanafanya kazi katika mashine hizo
wahakikishe wanafanya tathmini ya mizigo inayoonekana katika kontena
kama ina taarifa sahihi kwa kulinganisha na nyaraka za kuagizia mizigo
husika.
Pia
aliwataka kuhakikisha nyara za Serikali, silaha haramu, dawa za
kulevya, bidhaa za mionzi na nyingine zisizofaa hazipitishwi bandarini.
Mkurugenzi huyo pia aliwataka watumishi hao kujifunza kufanya
matengenezo ya mashine hizo angalau kwa asilimia 50 kuliko kutegemea
wataalamu kutoka nje pekee.
Alisema
TPA na TRA watahakikisha waendesha skana wanajifunza kufanya
matengenezo kwa asilimia 100 ili kuondokana na gharama za kutumia
wataalamu kutoka nje.
Wakati
alipotembelea Bandari ya Dar es Salaam na kuzungumza na wafanyakazi wa
bandari hiyo, Rais alitoa miezi miwili kwa TPA kununua mashine nne za
kisasa za kukagulia mizigo bandarini.
Alitoa
agizo hilo baada ya kubaini kuwa kati ya mashine nne za ukaguzi wa
mizigo zilizopo, ni mashine mbili tu ndizo zinafanya kazi na hazina
uwezo wa kukagua mizigo yote inayotoka na kuingia nchini kupitia bandari
hiyo hali inayosababisha kutokuwepo kwa udhibiti wa uhakika wa
udanganyifu.
Awali
baadhi ya wafanyabiashara ambao sio waaminifu walikuwa wanatumia
udhaifu wa mashine za bandarini hapo kusema uwongo kuhusu shehena
inayokaguliwa bandarini hapo kwa lengo la kukwepa kulipa kodi stahiki.