Katika
hali ya kushangaza, jana Mwenyekiti wa soko la Mbande Mbagala katika
Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Mokiwa Hassani aliomba kupigwa risasi
mbele ya Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Paul Makonda baada ya kutuhumiwa
kutoza kiwango kikubwa cha fedha katika upangishaji wa vizimba sokoni
hapo.
Mwenyekiti
huyo alitoa kauli hiyo baada ya mkuu huyo wa mkoa kufika sokoni hapo
kwaajili ya kusikiliza kero zinazowakabili wananchi ikiwa ni siku ya nne
ya ziara yake katika manispaa ya Temeke.
Kufuatia
tuhuma hizo ikamlazimu mkuu wa mkoa kumsimamisha mwenyekiti wa soko
hilo Hassani ili kujibu tuhuma hizo ndipo alipotoa kauli hiyo na
kufafanua kuwa bei hiyo ya shilingi laki nne kwa kizimba ni makubaliano
kati yao na wananchi hao, pia fedha hizo zimetumika kwa ajili ya
kuendesha soko hilo, ambalo bado halijakabidhiwa kwa Halmashauri.
Kufuatia
utetezi huo ikamlazimu Mkuu wa Mkoa kutumia busara ambapo aliuagiza
mkuu wa wilaya ya Temeke Felix Lyaniva kusimamia uundwaji wa uongozi wa
soko hilo haraka mpaka kufikia mwezi Desemba kero zinazolikabili soko
hilo ziwe zimetatuliwa.